1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la seneti lamuondolea kinga Matata Ponyo

Amina Mjahid
6 Julai 2021

Ofisi ya Seneti DRC imemuondolea kinga ya  bunge, Seneta Augustin Matata Ponyo na kuidhinisha mashtaka dhidi yake. Anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha zilizokusudiwa kurudishiwa wafanyabiashara waliowekeza nchini Congo

https://p.dw.com/p/3w7Dj
Premierminister der DR Kongo Matata Ponyo
Picha: DW/S. Mwanamilongo

Katika mashtaka yaliyosomwa  mwendesha mashtaka mkuu wa korti ya kikatiba anathibitisha kuwa Matata Ponyo, Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliamuru kutolewa zaidi ya dola milioni 138 za Kimarekani, baina ya mwaka 2012 na 2013.

Fedha zilizokusudiwa kufidia wafanyabiashara wa kigeni ambao mali zao zilichukuliwa mnamo 1973 na 1974, kufuatia sera ya utaifishaji iliyowekwa na marehemu rais Joseph-Desiré Mobutu.

Lakini fedha hizo hazijawahi kuwafikia walengwa. Eveline Mulemangabo, mwanasheria hapa nyumbani anakubali uzito wa mambo anayotuhumiwa Matata Ponyo, ila anaamini  ni mhimu kusubiri vyombo vya sheria kufanya kazi.

Seneti ilipinga shtaka la kwanza lililowasilishwa na  mwendesha mashtaka mkuu dhidi ya Seneta Matata, kuhusiana na ubadhirifu wa fedha zilizoandaliwa kwa mradi wa kilimo wa Bukangalonzo.

Karibu dola milioni 250 za marekani zilipotea bila athari, wakati mradi huo ulikuwa chini ya usimamizi wa serikali ya waziri mkuu huyo wa zamani. Na sasa kwa kuwa kinga za Matata zinaondolewa, kesi ya Bukangalonzo lazima pia itajitokeza tena, kama ilivyoelezewa pia na Octave Nasena wa baa ya Kinshasa-Matete.

"Matata lazima ajieleze mwenyewe pamoja na wakili wake ambaye atamsaidia katika taratibu hizi mbili kuonyesha kutokuwa na hatia. Ikiwa hatafanya hivyo, hatia yake ndiyo itaonyeshwa na mwendesha mashtaka mkuu. Hapo matokeo ni kwamba kesi hiyo itafikishwa mbele ya Mahakama ya makuu," alisema Nasena

Ni jana Jumatatu ndiyo ofisi ya Seneti iliondoa kinga za bunge za Matata, baada ya kumsikiliza akisaidiwa na wakili wake, Michel Shebele, ambaye tulijaribu kuzungumza naye ila nguvu zetu zikagonga mwamba.

Jean Noël Ba-Mweze, DW, Kinshasa.