1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaendeleza ubabe katika Bundesliga

3 Februari 2014

Bayern Munich haijatosheka yaiadhibu Frankfurt mabao 5-0 katika Bundesliga, na kufungua mwanya wa points 13, timu kongwe katika ligi ya Ujerumani Hamburg SV yateleza kuelekea eneo la kushuka daraja msimu huu.

https://p.dw.com/p/1B22x
Fußball Bundesliga 19. Spieltag FC Bayern München gegen Eintracht Frankfurt
Bayern Munich wakishangiria karamu ya mabao dhidi ya FrankfurtPicha: Getty Images

Bayern Munich inacheza katika ligi ya aina yake. Timu hiyo kutoka Bavaria ilipata ushindi wa kishondo jana Jumapili baada ya kuirarua Eintracht Frankfurt kwa mabao 5-0 na kujiimarisha zaidi kileleni mwa Bundesliga.

Kabla ya hapo FC Nürnberg ilipata ushindi nayo wa mabao 3-1 dhidi ya Hertha BSC Berlin ikiwa ni ushindi wake wa pili mfululizo msimu huu, baada ya kwenda nusu nzima ya msimu huu bila kupata ushindi.

Fußball Bundesliga 19. Spieltag Hertha BSC gegen 1.FC Nürnberg
Nürnberg wakifurahia bao dhidi ya Hertha BerlinPicha: Imago

Bayer Leverkusen inayoshika nafasi ya pili katika ligi hiyo imemaliza kipindi cha kupata matokeo mabaya kwa kuiangusha VFB Stuttgart kwa mabao 2-1 na kujihakikishia points tatu muhimu katika mapambano kuwania nafasi ya pili. Siku ya Ijumaa Borussia Dortmund ambayo iko nafasi ya tatu ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa mabao 2-1 dhidi ya timu inayoshika mkia katika Bundesliga ya Eintracht Braunschweig.

Sport Fussball Bundesliga Eintracht Braunschweig - Borussia Dortmund 19. Spieltag 31.01.2014
Braunschweig dhidi ya Borussia DortmundPicha: Bongarts/Getty Images

Wakongwe hatarini

Hali hata hivyo ni mbaya zaidi kwa upande wa wakongwe katika ligi hiyo Hamburg SV. Timu hiyo ilikubali kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Hoffenheim. Timu hiyo kongwe katika Bundesliga imekuwa wakati wote iliiwakilisha Ujerumani katika kiwango cha juu barani Ulaya , lakini sasa inazungumzia kujiokoa kutoka katika hatari ya kushuka daraja.

Tayari kuna minong'ono ya mazungumzo kuhusu kocha mpya mjini Hamburg. Katika miaka mitano iliyopita kumekuwa na mabadiliko mara 11 ya wakufunzi wa soka katika klabu hiyo kongwe ya Bundesliga.

Fußball Bundesliga 18. Spieltag Hamburger SV - FC Schalke 04
Wakongwe Hamburg SV dhidi ya Schalke 04Picha: picture-alliance/dpa

Mara kadha makocha hao hawakupewa nafasi ya kuendeleza falsafa zao za soka katika timu hiyo. Mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo Kreuzer hata hivyo amesema kuwa kocha wa sasa Bert van Marwijk ndie kocha sahihi kwa klabu hiyo , na pengine lizungumzwe suala lingine ambalo ni la uongozi.

Mara nyingi uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukihitaji timu kufikia nafasi ya juu na kufikia hadi namba sita , lakini matarajio hayo ni makubwa mno na timu inahatarisha uwezo wake na kujitumbukiza katika hatari ya kushuka daraja.

Kocha wa Hamburg Bert van Marwijk amesema kuwa kikosi chake hakina makini katika uchezaji.

UEFA EURO 2012 Portugal Niederlande
Kocha wa Hamburg SV Bert van MarwijkPicha: Reuters

"Kutokuwa makini, hili ndio tatizo letu: Tunatoa kirahisi nafasi za kufungwa mabao. Hili linapaswa kubadilika. Tunalazimika pia kuwa na uwezo wa kucheza mpira, kwa hisia. Tunapaswa kufunga mabao, na pia kuzuwia tusifungwe mabao. Na hilo hatulifanyi. Ni lazima niseme ukweli kwamba kwa wakati huu hilo hatuliwezi."

Nayo Schalke 04 imeilazimisha VFL Wolfsburg kukubali kipigo cha mabao 2-1 na kujipachika katika kundi la timu zinazowania kucheza katika Champions League msimu ujao, kwa kuchupa hadi nafasi ya nne. Kocha wa Schalke Jens Keller amesema kikosi chake kimeweza kufanikiwa kwa kupambana kiume.

"Nataka kusema kuwa kikosi changu , kimefanya kazi nzuri sana katika mpambano huu dhidi ya moja kati ya timu bora za Bundesliga. Na nimesema mara kadha kuwa ushindi huu umekuja wakati wachezaji wetu saba wa kikosi cha kwanza hawakuwepo, badala yake wachezaji sita wa kikosi cha pili walitumika. Na ndio sababu najisikia fahari mno kwa kazi walioifanya wachezaji na kushinda mchezo huu."

Borussia Monchengladbach ilicheezea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Hannover 96 ikiwa ni kipigo cha pili tangu kuanza kwa duru ya pili ya msimu wa Bundesliga mwaka huu.

Wakati huo huo mshambuliaji wa Hannover 96 Mame Biram Diouf amesema anatarajia kurefusha mkataba wake na timu hiyo, licha ya timu za Uingereza kuonesha nia ya kutaka kumsajili. Diouf mwenye umri wa miaka 26, anamaliza mkataba wake na kikosi hicho cha Hannover mwezi Juni mwaka huu. Kocha wa Cardiff Ole Gunner Solskjaer anaripotiwa kuwa alijaribu kumshawishi mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United kurejea katika Premier League wakati wa kipindi cha dirisha dogo la uhamisho mwezi uliopita.

Lakini Diouf sasa anataka kuurefusha mkataba wake na Hannover baada ya kuanza duru ya pili ya msimu huu vizuri.

CR7 Ronaldo

Katika ligi ya Uhispania La Liga Atletico Madrid ilichukua fursa ya kuteleza kwa viongozi wa ligi hiyo Barcelona nyumbani dhidi ya Valencia na kunyakua usukani wa ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Real Sociedad wakati Real Madrid ilizimwa na Athletic Bilbao katika sare ya bao 1-1.

Ronaldo Real Madrid 14.09.2013 Vertragsverlängerung
Cristiano Ronaldo CR7Picha: Reuters

Katika mchezo huo mshambuliaji maarufu wa Madrid Ronaldo maarufu kama CR7 alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika kipindi cha pöili kufuatia mvutano na mchezaji wa Athletic Bilbao.

Hata hivyo kocha wa Real Madrid , Carlo Ancelotti amemshutumu Carlos Gurpegi wa Athletic Bilbao kwa kuongeza chunvi katika tukio ambalo lilisababisha CR7 kuonyesha kadi nyekundu.

Mchezaji huyo ambaye ametawazwa hivi karibuni kuwa mchezaji bora duniani aliamriwa kutoka nje ya uwanja dakika 15 kabla mchezo kumalizika, akionekana kumpiga Gurpegi baada ya malalamiko yake ya kutaka penalti kukataliwa.

Huko nchini Uingereza Arsenal imerejea kileleni mwa Premier League , kwa muda hadi pale mchezo kati ya Manchester City na Chelsea utakapokamilika leo jioni(03.02.2014) , baada ya kuishinda nguvu Crystal Palace kwa mabao 2-0 jana Jumapili.

Bundi katika paa la Old Traford

Bundi lakini ameendelea kukita kambi katika paa la Old Traford , Manchester United msimu huu , baada ya kupata kipigo cha mabo 2-1 tena dhidi ya Stoke City siku ya Jumamosi na kuganda katika nafasi ya saba, points 15 nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Arsenal London.

Hata hivyo kocha wa Manchester David Moyes , "The chosen one", amesema hana wasi wasi wowote kuhusiana na jinsi timu yake inavyocheza licha ya kupokea kipigo cha nane katika msimu huu.

Amedokeza kuhusu mpira aliougusa Michael Carrick na kumwendea Charlie Adam na kufunga bao la kuongoza kwa Stoke na uwezo wa wachezaji wa kati wa Stoke City hadi kupata bao la pili ndio sababu ya kushindwa kwa United na kikosi hicho hakipaswi kusikitika sana kwa kushindwa huko.

Moyes amesema na hapa namnukuu: Nafikiri tumecheza vizuri, kwa hiyo sidhani suala la mchezo mbovu ni sahihi, Mwisho wa kumnukuu.

FC Everton Trainer David Moyes
Kocha wa Manchester United David MoyesPicha: Getty Images

Nchini Italia, Viongozi wa ligi hiyo Juventus Turin hawakuonesha dalili za kutosheka na ushindi wakati walipowazidi nguvu mahasimu wao wakubwa Inter Milan kwa mabao 3-1 jana na kuandika ushindi wao wa 11 nyumbani katika Serie A msimu huu. Napoli iliyoko katika nafasi ya tatu iliendelea kuburura miguu baada ya kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Atalanta.

Simba sports klabu ya mjini Dar Es Salaam imefufua mipango yake ya muda mrefu ya kuwa na uwanja wake binafsi. Timu kongwe za Simba na Yanga mjini Dar Es Slaam zinahangaika hivi sasa kupata viwanja vyao binafsi, lakini hadi sasa ndoto hiyo haijakuwa kweli. Ni timu moja tu nchini Tanzania ambayo ina uwanja wake binafsi mjini Dar Es Salaam , timu ambayo ilianzishwa miaka ya hivi karibuni inayomilikiwa na mfanyabiasha maarufu mjini Dar Es Salaam ya Azam FC. Afisa habari wa klabu ya Simba Asha Muhaji amesema katika mahojiano na DW kuwa Simba inataka kutengeneza kwa hivi sasa uwanja wa mazowezi pamoja na kulizungushia uzio eneo la uwanja huo ikiwa ni awamu ya kwanza ya mradi huo.

Na huko katika America ya kusini , mashabiki wamewavamia wachezaji wa klabu ya Corinthians, Wakorinto na kumshambulia mshambuliaji wa klabu hiyo Paolo Guerrero katika kituo cha mazowezi wakilalamika dhidi ya matokeo mabaya ya timu hiyo hivi karibuni.

Mario Gobbi amesema maandamano ya mashabiki yaligeuka kuwa ya ghasia na mashabiki walimkamata mshambuliaji huyo kutoka Peru na kumakaba shingo. Amesema baadhi ya wafanyakazi wengine wa klabu hiyo pia walishambuliwa siku ya Jumamosi baada ya mashabiki kiasi ya 100 kuingia katika viwanja vya mazowezi vya timu hiyo wakidai kupewa ruhusa ya kuzungumza na kocha na wachezaji.

Tennis, Davis Cup

Na katika mchezo wa tennis , nahodha wa timu ya taifa ya mchezo huo katika kombe la Davis Carsten Arriens amezomewa na mashabiki wa nyumbani mjini Frankfurt jana Jumapili licha ya kuiongoza timu yake katika ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya mabingwa mara tano wa kombe hilo Uhispania.

Sababu ya mashabiki kuchukua hatua hiyo ni kutokana na wachezaji maarufu wa tennis wa Ujerumani kujitoa katika kinyang'anyiro hicho kutokana na sababu mbali mbali.

Hii ilikuwa na maana kwamba mashabiki waliolipa kiasi cha euro 65 kuona mapambano ya wachezaji wawili wawili waliona pambano moja tu ambalo halikuwa na msisimko wowote, kati ya Daniel Brands na Roberto Bautista Agut wa Uhispania.

Na sasa ni michezo ya Olimpiki ya Sochi: Rais wa kamati ya olimpiki ya Kimataifa IOC Thomas Bach amesema usalama wa kutosha na ukosoaji wa Urusi kuhusu sheria ya kupinga ushoga havitachafua michezo hiyo ya Olimpiki mjini Sochi.

IOC Kandidat Thomas Bach
Mwenyekiti wa IOC Thomas BachPicha: Getty Images

Bach pia amerudia utetezi wake kuhusu matumizi ya Urusi katika michezo hiyo , akisema kuwa fedha hizo zinakwenda katika kufanyia mageuzi ya muda mrefu katika eneo hilo. Akizungumza na waandishi habari siku nne kabla ya ufunguzi wa michezo hiyo, Bach ameeleza matumaini yake kwa uwezo wa Urusi kuweza kutoa ulinzi kwa michezo hiyo huku kukiwa na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa wapiganaji wa eneo la kaskazini mwa eneo la Kaukasus.

Ngumi

Na kwa upande wa masumbwi , bingwa wa dunia wa ngumi za uzito wa juu Vladimir Klitschko atatetea taji lake dhidi ya Alex Leapai mjini Oberhausen , nchini Ujerumani tarehe 26 Aprili mwaka huu. Klitschko mwenye umri wa miaka 37, ambaye anashikilia mikanda ya WBO, WBA na IBF atatetea mataji yake hayo dhidi ya raia huyo wa Australia ambaye anapambana kuwania mataji ya kimataifa kwa mara ya kwanza. Leapai mwenye umri wa miaka 34, ameshinda mara 30 kati ya mapambano yake 37, akishindwa mara nne na sare mara tatu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe / ZR

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.