Bado serikali haijathibitisha kifo cha Rais Mutharika | Matukio ya Afrika | DW | 06.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Bado serikali haijathibitisha kifo cha Rais Mutharika

Ripoti kutoka vyanzo vya kitabibu zinasema Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi amefariki dunia baada ya kuugua maradhi ya moyo, bali hadi sasa serikali ya nchi hiyo haijathibitisha kifo hicho huku wasiwasi ukiongezeka.

Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika

Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika

Mwanzoni redio ya taifa ilikuwa imetangaza kwamba Mutharika, mwenye miaka 78, angelipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi, lakini kwa mujibu wa mashirika mbalimbali ya habari yaliyowanukulu madaktari waliomtibu kiongozi huyo, inaonekana alishafariki dunia wakati alipofikishwa hospitali.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Makamu wa Rais Joyce Banda, ndiye anayechukuwa nafasi ya kiongozi wa nchi, ingawa kuondolewa kwa Banda kutoka chama tawala hapo mwaka 2010 kunaweza kutatiza kipindi cha mpito.

Mutharika, aliyewahi kufanya kazi kama mchumi kwenye Benki ya Dunia, amekuwa akituhumiwa kwa kushindwa kuongoza na kutokuuendeleza uchumi wa nchi hiyo. Inasemekana alikuwa akimtayarisha mdogo wake, Waziri wa Mambo ya Nje Peter wa Mutharika, kuwa mrithi wake. Mara kadhaa, Peter amekuwa akionekana akikaimu wadhifa wa kaka yake anapokuwa hayupo.

Maandamano ya mwaka 2011 dhidi ya Mutharika mjini Lilongwe.

Maandamano ya mwaka 2011 dhidi ya Mutharika mjini Lilongwe.

Polisi katika mji mkuu, Lilongwe wameimarisha usalama, tangu tangazo la maradhi ya ghafla ya Mutharika ilipotangazwa hapo jana, huku wanajeshi wakionekana karibu na nyumba ya Banda. Bado vyombo vya habari vya serikali vinaendelea kutangaza kwamba rais huyo yuko Afrika ya Kusini kwa matibabu.

Kabla ya taarifa za kifo chake kusambaa, hali yake ilionesha kupata huruma za watu katika mji wa Blantyre, mji mkuu wa kibiashara wa Malawi, ambako wengi wanamuona kiongozi huyo kama sababu ya upungufu mkubwa wa mafuta, chakula na fedha za kigeni.

Baada ya kupokea taarifa ya kifo hicho, dereva mmoja wa teksi mjini humo akiwa kwenye msongo wa kusubiri mafuta, aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa "huenda mwisho wa mateso uko karibu."

Baada ya Mutharika kuchukuwa madaraka ya urais hapo mwaka 2004, uchumi wa Malawi uliimarika sana. Lakini licha ya uimarikaji huo uliochukua miaka saba mfululizo, mabishano ya kidiplomasia na mfadhili mkubwa wa Malawi, Uingereza, yalichangia kuirudisha nyuma nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Rais Bingu wa Mutharika Malawi katika jukwaa la uchumi duniani.

Rais Bingu wa Mutharika Malawi katika jukwaa la uchumi duniani.

Ukatwaji wa misaada ulipelekea kupungua kwa uingizwaji wa mafuta, chakula na madawa na kuporomoka kwa sarafu ya Kwacha ya nchi hiyo. Maandamano dhidi ya utawala wa Mutharika hapo mwaka jana yalikabiliana na ukandamizaji mkali wa polisi na kumalizika kwa vifo vya waandamanaji 20.

Waandamanaji walikuwa wanapinga kudorora kwa uchumi na pia tabia ya udikteta ambayo Mutharika alishukiwa kuanza kuwa nayo. Kupoteza kwake umaarufu nje ya nchi yake, kulikwenda sambamba na ugomvi baina yake na viongozi wenzake serikali, ukiwemo ule wa Makamo wa Rais, Joyce Banda, ambaye mwaka jana alimfukuza kwenye chama tawala, lakini akabakia na nafasi yake ya umakamo rais.

Uchaguzi mwengine ulikuwa unapangwa kufanyika nchini Malawi mwaka 2014.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Dahman