1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Ni nani Bassirou Diomaye Faye?

Saumu Mwasimba
26 Machi 2024

Rais Macky Sall ampongeza Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi baada ya Amadou Ba kukubali kushindwa kabla ya kutangazwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Jumapili.

https://p.dw.com/p/4e7jL
Bassirou Diomaye Faye
Rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: Luc Gnago/REUTERS

Mwanasiasa wa upinzani asiyejulikana sana nchini Senegal Bassirou Diomaye Faye ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais katika matokeo ya awali na kupongezwa na rais anayeondoka madarakani Macky Sall pamoja na wagombea wengine wa uchaguzi huo wa Jumapili.

Bassirou Diomaye Faye,mwenye umri wa miaka 44 ni mwanasiasa wa kambi ya upinzani ambaye hakuwa na umaarufu mkubwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi na aliachiliwa kutoka jela alikokuwa anashikiliwa pamoja na mshirika wake wa kisiasa Ousmane Sonko chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa rais.

Diomaye Faye kwahakika aliidhinishwa kugombea urais  na mwanasiasa Ousmane Sonko kwa niaba yake baada ya kukabiliwa na misukosuko mingi ya kisiasa.

Na hata jana baada ya matokeo kuonesha Bassirou Diomaye Faye ameshinda uchaguzi huo wa rais,Sonko aliwaambia wafuasi wake kwamba Bassirou ni yeye kwamaana ya kwanza alipo Bassirou ndipo alipo yeye.

 Bassirou Diomaye Faye,rais mteule Senegal
Bassirou Diomaye Faye,rais mteule SenegalPicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Aliinukia kwenye siasa chini ya kivuli cha umaarufu wa Sonko ambaye ni mwanamapinduzi anayepigania mshikamano wa Waafrika na ambaye aliyezuiwa kusimama kwenye uchaguzi huo wa rais.

Soma pia: Faye aahidi kuitawala Senegal kwa unyenyekevu na uwazi

Katika umri wa miaka 44 Bassirou anakuwa rais wa kwanza mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kutokea nchini Senegal.Ana shahada ya sheria, aliwahi kufanya kazi kama mkaguzi wa masuala ya kodi na hajawahi kushikilia nafasi yoyote ya kisiasa lakini ahadi yake kubwa aliyowapa Wasenegal ni kuwaletea mabadiliko.

Anajitambulisha zaidi kama sehemu ya wanasiasa wa kizazi kipya anayeamini katika uhuru wa kitaifa, kutumiwa kwa njia ya usawa kwa mali ya taifa hilo pamoja na kuleta mageuzi katika kile anachokiona ni mfumo wa sheria uliotawaliwa na rushwa na ufisadi.

Lakini wapinzani wake wanamtuhumu kuwa mwanasiasa anayeongoza kundi la wanaopenda majaribio,ambaye yuko tayari kufuata sera ambazo ni hatari kwa taifa hilo.

Kimsingi rais huyo mteule ameahidi kuipitia na kuijadili upya mikataba ya mafuta na uvuvi akisema haogopi kuanzisha sarafu mpya nchini Senegal itakayokuwa mbadala wa faranga ya CFA,hatua ambayo imepingwa na mpinzani wake aliyekabiliana nae katika uchaguzi huo wa rais Amadou Ba.

Siku moja baada ya Bassirou Faye na Sonko kuachiwa huru
Wafuasi wa Bassirou Diomaye Faye na Ousmane Sonko Picha: Abdou Karim Ndoye/REUTERS

Faye anatokea kwenye maisha ya kijijini,Muislamu kwa dini ambaye ana wake wawili alioonekana nao sambamba katika mkutano wake wa mwisho wa kampeini na aliwahi pia kuongoza chama cha wafanyakazi akipokea kijiti kutoka kwa mshirika wake Ousmane Sonko.

Kwa pamoja wanasiasa hao wawili walianzisha chama cha kisiasa cha PASTEF mnamo mwaka 2014 lakini baadae serikali ya rais Macky Sall ikakifuta chama hicho mwaka jana.

Na hata mwanawe mmoja wa kiume amempa jina la Ousmane kumuenzi mshirika wake huyo wa kisiasa. Na wote wawili walifungwa jela moja. Faye alishtakiwa kwa makosa chungunzima ikiwemo kuidharau mahakama mnamo mwezi Aprili mwaka jana na baadae Sonko akamfuata jela mwezi Julai baada na yeye kuhukumiwa kwa tuhuma za kuanzisha vuguvugu la kuihujumu serikali.

Wachambuzi nchini Senegal wakisimulia juu ya wanasiasa hao wawili,wanasema ni sawa na pande mbili za shilingi.