1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria kumchagua rais baada ya miezi 10 ya maandamano

Sylvia Mwehozi
12 Desemba 2019

Baada ya karibu miezi 10 ya mzozo wa kisiasa, Algeria inafanya uchaguzi wa rais ambao unapingwa vikali na waandamanaji wanaotaka uongozi mzima kujiuzulu na jeshi kuacha kujihusisha na siasa.

https://p.dw.com/p/3Ug7J
Wahl in Algerien 17.04.2014
Picha: picture-alliance/dpa

Jeshi ambalo ni mdau mkubwa wa kisiasa nchini Algeria, linauchukulia uchaguzi huo kama njia pekee ya kurejesha utulivu katika taifa hilo kubwa la Afrika na muuzaji mkubwa wa gesi asilia barani Ulaya likiwa na idadi ya wakaazi milioni 40.

Mapema asubuhi, kumeshuhudiwa utulivu kwenye vituo vya kupigia kura mjini Algiers, ingawa polisi walionekana kupiga doria mitaani. Jumla ya vituo 61,000 elfu vya kupigia kura kote nchini Algeria vilifunguliwa saa mbili asubuhi na vitafungwa saa 12 jioni huku matokeo yakitangazwa Ijumaa.

Hata hivyo waandamanaji ambao wameshiriki maandamano makubwa katika mji mkuu wa Algiers na miji mingine mikubwa kwa takribani miezi 10, wameapa kwamba watatusia kura ya Alhamis, ambayo wanadai imepangwa ili kuwabakisha viongozi wote waliopo madarakani. Wagombea watano wanaowania kuchaguliwa ni maafisa wa zamani waandamizi, wakiwemo wawili waliowahi kuwa mawaziri wakuu na mawaziri wawili wa kawaida.

Algerien Algier - Abdelaziz Bouteflika im Rollstuhl zur Wahl 2017
Abdelaziz Bouteflika wakati akipiga kura mwaka 2017Picha: Getty Images/AFP/R. Kramdi

Idadi ya wapiga kura watakaoshiriki uchaguzi wa rais inatarajiwa kuwa ndogo baada ya waandamanaji kupiga kelele za "hakuna kura", wakihimiza kususia kura na kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia. Yeyote atakayeshinda atakuwa na kibarua cha kutafuta kukubalika katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika, ambako raia wengi wanapinga utawala unaoungwa mkono na jeshi wakidai haufai, uliojaa ufisadi na ulioshindwa kudhibiti uchumi unaoyumba.

Maandamano yalizuka wakati Bouteflika alipotangaza mwezi Februari kuwa atawania muhula wa tano madarakani. Tangu wakati huo waandamanaji waliingia mitaani kwa zaidi ya wiki 40 za kutaka kuuvunja mfumo mzima wa uongozi uliotawala Algeria tangu ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1962.

Waandamanaji pia wameelekeza hasira yao kwa kiongozi wa kijeshi aliye na nguvu Luteni Jenerali Ahmed Gaed Salah. Hata hivyo kiongozi huyo amesisitiza kwamba uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa ikiwa ni njia pekee ya kurejesha serikali halali na kumaliza mkwamo wa kisiasa baina ya waandamanaji na serikali.