Afrika ya kati ; makubaliano yatiwa saini
13 Januari 2013Serikali na waasi wa muungano wa Seleka , ambao walisonga mbele katika mashambulizi yao hadi karibu na mji mkuu Bangui mwezi uliopita, wamekubaliana kuunda serikali ya mpito mwishoni mwa mazungumzo yao yaliyofanyika katika mji mkuu wa Gabon , Libraville siku ya Ijumaa(11.01.2013).
"Kiongozi wa nchi, ameondoa matumizi ya amri iliyotolewa Aprili 22, 2011, inayohusiana na kuteuliwa kwa serikali," imesema amri ya rais iliyosomwa katika televisheni ya taifa.
Waziri mkuu atimuliwa
Amri tofauti inaondoa uteuzi wa Faustin Archange Touadera, ambaye amekuwa waziri mkuu tangu mwaka 2008. Chini ya makubaliano ya amani , serikali mpya itaongozwa na mjumbe kutoka upinzani wa kisiasa na kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi wa bunge katika muda wa miezi 12 ili kuchukua nafasi ya bunge la sasa, ambalo linadhibitiwa na washirika wa rais Francois Bozize.
Kwa upande mwingine , waasi wamekubali kusitisha mapigano, na kuondoa kitisho kikubwa muongo wa Bozize kuwapo madarakani katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini, ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa na kumruhusu kumaliza kipindi chake cha sasa madarakani, ambacho kinamalizika mwaka 2016.
Waasi waonya
Hata hivyo , waasi wamesema kuwa wanaweza kuchukua tena silaha iwapo serikali itashindwa kutimiza orodha ya masharti yao katika makubaliano hayo, ikiwa ni pamoja na kuwaacha huru wafungwa wote wa kisiasa na kuondoa majeshi karibu yote ya kigeni yaliyoletwa ili kuliimarisha jeshi la nchi hiyo.
Seleka , muungano wa makundi matano tofauti ya waasi, yameanza mapigano mapema mwezi wa Desemba, wakimshutumu rais Bozize kwa kupuuzia makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2007 ambayo yaliahidi kutoa ajira na fedha kwa wapiganaji ambao wameweka silaha zao chini.
Nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na Chad, Gabon, Cameroon na Congo zimeweka maelfu ya wanajeshi wao kulisaidia jeshi la rais Bozize baada ya kushindwa mara kadha na kulilazimisha jeshi hilo kurejea nyuma karibu kilometa 75 karibu na mji mkuu Bangui.
Waasi hapo mapema walisisitiza kuwa kujiuzulu kwa Bozize ni moja kati ya masharti yao kwa ajili ya amani na kwamba rais huyo ambaye ametwaa madaraka katika mapinduzi ya mwaka 2003 yaliyoungwa mkono na Chad, analazimika kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.
Rais wa chad Idriss Deby, ambaye amehudhuria sherehe za utiaji saini makubaliano ya amani , amesema kuwa makubaliano hayo yanaonesha maridhio mazuri.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga