1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga: Frankfurt na Bremen wasaka mwelekeo mpya

2 Februari 2026

Kocha mpya wa Eintracht Frankfurt, Albert Riera, ameanza rasmi majukumu yake huku akiahidi kuiboresha timu na kuwarejesha wachezaji katika ubora wao.

https://p.dw.com/p/57vdC
Albert Riera na Jonathan Spector
Albert Riera akiichezea timu ya taifa ya Uhispania (Jezi Nyekundu) katika mechi dhidi ya USA, mwaka 2009.Picha: AP

Mchezaji huyo wa zamani wa Uhispania alisema alichojifunza katika maisha yake ya uchezaji ni kwamba kocha mzuri ni yule anayemfanya mchezaji kuwa bora zaidi, na sasa anataka kuleta falsafa hiyo Frankfurt.

Riera, mwenye umri wa miaka 43, anachukua nafasi ya Dino Toppmöller katika kikosi kilichotwaa Europa League mwaka 2022 lakini ambacho kwa sasa kinapitia kipindi kigumu, kikishika nafasi ya nane Bundesliga na kikiwa pointi nane nyuma ya nafasi za Ulaya.

Frankfurt hawajashinda mechi yoyote kati ya saba walizocheza mwaka 2026, wamefungwa mabao matatu katika sita kati ya hizo, na tayari wametolewa kwenye Ligi ya Mabingwa.

Akizungumza na gazeti la Bild, Riera amesema jukumu lake la kwanza si mbinu za uwanjani, bali kujenga imani na nidhamu ndani ya kikosi.

"Mkutano wa kwanza si kuhusu mbinu za mchezo. Ni kuhusu watu, kundi, nidhamu na kanuni. Kuangaliana machoni na kuaminiana,” alisema.

Utambulisho wake rasmi utafanyika Jumanne, huku mtihani wake wa kwanza ukiwa dhidi ya Union Berlin.

Bremen yajitafuta

Wakati Frankfurt wakianza ukurasa mpya, upande mwingine wa Bundesliga klabu ya Werder Bremen inaendelea kusaka kocha mpya baada ya kumtimua Horst Steffen kufuatia mechi 10 bila ushindi na kushuka hadi nafasi ya 15, moja tu juu ya eneo la kushuka daraja.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Bo Svensson na Bo Henriksen—wote raia wa Denmark—ndio wanaoongoza katika mbio za kuchukua nafasi hiyo. Sky TV imeripoti kuwa Bremen tayari wameanza mazungumzo na makocha hao.

Henriksen, 50, alifutwa Mainz mwezi Desemba licha ya kuiokoa timu hiyo dhidi ya kushuka daraja mwaka 2024 na kuipeleka Europa Conference League msimu uliofuata.

Svensson, 46, aliinoa Mainz kati ya 2021–2023 kabla ya kujiunga na Union Berlin kwa miezi sita, ambako aliachishwa kazi Desemba 2024 baada ya kupokea kipigo cha 4–1 kutoka Bremen.

Kwa sasa, Bremen wanajiandaa kwa safari ya Freiburg Jumamosi, huku Frankfurt wakianza maisha mapya chini ya Riera—ishara kwamba msimu wa Bundesliga unaendelea kuwa na misukosuko ndani na nje ya uwanja.