BBC kwazidi kufukuta | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

BBC kwazidi kufukuta

Viongozi wa ngazi za juu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, wamejiuzulu ikiwa ni siku moja baada ya mwenyekiti wa shirika hilo kusema wanahitaji mageuzi ya kina kulikabili sakata la udhalilishaji wa watoto.

Makao ya BBC mjini London.

Makao ya BBC mjini London.

Helen Boaden, Mkurugenzi wa masuala ya habari na msaidizi wake Steve Mitchell wameachia ngazi siku mbili baada ya Mkurugenzi Mtendaji George Entwistle kufanya hivyo ili kubeba jukumu katika sakata la kurusha taarifa za uongo dhidi ya mwanasiasa mmoja zikisema kuwa anahusika na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto. Kitengo kinachoshughulika na mahusiano ya umma cha BBC hakikuweza kuthibitisha mara moja taarifa hizo lakini taarifa zilizopo kwenye mtandao wa shirika hilo zinasema kuwa kutakuwa na tamko baadaye siku ya Jumatatu.

Mkurugenzi wa masuala ya habari wa BBC Helen Boaden ambaye amejiuzulu siku ya Jumatatu.

Mkurugenzi wa masuala ya habari wa BBC Helen Boaden ambaye amejiuzulu siku ya Jumatatu.

Ni pigo lingine kwa BBC

Taarifa za kujiuzulu kwa viongozi hao ni pigo la hivi karibuni kabisa kwa shirika hilo ambalo limo matatani kutokana na mkasa huo wa udhalilishaji wa watoto pamoja na matatizo ya watangazaji wake katika kuripoti suala hilo.

George Entwistle ameachia nafasi yake Jumamosi iliyopita ikiwa ni miezi miwili tu tangu aipate ikiwa ni hatua ya kuwajibika kwa kurusha taarifa kwenye kipindi kimoja cha habari kinachoruka usiku cha Newsnight ambacho kwa makosa kilimtuhumu mwanasiasa wa zamani kuwa anahusika pia na vitendo hivyo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto.

Katika tamko lake kuhusu hatua hiyo George alisema: "Kutokana na ukweli kuwa mkurugenzi mtendaji pia ndiye mhariri mkuu na moja kwa moja anawajibika kwa taarifa zote na pia kwa kuzingatia dhana ya uandishi mbaya uliofanywa katika kipindi cha Newsnight siku ya Ijumaa tarehe 2 mwezi Novemba, nimeamua kuwa kitu cha busara kabisa kufanya ni kujiuzulu nafasi ya ukurugenzi mkuu."

Naibu Mkurugenzi wa habari wa BBC Steve Mitchell naye amejiuzulu.

Naibu Mkurugenzi wa habari wa BBC Steve Mitchell naye amejiuzulu.

Mkurugenzi kuendelea kulipwa

Entwistle atapata fedha kiasi cha paundi za Uingereza 450,000 sawa na dola za Marekani 715,000 kama mshahara wake wakati akiwa nje ya ofisi. Kitengo cha masuala ya fedha cha BBC kimesema kuwa malipo hayo ni muhimu kwa kuwa kiongozi huyo ataendelea na kazi katika kusaidia mipango ya uchunguzi katika sakata jingine la udhalilishaji wa watoto linalomkabili mtangazaji wa zamani wa shirika hilo marehemu Jimmy Savile.

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie akiwasili katika jumba la utangazaji wa shirika hilo.

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie akiwasili katika jumba la utangazaji wa shirika hilo.

Malipo hayo ya Entwistle yamekosolewa vikali na mbunge mmoja nchini humo ambaye anasema ni muhimu kuhoji kama fedha hizo ni halali kupewa mtu huyo.

Mhasibu wa zamani wa chama cha Conservativ katika serikali ya Margaret Thatcher kwenye miaka ya 80 ambaye ndiye aliyetuhumiwa kimakosa na shirika hilo Robert McAlpine amesema ataishitaki BBC pamoja na vyombo vingine vya habari kutokana na sakata hilo.

Mwandishi: Stumai George/DPAE/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com