Bush apigia debe mkakati wake kuhusu Irak | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 04.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Bush apigia debe mkakati wake kuhusu Irak

Rais wa Marekani George W.Bush,alikwenda Irak siku ya Jumatatu,bila ya kuitangaza ziara hiyo hapo kabla.Inasemekana,huenda ikawa kuna uhusiano kati ya ziara hiyo na ripoti itakayotolewa juma lijalo na Mkuu wa Majeshi ya Marekani nchini Irak,Jemadari David Petraeus,juu ya maendeleo yaliyopatikana hadi hivi sasa nchini humo.

Rais Bush alipotembelea vikosi vya Marekani katika Wilaya ya Anbar nchini Irak,tarehe 3 Septemba 2007

Rais Bush alipotembelea vikosi vya Marekani katika Wilaya ya Anbar nchini Irak,tarehe 3 Septemba 2007

Hii ni mara ya tatu kwa Rais wa Marekani,George W.Bush kuitembelea Irak tangu kuiangusha serikali ya zamani ya nchi hiyo.Tarehe ya kufanya ziara hiyo imechaguliwa vizuri,kwani Septemba 3 ni Siku ya Wafanyakazi nchini Marekani.Kwa hivyo, hiyo ni siku iliyofaa kwa rais kuonyesha kuwa yeye yupo pamoja na wale wanaohudumia taifa kwa bidii.

Muhimu zaidi ni kuwa Bush alikwenda Al Anbar, ambayo ni wilaya iliyoshuhudia mapambano makali kabisa tangu Irak ilipovamiwa na Marekani katika mwaka 2003.Miji ya Fallujah na Ramadi ipo katika wilaya ya Anbar,ambako hupita barabara kuu inayojulikana kama “Barabara ya Mauti.“

Lakini kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi wa Marekani,sifa hiyo mbaya ya Anbar,sasa ni historia.Kwani tangu majuma kadhaa yaliyopita, kuna usalama katika wilaya hiyo,baada ya baadhi kubwa ya Waarabu wa madhehebu ya Kisunni,katika eneo hilo,kuanza kupigana bega kwa bega na majeshi ya Marekani,dhidi ya wanamgambo wa Al-Qaeda na kuwatimua waasi hao.Sasa,Wasunni katika wilaya ya Anbar,wanaaminiwa na Wamarekani,hadi kupewa silaha.

Lengo la ziara ya Bush katika wilaya hiyo na pia mkutano wake pamoja na wakuu wa Kiarabu wa makundi ya kikabila kutoka Al Anbar,ni kuonyesha kuwa utulivu unaweza kupatikana na vile vile mkakati wake unazaa matunda.Tangu mwanzo wa mwaka huu,Marekani imepeleka Irak wanajeshi 30,000 wengine kuimarisha usalama katika mji wa Baghdad na Wilaya ya Anbar.Uamuzi huo ulizusha mabishano makali kati ya Bush na Baraza la Kongress nchini Marekani.Bush anahitaji kuonyesha kuwa mradi huo umesaidia kuimarisha usalama nchini Irak.

Kwa hivyo juma lijalo,kamanda wa majeshi ya Marekani nchini Irak,Jemadari David Petraeus na Balozi wa Marekani mjini Baghdad,Ryan Cocker wanatazamiwa kueleza mbele ya Bunge la Marekani mjini Washington,maendeleo ya kisiasa na kijeshi yaliyopatikana nchini Irak.Ripoti hiyo inangojewa kwa hamu kubwa,licha ya kuaminiwa kuwa ni dhahiri kwamba itatoa sura nzuri.Kwa mujibu wa duru zinazoaminika,Jemadari Petraeus,hasa ataeleza mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya ya Anbar.

Rais Bush,wakati wa ziara yake ya ghafula nchini Irak,alikutana na Jemadari Petraeus na pia Balozi Crocker,kupigia debe mkakati wake kuhusu Irak.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com