Al-Sissi ziarani Urusi, akutana na waziri wa ulinzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Al-Sissi ziarani Urusi, akutana na waziri wa ulinzi

Mkuu wa majeshi ya Misri Abdul-Fattah al-Sissi anakutana na waziri wa ulinzi wa Urusi mjini Moscow, katika ziara ya kwanza ya nje tangu alipomuangusha rais Mohammed Mursi.

Jemedari Adbul-Fattah Al-Sissi.

Jemedari Adbul-Fattah Al-Sissi.

Ziara hiyo ya ngazi ya juu inakuja huku kukiwa na ripoti kuhusu makubaliano ya silaha zenye thamani ya dola bilioni mbili, ambayo huenda yakapanua ushawishi wa Urusi kwa mshirika muhimu wa Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Wakati wa kuanza kwa mkutano wa leo na Jemedari Abdel-Fattah al-Sissi, waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alisema makubaliano ya kuiuzia Misri silaha ni moja ya ajenda za mkutano huo. Alisema watajadili masuala muhimu ya kijeshi na ushirikiano katika nyanja ya ufundi wa kijeshi, hali ya masuala hayo wakati huu na matarajio ya baadaye.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu.

Saudi Arabia, UAE wafadhili

Shoigi alisema Urusi inaamini kuwa Al-Sissi amefanikiwa kurejesha utulivu nchini Misri, na inaunga mkono juhudi zake za kupambana na ugaidi. Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Al-Ahram la nchini Misri, makubaliano ya silaha kati ya Misri na Urusi yatafadhiliwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ziara hiyo ya Al-Sissi imekuja karibu miezi mitatu baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov na waziri wa ulinzi Sergei Shoigu kufanya ziara mjini Cairo. Urusi imekuwa ikijaribu kutanua ushawishi wake nchini Misri, wakati ambapo uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani umeshuka kutokana na hatua ya jeshi kumuondoa rais Mohammed Mursi Julai mwaka jana, na ukandamizaji mbaya uliyofuatia mapinduzi hayo, ambamo mamia waliuawa na maelfu kukamatwa. Marekani imekuwa muungaji mkono mkuu wa kigeni wa Misri na mfadhili tangu miaka ya 1970.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Nabil Fahmy, ambaye amefuatana na Sissi katika ziara ya Moscow, aliupuuza uvumi wa mabadiliko makubwa katika sera ya kigeni wakati wa ziara ya ujumbe wa Urusi miezi mitatu iliyopita. Mwezi Novemba mwaka jana , shirika la habari la Urusi Interfax, liliripoti kuwa Misri imeonyesha nia ya kununua makombora ya masafa marefu ya Urusi , ndege za kivita aina ya MiG-29, helikopta za mapambano na silaha nyingine.

Rais wa Misri aliepinduliwa Mohammad Mursi akiwa kizimbani.

Rais wa Misri aliepinduliwa Mohammad Mursi akiwa kizimbani.

Mkuu wa shirika la ushauri kuhusu masuala ya usalama na ulinzi katika kitupo cha utafiti wa Ghuba kilichopo katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Mustafa al-Ani, alisema ununuzi huo utaonyesha uungaji mkono wa mataifa ya Ghuba kwa utawala wa Misri baada ya kuondolewa kwa Mursi.

Uhusiano wa enzi za Kisovieti

Misri imekuwa mpokeaji wa pili mkubwa wa msaada wa Marekani baada ya Israel, ikiwa ni njia ya kuendeleza mkataba wa amani wa mwaka 1979 kati ya Israel na Misri. Marekani ilisitisha mwezi Oktoba sehemu kubwa ya msaada huo wa karibu dola bilioni 1.5 kila mwaka, ambao kwa sehemu kubwa unakwenda kwa jeshi.

Urusi ilikuwa mshirika wa karibu zaidi wa Misri kwa miongo miwili kuanzia mwaka 1950, wakati muungano wa Kisovieti ulipoziunga mkono harakati za kiongozi mzalendo Gamal Abdel-Nasser kulifanya taifa hilo la kirabu kuwa la kisasa zaidi, na kuunda jeshi lililo na zana bora wakati wa kilele cha vita baridi na mgogoro kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape
Mhariri: Mohamed Adul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com