1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
14 Januari 2022

Wasiwasi juu ya mwandishi wa habari wa Uganda. Wanajeshi wa Ujerumani watakiwa waendelee kuwapo nchini Mali ni muhtasari wa matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii.

https://p.dw.com/p/45Xld
Uganda Autor Kakwenza Rukirabashaija
Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linaelezea wasiwasi juu ya mwandishi wa riwaya na mwandishi habari maarufu wa nchini Uganda, Kakwenza Rukirabhaija.Gazeti hilo linasema mwandishi huyo alikamatwa na maafisa wa ujasusi tarehe 27 mwezi uliopita. Die tageszeitung linatuarifu kwamba Kakwenza Rukirabashaija alichukuliwa kikuku kutoka nyumbani kwake na majasusi hao.

Sababu ni kwamba alithubutu kumkebehi Muhoozi Kainerubaga, mtoto wa rais na ambaye pia ni jenerali mmojawapo wa ngazi za juu nchini Uganda. Muhoozi Kainerubaga anawania kuwa rais wa Uganda. Kwa usemi mwingine anawania kumrithi baba yake, rais Yoweri Museveni. Mwandishi huyo Rukirabashaija anafahamika kuwa mtu mwenye mdomo usiokuwa na mfuniko. Amemwita mtoto huyo wa rais, mlafi na anachokijua kuwa mafanikio ni kupora mali za umma na kujilimbikizia nyota mabegani!

Gazeti la die tageszeitung linasema hii si mara ya kwanza kwa mwandishi huyo kuingia matatani. Hata hivyo hakubali kunyamaza kimya na ameandika riwaya juu ya mfumo wa ufisadi katika nchi ya kubuni. Gazeti la die tageszeitung limemnukulu mwandishi huyo Kakwenza Rukirabhaija akisema kuandika vitabu ni kosa barani Afrika kwa sababu viongozi wanafikiri mtu anaandika juu yao.

Weser-Kurier

Gazeti la Weser Kurier linazungumzia juu ya wanajeshi wa Ujerumani waliopo nchini Mali. Linasema wanasiasa nchini Ujerumani wanataka wanajeshi hao waendelee kuwapo nchini humo sababu Mali imewakaribisha mamluki wa Urusi. Hata hivyo linafafanua kwamba wanajeshi wa Ujerumani wako nchini Mali kama sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini humo. Gazeti la Weser Kurier limewanukulu wanasiasa wa Ujerumani wakisema kwamba litakuwa kosa kuondoka Mali haraka.

Wanajeshi wa Ujerumani 1300 wako nchini Mali na wanasaidia katika juhudi za kupambana na magaidi. Hata hivyo gazeti la Weser Kurier linatilia maanani kwamba uamuzi wa watawala wa kijeshi nchini Mali wa kuwakaribisha askari wa kukodiwa wa Urusi haujazifurahisha nchi za Umoja wa Ulaya. Gazeti hilo limemnukulu waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa  akisema kwamba warusi hawako nchini Mali ili kupambana na magaidi bali kwa ajili ya kuuimarrisha utawala wa wanajeshi.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche linazungumzia juu ya maradhi ya askari kupora mamlaka linasema wanajeshi hao wanajifanya kuwa waokozi lakini ukweli ni kwamba wanapora mamlaka kwa faida zao. Katika maoni yake Gazeti linakumbusha kwamba mnamo mwaka uliopita serikali tano ziliangushwa duniani na nne kati ya hizo ni barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia juu ya alichokiita janga la mapinduzi ya kijeshi. Gazeti hilo linasema kuongezeka kwa idadi ya serikali zinazoangushwa na wanajeshi barani Afrika ni jambo la kushtusha kwa sababu jumuiya ya kimataifa haina nguvu ya kuwaweka sawa wanajeshi hao. Hata hivyo linaeleza kuwa mapinduzi ya kijeshi ni dalili ya udhaifu katika nchi husika na aghalabu jutokea kwenye nchi zenye taasisi dhaifu au zenye viongozi wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi zao vizuri.

Gazeti linasema wanajeshi hao hujifanya kuwa wakombozi lakini baada ya muda mfupi shabaha zao za kweli zinadhihirika kama ilivyobainika nchini Guinea na Mali. Gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba nchini Sudan raia wamewekwa katika hali ya sintofahamu na  wanajeshi. Raia wanataka demokrasia lakini askari wanaelekea kwingine kabisa!

Neues Deutschland

Makala ya gazeti la Neues Deitschland inazungumzia juu ya masaibu yanayowakumba wakimbizi nchini Libya. Wakimbizi hao kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara wanakusudia kwenda  Ulaya. Gazeti la Neues Deutschland linafahamisha kwamba mamia ya wakimbizi hao walikamatwa kiholela mapema wiki hii nchini Libya.

Kwa mujibu wa gazeti hilo wapiganaji wa brigedi ya Yansour waliokuwa wamefunika nyuso zao waliwavamia wakimbizi hao  kwenye kitongoji cha Ain Zara katika mji wa Tripoli na kuwakamata. Gazeti limekariri taarifa zinatosema kuwa wakimbizi 600 walikamatwa mapema wiki hii kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Gazeti la Neues Deutschland linasema hii si mara ya kwanza kwa kadhia kama hiyo kutokea nchini Libya.

Mnamo miezi iliyopita wizara ya mambo ya ndani ya Libya ilitoa amri ya kuyabomoa makaazi ya wakimbizi katika mji wa Tripoli. Gazeti limemnukulu mkimbizi mmoja kutoka Ivory Coast akisema kwamba Libya inawafukuza wakimbizi. Gazeti la Neues Deutschland limewakariri wachambuzi wakisema kuwa waziri mkuu Dbaiba anafanya kampeni kwa kuwanyanyasa wakimbizi.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen