1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya treni Cameroon yauwa watu 55

Bruce Amani
22 Oktoba 2016

Watu 55 wamefariki dunia na wengine takriban 600 wamejeruhiwa baada ya treni iliyokuwa imejaa watu kuanguka nchini Cameroon Ijumaa ilipokuwa ikisafiri kutoka mji mkuu Yaounde kuelekea mjini Douala

https://p.dw.com/p/2RY3R
Kamerun Zugunglück zwischen Douala Yaounde
Picha: DW/H.Fotso

Waziri wa uchukuzi wa Cameroon Edgar Alain Mebe Ngo'oo amesema mabehewa kadhaa ya treni hiyo iliyokuwa imejaa watu yaling'oka kutoka njia ya reli muda mfupi kabla ya kufika katika mji wa Eseka.

Watu wengi walilazimika kutumia usafiri wa treni hiyo ya kampuni ya Camrail kuelekea Douala baada ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa Alhamisi kusomba daraja muhimu na kukatiza usafiri wa magari. Kilichosababisha ajali hiyo bado hakijabainika lakini duru zinaarifu kuwa mabehewa zaidi yaliongezwa kwenye treni hiyo ili kubeba abiria zaidi. Baadhi ya waliojeruhiwa wako katika hali mahututi.

Shughuli za kuwaokoa manusura wa ajali ya treni Cameroon
Shughuli za kuwaokoa manusura wa ajali ya treni CameroonPicha: DW/H.Fotso

Mfanyakazi mmoja wa reli alisema kuwa kampuni hiyo iliongeza mabehewa nane kwa treni hiyo inayokuwa kwa kawaida na mabehewa tisa, ili kumudu idadi kubwa ya abiria waliotaka kusafiri. Maafisa wa reli waliiambia redio ya taifa kuwa treni hiyo ilikuwa na abiria 1,300 badala ya idadi yake ya kawaida ya watu 600.

Mwandishi wa habari wa Shirika la Reuters aliyekuwa akisafiri kwenye behewa moja karibu na sehemu ya mbele ya treni hiyo alisema alisikia mshindo mkubwa. "niliangalia nyuma na mabehewa yaliyokuwa nyuma yetu yaliacha reli na kuanza kubingiria. Kulikuwa na moshi mkubwa" alisema.

Mhudumu mmoja wa kampuni ya Camrail, ambayo inasimamiwa na kampuni ya Ufaransa ya Ballore akizungumza katika eneo la ajali alisema kuna miili ya wanawake, na watoto na kuongeza wafanyakazi wenzake watatu ni miongoni mwa watu waliofariki. Joel Bineli, abiria aliyekuwemo kwenye treni hiyo iliyoanguka aliambia Reuters kuwa kulikuwa na miili mingi iliyokatika vipande vipande kwenye barabara ya reli.

Camrail ilisema iliyatuma makundi ya watu kwenda katika eneo la ajali na kuwa waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini. Wengine walisafirishwa kwa magari hadi Douala. Barabara nyingi za reli katika Afrika Magharibi na Kati zina sifa ya ukarabati duni na kushindwa kukidhi kanuni za usalama. Matukio ya matreni kuwacha reli hutokea mara kwa mara.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Caro Robi