1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
19 Agosti 2022

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na uchaguzi mkuu wa Kenya. Hali ya nchini Mali na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika nchi za DR Kongo, Afrika Kusini na Rwanda.

https://p.dw.com/p/4FmTf
Kenia Nairobi | William Ruto gewinnt Präsidentschaftswahl
Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland limeandika juu ya uchaguzi mkuu wa nchini Kenya. Gazeti hilo linasema Raila Odinga bado hajakubali kushindwa. Hata hivyo linatilia maanani kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa amani katika kipindi kirefu nchini Kenya. Neues linasema bwana Odinga anakusudia kwenda mahakamani kupinga matokeo ambapo mshindani wake William Ruto alishinda kwa asilimia finyu. Odinga amesema matokeo ya uchaguzi yanapaswa kukubaliwa na makamishna wote saba wa uchaguzi lakini haikuwa hivyo kwa sababu wanne walikataa kuyapitisha matokeo hayo. Gazeti linasema sasa ni jukumu la mahakama ya juu kutoa uamuzi. Gazeti la Neus Deutschland linatilia maanani kwamba chaguzi za Kenya aghlabu zimekuwa zinaandamana na mivutano tangu mwaka 2002.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linasema William Ruto  ametangazwa kuwa rais mteule lakini mshindani wake Raila Odinga anaona vingine. Gazeti hilo linaeleza kuwa Ruto amekabidhiwa hati ya urais baada ya kushinda kwa kupata asilimia 50.5 ya kura. Süddeutsche linasema kiwango hicho kitatosha kumwezesha kuingia madarakani ikiwa mambo yataendelea kutulia na limemnukulu mtaalamu wa masuala ya katiba Bobby Mkangi akisema kuwa mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi ni mkuu wa tume ya uchaguzi tu.

Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba makamishna wanne waliokataa kuyatambua matokeo waliahidi kutoa maelezo zaidi lakini hawajatokea tena. Hata hivyo limamnukulu bwana Raila Odinga akisema kwamba mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati amekiuka katiba.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema katika makala yake kwamba Wafaransa wanaondoka na Warusi wanakuja. Gazeti hilo linazungumzia juu ya hali ya nchini Mali. Linaeleza kuwa askari wa mwisho wa Ufaransa waliondoka nchini Mali mapema wiki hii. Walivuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Niger.

Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa askari hao wa Ufaransa walikuwapo nchini Mali kwa muda wa miaka 9  wakipamabana na magaidi na kulinda usalama kwa jumla. die tageszeitung limemnukulu mtaalamu wa masuala ya kijamii Yacouba Dogoni akisema kuwa hapo awali Mali ilipendelea ushirika na Ufaransa lakini kwa sababu lengo halikufikiwa, Mali imetazama kwingineko yaani Urusi.

Mtaalamu huyo amesema Urusi sasa ni mlinzi mpya wa Mali. Gazeti linaeleza kuwa serikali ya Mali inadai kwamba Wafaransa wanawapa silaha magaidi na ndiyo sababu Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali aliomba kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama. Gazeti la die tageszeitung linasema idadi ya askari wa kukodiwa wa Urusi wanaoitwa Wagner haijulikani lakini hali ya uslama imezidi kuwa mbaya nchini Mali.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika nchi za Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo, Afrika Kusini na Rwanda. Gazeti linasema nchini Rwanda Blinken alikutana na rais Kagame pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Vincent Biruta. Walijadili hali mbaya ya usalama kwenye mpaka baina ya Rwanda na Jahmuri wa Kidemokrasia ya Kongo.

Frankfurter Allgemeine linaeleza kuwa kabla ya kuanza ziara nchini Rwanda waziri Blinken alielezea wasi wasi wake kutokana na ilichosema ripoti ya kuaminika ya Umoja wa Mataifa. Ripoti hiyo imeeleza kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa kundi la M23 nchini Kongo. Hata hivyo serikali ya Rwanda imekanusha madai yaliyomo katika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa. Gazeti linasema usalama wa raia huko mashariki mwa Kongo unahatarishwa kutokana na uwepo wa kundi hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amezitaka Kongo na Rwanda ziache kuyaunga mkono makundi ya waasi ya kila upande.

Mbali na mgogoro wa mashariki mwa Kongo waziri Blinken pia alizungumzia juu ya suala la haki za binadamu nchini Rwanda ikiwa pamoja na kufungwa jela bila ya haki, Paul Rusesabagina. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Rusesabagina aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela alikuwa mpinzani wa serikali ya Kagame. Gazeti linakumbusha kwamba alipatikana na hatia ya kuanzisha makundi yaliyokuwa na silaha ya kuipinga serikali. Gazeti linasema bwana Blinken pia alipata wasaa wa kutembelea kumbukumbu ya mauaji ya kimbari.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen