1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
21 Mei 2021

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mkutano wa viongozi 15 wa Afrika na Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa serikali ya Ethiopia kuahirisha uchaguzi na mzozo juu ya mwili wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/3tiFQ
Frankreich | Filipe Nyusi | Treffen mit Emmanuel Macron
Picha: Lafargue Raphael/ABACA/picture alliance

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung lililoandika juu ya mkutano wa kilele baina ya viongozi 15 wa Afrika na wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Paris. Mkutano huo ulifanyika baada ya kikao maalumu kilichofanyika kwa ajili ya kuisaidia Sudan kwa kuipunguzia mzigo wa madeni. Gazeti la die tageszeitung linasema mkutano wa kilele baina ya viongozi wa Afrika na wa Umoja wa Ulaya uliweka kipaumbele katika namna ya kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na mzigo wa madeni kwa kuzifutia madeni

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 bara la Afrika limerudi nyuma katika mapato jumla ya ndani. Linasema uchumi wa nchi za Afrika umeathirika vibaya kutokana na janga la corona.

Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linasema si wote waliohuduria mkutano huo waliokubaliana na njia hiyo. Waziri wa fedha wa Benin ameeleza kuwa kufutiwa madeni kunaandamana na hatari ya kuondolewa hadhi ya kuweza kupata mikopo.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya uamuzi wa Ethiopia wa kuahirisha tena uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao. Serikali ya Ethiopia imesema hatua hiyo imesababishwa na matayarisho hafifu. Neue Zürcher linakumbusha kwamba hapo awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita lakini uliahirishwa kutokana na janga la corona. Gazeti hilo linasema hii ni mara ya kwanza kwa waziri mkuu Abiy Ahmed kusimama mkabala na wapiga kura tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2018.

Gazeti la Neue Zürcher linakumbusha kwamba waziri mkuu huyo wa Ethiopia aliingia madarakani kwa kuonyesha matumaini makubwa miongoni mwa watu wake. Alijitokeza kama mtetezi mkubwa wa mageuzi. Gazeti hilo linasea ni kweli kwamba alichukua hatua kadhaa za kutia moyo ikiwa pamoja na kuleta mkataba wa amani na nchi jirani ya Eritrea na kwa ajili hiyo alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel. Lakini gazeti la Neue Zürcher linasema Abiy Ahmed amebadilika.

Mtazamo wake umekuwa wa mabavu,wanasiasa wa upinzani wa jimbo la Oromo bado wamo jela. Neue Zürcher linasema mgogoro wa jimbo la Tigray umetokana na uamuzi wa kwanza wa kuahirisha uchaguzi. Maalfu ya raia wamekufa kutokana na mgogoro wa jimbo la Tigray.

Die Zeit

Nalo gazeti la Die Zeit linatukumubusha juu ya mvutano wa muda mrefu kati ya Ujerumani na Namibia kuhusu mauaji ya halaiki ya watu wa makabila ya Nama na Herero yaliyofanywa na askari wa Ujerumani katika enzi za ukoloni nchini Namibia. Gazeti hilo linasema baada ya kuvutana kwa muda mrefu, Ujerumani na Namibia hatimaye zimefikia mkataba wa pembeni juu ya maridhiano. Gazeti la Die Zeit linasema Ujerumani inatambua ukatili waliofanyiwa watu wa Namibia enzi za ukoloni kuwa mauaji halaiki. Hata hivyo gazeti linasema bado pana utatanishi na hakuna kilichotiwa saini mpaka sasa. Hata hivyo gazeti hilo linafahamisha kwamba rais wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier atafanya ziara ya kihistoria nchini Namibia ambapo atapigiwa makofi ya kumlaki, lakini pia ataonyeshwa ishara za kumpinga!

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakamilisha makala yetu kwa kutupeleka Zimbabwe ambako mzozo juu ya mwili wa rais wa zamani hayati Robert Mugabe umezuka tena. Gazeti linatufahamisha kwamba baada ya mjane wa Mugabe, Grace kufanikiwa kumzika mumewe kwenye maziara ya familia, mahakama ya jadi imemwita mama huyo kutaka mwili wa Mugabe ufukuliwe ili ukazikwe kwenye kaburi lililopangwa kulingana na jadi ya kabila lake karibu na kaburi la mama yake na ndugu zake. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba hayati Mugabe mwenyewe hakutaka kuzikwa kwenye makaburi ya mashujaa baada ya jeshi lake kumwondoa madarakani mnamo mwaka 2017. Gazeti linasema mjane wake Grace Mugabe hatimaye alifanikiwa kumzika mumewe kwenye makaburi ya familia lakini sakata la mwili wa Mugabe bado linaendelea.

Vyanzo:Deutsche Zeitungen