1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab waua 39, katika shambulizi Nairobi

22 Septemba 2013

Wanajeshi wa Kenya wanapambana na wanamgambo wa Somalia ndani ya jumba moja la maduka jijini Nairobi, baada ya watu waliokuwa na bunduki kulivamia jumba hilo na kuwauwa watu 39. Wengine 150 wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/19lit
Wananchi wakiokolewa kutoka ndani ya jumba lililovamiwa jijini Nairobi
Wananchi wakiokolewa kutoka ndani ya jumba lililovamiwa jijini NairobiPicha: Reuters

Maafisa wa Kenya wanasema operesheni kubwa zinaendelea huku polisi na wanajeshi wakipambana katika jaribio la mwisho la kufikisha kikomo makabiliano hayo yaliyodumu zaidi ya saa 18. Serikali ya Kenya imesema idadi kadhaa ya watu wasiojulikana wanashikiliwa mateka katika maeneo kadhaa ya jumba hilo la maduka la Westgate.

Shambulizi la kulipiza kisasi

Wanamgambo wa al-Shabaab wamesema shambulizi hilo lililofanywa katika jumba hilo linalomilikuwa na Israel ni hatua ya moja kwa moja ya kulipiza kisasi uvamizi uliofanywa na majeshi ya Kenya nchini Somalia, ambako majeshi ya Muungano wa Afrika yanapambana na wanamgambo wa kiislamu wenye itikadi kali. Msemaji wa al-Shabaab Sheikh Ali Mohamud Rage amesema katika taarifa kuwa walikuwa wameionya Kenya lakini ikapuuza, kwa kuendelea kuvamia ardhi yao kwa nguvu, huku wakiwaua raia wasio na hatia. Amesema wataendelea kufanya hivyo hadi Kenya itakapoviondoa vikosi vyake nchini Somalia. Rais Uhuru Kenyatta amesema katika hotuba kwa taifa iliyorushwa kwenye televisheni kuwa “yeye binafsi amewapoteza jamaa zake katika shambulizi hilo la Westgate” lakini akasema nchi hiyo imeweza kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi hapo awali, na hivyo watawashinda tena hao magaidi. Uhuru amesema, “nasema wazi kuwa tutawasaka wahusika hao kila mahali watakotorokea. Tutawapata. Tutawaadhibu kwa tukio hilo linalochukiza”. Aliongeza kuwa “ugaidi ni filosofia ya uwoga”.

Makabialiano ya risasi baina ya vikosi vya usalama na wanamgambo ndani ya jumba la Westgate
Makabialiano ya risasi baina ya vikosi vya usalama na wanamgambo ndani ya jumba la WestgatePicha: Reuters

Polisi ya Kenya imewataja wavamizi hao kuwa “kundi la kigaidi” la watu kama kumi. Jumba hilo la Westgate ni maarufu miongoni mwa Wakenya wa kipato cha juu pamoja na raia wa kigeni, na lilikuwa limejaa takribani wateja 1,000 wakati watu hao majambazi walipolivamia mwendo wa saa tano mchana jana Jumamosi (21.09.2013), wakarusha maguruneti na kuanza kumimina risasi kiholela. Saa chache baada ya makabiliano ya risasi, duru za usalama zilisema polisi na jeshi wamefaulu kuwazingira magaidi hao katika eneo moja na kufaulu kuwaokoa mamia ya wateja na wafanyakazi wa jumba hilo.

Raia wa Kigeni miongoni mwa walouawa

Watu wa kila umri ambao walionekana kushtuka walikimbia kila mahali kutoka ndani ya jumba hilo, wengine wakiwa wamewabeba watoto wao, na wengine wakitambaa karibu na ukuta ili kuepuka risasi za kiholela. Waliokuwepo wanasema wavamizi hao walizungumza kitu kama “Kiarabu au Kisomali”.

Mwanajeshi akishika doria nje ya Jumba la Maduka la Westgate, Nairobi
Mwanajeshi akishika doria nje ya Jumba la Maduka la Westgate, NairobiPicha: picture alliance/AP Photo

Ufaransa imethibitisha kuwa raia wake wawili ni miongoni mwa waliouawa katika kile ilichokilaani kuwa ni shambulizi la”uwoga”. Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper amesema Wacanada wawili, mmoja wao mwanadiplomasia, ni miongoni mwa waliouawa.

Marekani imesema raia wake ni miongoni mwa waliojeruhiwa, katika shambulizi hilo ambalo Ikulu ya White House imelaani na kulitaja kuwa ni la “kikatili”. Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni John Kerry amesema Marekani imetoa msaada kwa serikali ya Kenya ili kusaidia kuikabili hali hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague amesema bila shaka “kuna raia wa Uingereza ambao wamejikuta katika hali hiyo na hivyo watapaswa kujiandaa kwa habari zozote”. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anafuatilia shambulizi hilo kwa karibu na tahadhari, huku akililaani vikali.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo