1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alama ya 'amani na upendo' yaweza kukuchongea

Mohammed Khelef
11 Januari 2017

Je, unajuwa kuwa kupiga picha ukiwa umeweka alama ya "amani na upendo" kwa kuonesha vidole viwili kunaweza kupelekea kuibiwa data zako muhimu?

https://p.dw.com/p/2Vce0
USA Dalai Lama beim National Prayer Breakfast 5.2.2014
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Utafiti mpya wa Taasisi ya Taaluma za Teknolojia ya Japan (NII) unazua mashaka juu ya pozi hili maarufu la kupigia picha, hasa miongoni mwa vijana na wanaharakati.

Hii ni kwa kuwa teknolojia ya kutambua alama za vidole inazidi kukuwa na kutumika katika kuwatambua watu, kama vile ambavyo sasa hutumika kwenye kufungia na kufungulia simu za mkononi, tablet au kompyuta.

Katika ulimwengu wa sasa, ambapo vifaa hivyo vimeundwa vikiwa na kamera zenye nguvu sana na mitandao ya kijamii ikiwa inatumiwa kutuma picha, kuna hatari kubwa sana ya data binafsi za mtu kuweza kuvuja na kuwafikia wengine.

Watafiti wa NII waliweza kunakili alama za vidole kwa kutumia picha zilizopigwa kwa kamera zilizo umbali wa mita tatu kutoka alipo mtu mwenyewe. 

"Kwa kuinua tu alama ya "amani na upendo" mbele ya kamera, alama za vidole vyako zinaonekana wazi kabisa," anasema mtafiti wa NII, Isao Echizen.

Mtafiti huyo alikiambia kituo cha televisheni cha Yomiuri nchini Japan kwamba "data za kwenye alama za vidole zinaweza kutengenezwa tena kwa kutumia miale mikali kwenye picha."

"Hili hata halihitaji teknolojia ya kiwango cha juu wala ya gharama kubwa sana. Mtu yeyote anaweza kuzinakili alama za vidole," unasema utafiti huo. 

Kwa sasa, taasisi ya NII imebuni ngozi laini inayoweza kuvishwa kwenye vidole na ambayo inaficha alama za mvaaji, lakini upatikanaji wa teknolojia hiyo hautakuwa rahisi hadi miaka miwili ijayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo