1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bomu laupiga uwanja wa ndege wa Goma, mashariki mwa Kongo

17 Februari 2024

Bomu limeupiga uwanja wa ndege wa mji wa Goma uliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mapema leo, wakati mapigano yakiendelea kupamba moto kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4cWpR
Vikosi vya kulinda amani Kongo vikiwa kwenye uwanja wa ndege wa Goma
Uwanja wa Ndege wa mji wa Goma ndiyo mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo Picha: Glody Murhabazi/AFP

Chanzo kimoja kutoka kwenye serikali ya mkoa wa Kivu Kaskazini kimethibitisha kuanguka kwa bomu kwenye uwanja huo.

Hata hivyo duru nyingine za upande wa usalama zimearifu kuwa ni mabomu mawili ndiyo yameushambulia uwanja huo wa ndege lakini "hakuna madhara yaliyotokea". Wataalamu wawili wametumwa kwenda Goma kuchunguza shambulio hilo lilifanywa kutokea wapi.

Mapigano makali yameongezeka katika siku za karibuni kuzunguuka mji wa kimakakati wa Sake ulio karibu na Goma, kati ya vikosi vya Kongo na waasi wa M23 ambao serikali mjini Kinshasa, Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi yanasema wanaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, madai ambayo Kigali inakanusha .