Burkina Faso yapata rais mpya wa mpito | Matukio ya Afrika | DW | 17.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Burkina Faso yapata rais mpya wa mpito

Mwanadiplomasia Michel Kafando amechaguliwa kuwa rais mpya wa mpito Burkinafaso kuiongoza nchi hiyo kwa takriban mwaka mmoja kuelekea hatua ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, kufuatia kujiuzulu Blais Compaore.

Rais wa Mpito Burkina Faso Michel Kafondo

Rais wa Mpito Burkina Faso Michel Kafondo

Uteuzi wa waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Burkina Faso na balozi wa Umoja wa Mataifa, Michel Kafando unatarajiwa kumaliza wiki kadhaa za ghasia na maandamano, yaliomuondoa rais aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 27 Blaise Compaore, na kutoa nafasi kwa jeshi kudhibiti madaraka.

Hatua hii vile vile inakuja saa chache kabla ya muda wa mwisho uliotolewa na Umoja wa Afrika ulioonya kuwa nchi hiyo itawekewa vikwazo iwapo haitomchagua kiongozi wa mpito ifikapo siku ya Jumatatu.

Rais wa Mpito Burkina Faso Michel Kafondo , na balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Jean-Maurice

Rais wa Mpito Burkina Faso Michel Kafondo , na balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Jean-Maurice

Baada ya kuteuliwa, Michel Kafondo aliye na umri wa miaka 72 aliwaambia waandishi habari kwamba anatambua jukumu alilopewa ameshaona ukubwa wa kazi yake na kujua mipaka yake.

Kwa upande wake katibu mkuu anayesimamia mchakato huo wa kipindi cha mpito Ablasse Ouedraogo, amesema kipindi cha rais wa mpito kitamalizika wakati atakapopatikana rais kupitia uchaguzi unaotarajiwa kufanaika baadaye mwaka ujao.

"Rais wa serikali ya mpito anachukua nafasi ya rais wa Burkina Faso, ataheshimu katiba na pia mkataba wa serikali ya mpito. Muhula wakeutamalizika baada ya kuapishwa rais atakayepatikana kutokana na uchagzi mkuu," alisema Ablasse Ouedraogo,

Viongozi wa utawala wa mpito hawatoruhusiwa kugombea Uchaguzi Mkuu

Chini ya mpango huo rais wa mpito atamchagua Waziri Mkuu ama kutoka upande wa raia au jeshi atakayeongoza serikali ya mpito ya wajumbe 25.

Kiongozi wa raia pia ataongoza bunge litakalokuwa na viti 90 litakalojulikana kama baraza la kitaifa la mpito.

Rais aliyejiuzulu Burkina Faso Blaise Compaore

Rais aliyejiuzulu Burkina Faso Blaise Compaore

Kulingana na mpango huo hakuna mwanachama yeyote kutoka utawala wa mpito atjkayeruhusiwa kugombea katika uchaguzi wa Novemba mwaka 2015.

Awali saa kadhaa baada ya majadiliano, kundi la maafisa 23 wengi wao wakiwa raia walimchagua Kafando kuiongoza Burkina Faso kama rais wa Mpito.

Muandishi habari Cherif Sy na mwanasosholojia waziri wa zamani Josephine Ouedraogo pia walikuwepo katika orodha ya watu waliopendekezwa kuwania kuiongoza nchi hiyo ya Afrika. Hata hivyo Cherif Sy amempongeza Kafando kwa kuchaguliwa.

"Nampongeza kwa kupata imani hiyo,nadhani ni majukumu makubwa kwa sababu tuko katika kipindi cha mgogoro, na naamini atashirikiana na kila mtu kutimiza matarajio ya wanachi. Matarajio ya vijana waliojitolea kumuondoa Balaise Compaore. Vijana hao wana matarajio makubwa, ambayo yanahitaji majibu," aliema Cherif Sy.

Aidha Kafando, ambaye kwa sasa atalazimika kuthibitishwa na baraza la katiba, aliwahi kuwa balozi wa Burkina Faso katika Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka wa 1998 hadi mwaka 2011.

Pia aliwahi kuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Burkina Faso kuanzia mwaka wa 1981 hadi mwaka 1982. Maandamano makubwa yalifanyika Burkinafaso kupinga hatua ya Blaise Compaore kutaka kubadilisha katiba ili aendelee kuiongoza nchi hiyo baada ya miaka 27 ya utawala wake.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri Yusuf Saumu

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com