1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Mei 2021

Yaliyoandikwa juu ya Afrika kwenye magazeti ya Ujerumani ni pamoja na maafa yaliyowakumba watu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na mlipuko wa Volcano miomgoni mwa mengine.

https://p.dw.com/p/3u5zI
Bildergalerie | DR Congo | Ausbruch des Nyiragongo und Evakuierung von Goma
Picha: Hugh Kinsella Cunningham/Save the Children/Reuters

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung juu ya maafa yaliyowakumba watu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na kulipuka kwa volkano kwenye mlima Nyiragongo. Gazeti hilo linafahamisha kwamba watu kadhaa wamekufa na zaidi ya alfu 20 wengine wameyapoteza makazi yao karibu na mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Gazeti la die tageszeitung linasema hali bado haijatulia kutokana na kutokea kwa mitetemeko. Gazeti hilo limeripoti kwamba mitetemeko ya ardhi ipatayo 100 inatokea kila siku.

Pamoja na kuzungumzia juu ya maafa hayo yaliyosababishwa na milipuko ya volkano gazeti la die tegeszeitung pia limeangazia hatua iliyochukuliwa na serikali kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kuwaachisha kazi mameya wa miji mikubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini na kuwateua maafisa wa polisi kushika nafasi zao. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba serikali ya Kongo imechukua hatua hiyo licha ya kuwapo madai juu ya ufisadi miongoni mwa polisi.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linazungumzia juu ya matukio ya nchini Mali. Linasema kwa mara ya pili katika muda wa miezi tisa jeshi limetwaa tena mamlaka. Wakati huo huo gazeti la Die Welt linakumbusha kwamba wanajeshi wa Ujerumani wako nchini Mali kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo. Wanajeshi hao wa Ujerumani ni  sehemu ya jeshi la Umoja wa Ulaya linalolinda amani katika nchi hiyo ya Afrika magharibi inayopambana na  magaidi.

Kutokana na wanajeshi nchini Mali kutwaa mamlaka kwa mara ya pili mnamo muda wa miezi 9, miito inazidi kusikika nchini Ujerumani juu ya kuwandoa wanajeshi wake kutoka Mali. Gazeti la Die Welt pia limenukulu maoni mbalimbali ya mashirika ya kimataifa na viongozi wa dunia juu ya matukio ya nchini Mali. Limemnukulu rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema hatua iliyochukuliwa na wanajeshi nchini Mali ya kuiangusha serikali ya mpito ni jambo lisilokubalika.

Gazeti linasema hatua ya wanajeshi wa Mali imelaaniwa pia na Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika. Umoja wa Ulaya pia umewalaani wanajeshi wa Mali na kutaka viongozi wa kiraia warejeshwe madarakani. Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba wanajeshi wa Ujerumani wanatoa mafunzo kwa jeshi la Mali lakini linauliza jee hayo ni mafunzo ya aina gani yanayofungua njia inayoelekea kwenye kuziangusha serikali mara kwa mara?

Gazeti hilo limemnukulu mwakilishi wa wakfu wa Ujerumani Konrad Adenauer nchini Mali bwana Thomas Schiller akisema maji yamemwagika na hayazoleki. Bwana Schiller amesema hata ikiwa wanasiasa watarejeshwa madarakani, hawatafua dafu mbele ya wanajeshi.! 

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia kitendawili juu ya kiongozi wa magaidi wa Boko Haram Abubakar Shekau nchini Nigeria. Jee amekufa baada ya kujilipua? Gazeti linauliza. Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba magaidi wa Boko Haram wameleta madhara makubwa nchini Nigeria katika miaka ya karibuni wakiongozwa na Abubakar Shekau.

Linasema mara kadhaa kifo cha gaidi huyo kimevumishwa, kwa mfano mnamo mwaka 2016 ambapo jeshi la Nigeria lilidai kumuua Shekau. Hata hivyo baadaye alitokea kwenye video. Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba watu zaidi ya 40,000 wameuawa kutokana na mashambulio ya magaidi wa Boko Haram. Linasema watu nchini Nigeria wanauliza kwa nini serikali ilishindwa kumkamata katika muda wote wa miaka 11 iliyopita.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linatahadharisha juu ya hatari ya kutokea njaa kwenye kisiwa cha Madagascar na linaeleza kuwa Umoja wa Mataifa hauna fedha za kutosha ili kuweza kuwasaidia watu wa kusini mwa kisiwa hicho. Gazeti linasema sehemu hiyo imekumbwa na ukame usiokuwa na kifani katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Mvua haijanyesha kwa miaka mitatu.

Watoto kadhaa wameshakufa kutokana na utapiamlo. Gazeti linasema watu zaidi ya milioni moja wanahitaji msaada wa chakula. Neue Zürcher linasema hali ni ya kutatiza kutokana na uhafifu wa miundombinu. Linasema ni vigumu kuwafikia watu wanaohitaji misaada ya haraka. Gazeti la Neue Zürcher linasema kwa mujibu wa shirika la chakula duniani WFP, kiasi cha dola milioni 75 kinahitajika kwa ajili ya kuepusha baa la njaa kisiwani Madagaskar lakini mpaka sasa kilichopatikana ni dola milioni 23  tu. Gazeti la Neue Zürcher limepiga mbiu ya mgambo.Tunatumai jumuiya ya kimataifa itaitikia kwa haraka.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen