1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
18 Desemba 2020

Yaliyoandikwa juu ya Afrika kwenye magazeti ya Ujerumani: Kampuni ya Facebook yazifunga akaunti za watu waliobainika kueneza propaganda. Mvutano wa kidiplomasia baina ya Kenya na jirani yake Somalia.

https://p.dw.com/p/3muIy
Symbolbild I Digitales Erbe I Facebook
Picha: picture-alliance/imageBROKER

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya uamuzi wa kampuni ya Facebook wa kuzifunga akaunti za watu wanaohusiana na jeshi la Ufaransa baada ya kubainika walikuwa wanaeneza propaganda katika nchi za Afrika. Kampuni ya Facebook ilitangaza uamuzi huo mapema wiki hii. Facebook imesema iliweza kubainisha mitandao mitatu iliyokuwa inatumia akaunti bandia na kuamua kuzifunga. Gazeti la Neue Zürcher linasema mara kwa mara ni wahusika kutoka Urusi na China wanaojaribu kushawishi mitazamo ya watu katika nchi za Afrika kwa kupitia kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo gazeti hilo linasema safari hii kampuni ya Facebook imezifunga akaunti za wafaransa wanaoeneza propaganda barani Afrika. Kulingana na taarifa ya gazeti la Neue Zürcher, nchi zilizolengwa katika operesheni hiyo ya propaganda ni pamoja na Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Niger, Burkina Faso, Algeria, Ivory Coast na Chad.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema wakati chanjo dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona imeanza kutolewa katika nchi tajiri, mataifa ya Afrika yatapaswa  kusubiri hadi kati kati ya mwaka ujao. Afrika Kusini pia itakuwamo katika kundi hilo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mara tu baada ya virusi vya  corona kulipuka nchini Afrika Kusini, rais Cyril Ramaphosa alichukua hatua kali ili kudhibiti maambukizi. Hata hivyo gazeti linasema, katika mbio za kuwania chanjo, Afrika kusini, nchi inayoongoza kwa nguvu za kiuchumi barani Afrika, pia itapaswa kusubiri katika mgao wa chanjo.

Mwenyekiti wa kikosi kazi nchini Afrika Kusini amenukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine akisema Afrika kusini haina raslimali za kutosha za kuiwezesha kuruka mstari katika ugavi wa chanjo hizo. Gazeti hilo llinatilia maanani kwamba Marekani, India na Umoja wa Ulaya zimeagiza dozi bilioni nne za chanjo dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Gazeti linafahamisha kwamba Afrika Kusini ndiyo inayoongoza barani Afrika kwa idadi ya watu waliokufa na walioambukizwa. Wanasayansi wa Afrika Kusini wameilaumu serikali kwa kushindwa kuchukua juhudi za mapema ili kuwasiliana na kampuni za dawa. Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hata baada ya kupatikana chanjo kati kati ya mwaka ujao ni asilimia 10 ya wananachi ambao kwanza watapatiwa chanjo hiyo .

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya mvutano wa kidiplomasia baina ya Kenya na jirani yake Somalia. Somalia imevunja uhusiano wake wa kibalozi na Kenya baada ya kiongozi wa Somaliland kufanya ziara nchini Kenya na kulakiwa kama mkuu wa nchi hiyo. Somaliland ni nchi yenye mamlaka ya ndani lakini kisheria inapaswa kuwa sehemu ya Somalia. Somaliland ilijitangazia uhuru mnamo mwaka 1991 baada ya kuangushwa kwa utawala wa Mohammed Siad Barre mnamo mwaka huo. Gazeti linaeleza kwamba tangu mwaka huo Somalia imetumbukia katika vurumai.

Gazeti la Süddeutsche linaeleza kuwa mpaka leo Somaliland haijatambuliwa kimataifa lakini ina serikali yake. Gazeti hilo linasema Kenya na Somalia zinavutana sasa juu ya hadhi ya Somaliland kwa sababu Somalia bado inaizingatia Somaliland kuwa sehemu yake. Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba mnamo mwezi Novemba Somalia ilimtimua balozi wa Kenya na ilimrudisha nyumbani balozi wake kutoka Kenya. 

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya wanafunzi waliotekwa nyara nchini Nigeria ambao sasa wameachiwa. Linasema kundi la kigaidi la Boko Haram limesema kuwa liliwateka watoto hao. Kiongozi wa kundi hilo la magaidi Abubakar Shekau amesema kundi lake lilifanya operesheni hiyo kwa lengo la kuendeleza uislamu na kuzuia vitendo vinavyokwenda kinyume na uislamu.

Wanafunzi hao zaidi ya 300 walitekwa nyara kwenye shule moja ya ufundi katika mji wa Kankara kwenye jimbo la Katsina la kaskazini mwa Nigeria. Gazeti la die tageszeitung linakumbusha kwamba hii ni mara ya pili kwa idadi kubwa ya wanafunzi kutekwa nyara nchini Nigeria. Mnamo mwaka 2014 magaidi wa Boko Harama  waliwateka nyara wanafunzi wasichana wa Chibok 276.

Gazeti la die tageszeitung linasema rais Muhammadu Buhari mara kwa mara amesema kuwa kundi la Boko Haram halipo tena lakini inalekea linaendelea kuwa na nguvu na ndiyo sababu limejitokeza na kusema kuwa ndilo lililowateka nyara wanafunzi hao.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen