1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ancelotti akasirishwa na kipigo dhidi ya Liverpool katika FA

Sekione Kitojo
6 Januari 2020

Kipigo cha Everton dhidi ya Liverpool chamkasirisha kocha Carlo Ancelotti , hasa kwa kuwa Liverpool iliweka kikosi cha vijana chipukizi tisa.

https://p.dw.com/p/3VmvD
FC Bayern Muenchen- Carlo Ancelotti
Picha: Imago/Sven Simon/F. Hoermann

Mwishoni  mwa  juma  hili ilirindima michezo  ya kombe  la  FA  ambapo  Crystal Palace imejiunga  na  orodha  ya vikosi  vya  Premier League  vilivyoyaaga  mashindano  hayo msimu huu   baada  ya  kupoteza  kwa  bao 1-0 dhidi  ya  Derby County katika  duru  ya  tatu  hapo  jana. Chelsea  iliishinda  Nottingham Forest  kwa  mabao 2-0 na  Sheffield United iliionesha  mlango wa kutokea  Fylde  na  kufikia  duru  ya  nne, lakini  Tottenham Hot Spur itabidi  kurejea  mchezo  wake  dhidi ya  Middlesbrough baada  ya kutoka  sare ya  bao 1-1.

Fußball TSG 1899 Hoffenheim v FC Bayern München - Bundesliga
Kocha wa Everton Carlo AncelottiPicha: Imago/Thomas Frey

Aston Villa  na  Brighton zilisalim  amri baada  ya  kuondolewa  katika  kinyang'anyiro  hicho. Leo Arsenal inapimana  nguvu  na  Leeds  United, wakati Tottenham  itabidi warejee uwanjani  kesho Jumanne  kuamua  nani  ni  nani  dhidi  ya Middlesbrough. Manchester United nayo  itarejea  uwanjani  kesho kuoneshana   kazi  na Wolverhampton  baada  ya  kumaliza mchezo wao  kwa  sare  ya  bila  kufungana.

Kocha wa Everton Carlo Ancelotti  anapanga  uchunguzi  wa  haraka kuhusiana  na  kikosi  chake  kilivyopata  kipigo  cha  kufadhaisha katika  kombe  la  FA  dhidi  ya  makinda  wa  Liverpool. Kikosi  cha Ancelotti  kilipoteza  nafasi  adimu  kushinda  mchezo  huo uwanjani Anfield  kwa  mara  ya  kwanza  tangu  mwaka  1999 wakati chipukizi mwenye umri  wa  miaka  18 Curtis Jones  alipoifungia  Liverpool bao  la  ushindi jana Jumapili  katika  mchezo  wa  watani  wa  jadi, Derby.

Großbritannien Fußball Premier League | Liverpool FC vs. Everton FC
Kocha wa Liverpool Juergen Klopp akiwa na mchezaji wa kati wa timu hiyo Nathaniel Phillips baada ya ushindi wa duru ya tatu katika kombe la FA.Picha: Getty Images/C. Brunskill

Klopp alifanya  mabadiliko ya wachezaji 9, akianza  na  kikosi chenye thamani  ya  pauni  milioni 43.9 , wakati Everton  kikosi  chake kina thamani ya  pauni  za  Uingereza  milioni 222. Everton haijashinda dhidi  ya  Liverpool  tangu  mwaka  2010, na  kuifanya  Derby  ya Merseyside kuwa  chungu  kwa  kocha  huyo  aliyetokea  Napoli Carlo Ancelotti, ambaye  yuko  tayari  kujadili  jinsi  wachezaji  wake walivyocheza.

Nae  mlinzi  wa  Manchester United  Harry Maquire  anaweza kukosa  pambano  la  nusu  fainali ya  kombe  la  ligi  mchezo  wa mkondo wa kwanza  dhidi  ya  Manchester City  baada  ya  kuumia katika  mchezo wa  kombe  la  FA  mwishoni  mwa  juma, amesema kocha  wa  timu  hiyo Ole Gunnar Solskjaer.