1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Binali achaguliwa kukiongoza chama tawala Uturuki

22 Mei 2016

Chama tawala nchini Uturuki Jumapili (22.05.2016)kimemthibitisha mshirika anayeaminiwa na Rais Receyp Tayyip Erdogan kuwa mwenyekiti wake mpya na kufunguwa njia ya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1IsdL
Picha: Reuters/U. Bektas

Chama tawala nchini Uturuki Jumapili (22.05.2016)kimemthibitisha mshirika anayeaminiwa na Rais Receyp Tayyip Erdogan kuwa mwenyekiti wake mpya na kufunguwa njia ya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Binali Yildimir amepata kura 1,405 kati ya 1,470 za wajumbe wa chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP) waliohudhuria mkutano wa dharura wa chama hicho.

Yildimir mwenye umri wa miaka 60 ambaye ni mwanachama muasisi wa chama hicho sasa atachukuwa nafasi ya Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu ambaye mapema mwezi huu alitangaza kujiuzulu kutokana na kutofautiana na Rais Erdogan.

Yildirim ambaye amegombea uongozi wa chama hicho bila ya kuwa na mpinzani anatagemewa kukubaliana zaidi na Erdogan ambaye anashinikiza mabadiliko makubwa ya katiba ambayo yatampa madaraka makubwa ya utendaji rais cheo ambacho ni cha heshima tu nchini Uturuki.

Kwa jadi wadhifa wa waziri mkuu nchini uturuki unakwenda kwa kiongozi wa chama kikubwa bungeni na Erdogan anatarajiwa kumtaka rasmi Yidrim aunde serikali mpya.

Erdogan amwagiwa sifa

Katika hotuba yake kabla ya kupigiwa kura Yildirim ametowa heshima zake kwa Erdogan kwa kusema kwamba "siku zote tumekuwa na fahari kusema kwamba sisi ni washirika wa Erdogan, hatima yetu ni moja na shauku yetu ni moja.Ameongeza kusema kwamba "Bw. Rais tunakuahidi kwamba shauku yako ni yetu, mapambano yako yatakuwa yetu na njia yako itakuwa yetu."

Wanachama waliohudhuria mkutano wa dharura wa chama tawala nchini Uturuki cha AKP mjini Ankara. (22.05.2016)
Wanachama waliohudhuria mkutano wa dharura wa chama tawala nchini Uturuki cha AKP mjini Ankara. (22.05.2016)Picha: Reuters/U. Bektas

Pia ameapa kutowa ushirikiano wake katika kuanzisha katiba mpya kwa kubadili mfumo wa kisiasa nchini Uturuki kuwa ule wa urais kuifanya hali ambayo ípo hivi sasa nchini humo kuwa ya kisheria.

Mapema katika ujumbe uliosomwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Erdogan kwa mara nyengine tena amesisitiza haja ya kuwepo kwa katiba mpya na mfumo mpya wa serikali na kusema kwamba anataraji huko mbele kutafanyika masahihisho ya mfumo wa sasa wa utawala wenye mkorogo. Wajumbe na maafisa wa chama walisimama wakati hotuba yake ikisomwa.

Erdogan amesema "Uhusiano wangu wa kisheria na chama cha AKP yumkini ukawa umemalizika siku alipokula kiapo cha urais lakini uhusiano wake wa mapenzi na chama hicho haukumalizika na katu hautomalizika"

Yidirim apongezwa na kukosolewa

Wafuasi wa Yidirim wanampongeza kwa dhima yake ya kuendeleza miradi mikubwa ya miundo mbinu ambayo imesaidia kuuchangamsha uchumi wa Uturuki na kuongeza umashuhuri wa chama cha AKP.Lakini wakosoaji akiwemo kiongozi wa chama kikuu cha upinzani wanamtuhumu kwa rushwa madai ambayo yanakanushwa na Yidirim.

Mwenyekiti mpya wa chama cha AKP Benali Yildirim (kushoto ) akiwa na Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu aliyejiuzulu wakati wa mkutano wa dharura wa chama cha AKP mjini Ankara. (22.05.2016)
Mwenyekiti mpya wa chama cha AKP Benali Yildirim (kushoto ) akiwa na Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu aliyejiuzulu wakati wa mkutano wa dharura wa chama cha AKP mjini Ankara. (22.05.2016)Picha: Reuters/R. Ozel

Mabadiliko ya uongozi wa chama hicho yanakuja wakati nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya Kujihami ya NATO ikikabiliwa na vitisho mbali mbali vya usalama ikiwa ni pamoja na kuanza upya kwa mzozo na waasi wa Kikurdi kusini mashariki mwa nchi hiyo, wimbi la mashambulizi ya kujitowa muhanga ya wanamgambo wa Kikurdi na Dola la Kiislamu halikadhalika kuongezeka kwa taathira kutokana na vita katika nchi jirani ya Syria.

Davutoglu ambaye aliwahi kuwa mshauri wa Erdogan na waziri wa zamani wa mambo ya nje alitafautina na rais katika masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuwa na mazungumzo ya amani na waasi wa Kikurdi na kesi ya waandishi wa habari wanaotuhumiwa kwa upelelezi na wanataaluma wanaotuhumiwa kuunga mkono ugaidi.

Katika hotuba yake ya kuaga Davutoglo amesema kujiuzulu halikuwa takwa lake lakinin alikubali kufanya hivyo kudumisha umoja wa chama.

Mwandisxhi : Mohamed Dahman

/AP

Mhariri : Yusra Buwayhid