1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil kufanya duru ya pili ya uchaguzi

8 Oktoba 2018

Mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro atakabiliana na mgombea mwenzake wa sera za mrengo wa kushoto Fernando Haddad, katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais, iliyopangwa kufanyika Oktoba 28.

https://p.dw.com/p/369QQ
Brasilien Wahl 2018 | Bolsonaro erscheint nit zur Pressekonferenz
Picha: Getty Images/AFP/M. Pimentel

Mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro atakabiliana na mgombea mwenzake wa sera za mrengo wa kushoto Fernando Haddad, katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais, iliyopangwa kufanyika Oktoba 28. Kwenye matokeo ya awali ya duru ya kwanza ya uchaguzi huo, Bolsonaro aliongoza kwa takriban asilimia 46. 

Bolsonaro wa chama cha Social Liberal alipata takriban asilimia 46 ya kura katika duru ya kwanza, huku mpinzani wake Fernando Haddad kutoka chama cha Wafanyakazi, akimfuatia akiwa na chini ya asilimia 29 ya kura.

Na baada ya matokeo hayo, mwenyekiti wa chama cha Social Liberal Gustavo Bebianno alizungumza na waandishi wa habari, alinukuliwa akisema, ''Kimsingi ilikuwa kura milioni 50, kulikuwa tu na idadi ndogo ya kura zinazohitajika ili kupata ushindi katika duru ya kwanza. Chama cha PSL, na timu ya kampeni ya Jair Bolsonaro, tumejiandaa kwa ajili ya duru ya pili. Katika duru ya kwanza hatukuwa na muda wa kutosha kujinadi kwenye televisheni."

Matokeo ya duru ya kwanza yameongeza uwezekano kwamba Bolsonaro mwenye misimamo mikali ya kizalendo huenda akawa rais wa taifa hilo ambalo halijawa na serikali yenye nguvu ya siasa kali za mrengo wa kulia tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1985.

Brasilien Wahl 2018 | Stimmabgabe Fernando Haddad
Fernando Haddad, mgombea, chaguo la aliyekuwa rais wa taifa hilo Inacio Lula da SilvaPicha: imago/Xinhua/G. Bilo

Mpinzani wake Haddad, ambaye ni meya wa zamani wa Sao Paulo aliwaambia wafuasi wake baada ya mjadala uliofanyika jana usiku kwamba anahisi changamoto kubwa kufuatia matokeo hayo ya awali, ambayo aliyaeleza kuwa yanahatarisha demokrasia ya Brazil.   

Bolsonaro, kapteni wa zamani wa jeshi, amepigia debe ahadi yake ya kuchukua hatua kali dhidi ya machafuko na ufisadi, lakini pia kuusifia utawala wa zamani wa kiimla wa kijeshi, matamshi ya dharau dhidi ya wanawake na wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, lakini pia anataka kukabiliana na uhalifu kwa kudhoofisha udhibiti wa jeshi la polisi ambalo tayari liko katika hali mbaya.

Haddad, mwanasiasa wa sera za mrengo wa kushoto, anasimama badala ya aliyekuwa rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye hivi sasa anatumikia kifungo cha miaka 12 jela kwa tuhuma za rushwa, na kuzuiwa kugombea nafasi hiyo mapema mwaka huu.

Kampeni zake, ziliangazia malengo la kiasili ya sera za mrengo wa kushoto ya kupambana na hali iliyodumu kwa muda mrefu wa kukosekana usawa, kufuta mageuzi makubwa katika sekta ya ajira yaliyopitishwa mwaka jana pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu.

Mwandishi: Lilian Mtono/DW

Mhariri: Grace Patricia Kabogo