Arsenal mabingwa wa FA Cup England
2 Agosti 2020Alikuwa mshambuliaji Pierre Emerick Aubameyang ambaye anahusishwa na tetesi za kutaka kuihama timu hiyo, aliyepachika mabao yote mawili muhimu kwa ushindi wa Arsenal. Muda pekee ambao Pierre-Emerick Aubameyang alionekana kutokuwa na uhakika ni wakati ulipowadia kuchukua kombe hilo la FA.
Mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji huyo yalibadilisha muelekeo wa fainali hiyo kwa Arsenal na kufanikisha ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea siku ya Jumamosi katika fainali ya kwanza ya kombe hilo iliyochezwa bila mashabiki.
Vizuwizi kutokana na virusi vya corona vilikuwa na maana hakukuwa na mwanamfalme William katika uwanja wa Wembley kukabidhi kombe hilo katika kizimba cha mfalme katika uwanja huo maarufu duniani.
Kwa hiyo Aubameyang alilazimika kuchukua kombe hilo binafsi uwanjani hapo akiwa kama nahodha wa timu. Kwa kuchukua kitako cha kombe hilo pia, kilisababisha Aubameyang kudondosha kombe hilo.
"Nilimuona akitembea akiwa amechukua pia sehemu ya chini ya kombe hilo," mlinzi wa Arsenal Rob Holding alisema, "na ilikuwa kama, "Unahitaji kuondoa sehemu hiyo ya chini !"
Kombe hilo lilinyanyuliwa juu , wakati vikimwagika vikaratasi vya rangi ya dhahabu kwa kikosi hicho cha Arsenal katika uwanja ambao ulikuwa mtupu uwanja ambao una uwezo wa kusheheni mashabiki 90,000 baada ya fainali hiyo ya 139 ya mashindano hayo ya muda mrefu zaidi duniani katika mchezo wa kandanda.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape