1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Agosti 2020

Matukio ya nchini Mali ni miongoni mwa mambo yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya matukio na masuala ya barani Afrika.

https://p.dw.com/p/3hdV4
Mali Ibrahim Boubacar Keita
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Die Zeit

Tunaanza na makala ya gazeti la Die Zeit juu ya matukio ya nchini Mali. Gazeti hilo linauliza jee ni tukio la kushangilia kwamba jeshi la nchi hiyo limetwaa mamlaka? Gazeti la Die Zeit limemnukulu waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas akiwataka wanajeshi hao warejeshe utawala wa kisheria mara moja. Hata hivyo gazeti hilo linasema watu wa Mali hawamwelewi waziri huyo wa Ujerumani anapozumgumza juu ya utawala wa kikatiba, kwa sababu kwa muda wa miaka mingi utaratibu kama huo haukuwapo nchini Mali.

Gazeti la Die zeit linakumbusha kwamba kwa muda wa miezi kadhaa watu nchini Mali wamekuwa wanaandamana kumtaka rais Ibrahimu Boubacar Keita ajiuzulu. Die Zeit linasema Ujerumani na washirika wake wa Ulaya walifunga macho wakati Mali ilipoanza kwenda mrama. Gazeti hilo linasema pana kitendawili nchini Mali, jee sasa tufanye nini juu ya wanajeshi waliopindua serikali ambao wameshangiliwa kwa nderemo na wananchi?  Linatilia maanani kwamba ufisadi ulikithiri kwenye mji mkuu,Bamako wakati kwingineko nchini watu waliendelea kuwa masikini. Gazeti hilo linasema kwa sasa hali bado ni ya mkanganyiko nchini Mali, lakini hatua iliyochukuliwa na wanajeshi inatoa fursa ya kuleta mabadiliko kwa watu wa Mali na pia funzo kwa jumuiya ya kimataifa. Kwa muda wa miaka mingi washirika wa magharibi walifumbia macho ufisadi mkubwa uliokuwa unatendeka nchini Mali.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya habari za kufurahisha: maradhi ya kupooza, yaani polio yametokomezwa barani Afrika. Gazeti hilo limeinukulu taarifa ya shirika  la afya duniani WHO inayosema kwamba maradhi hayo ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yanawakumba watoto yametokomezwa kutokana na kampeni kabambe ya chanjo. Gazeti hilo linasema mafanikio hayo ni hatua ya kihistoria katika juhudi za kupambana na maradhi hayo duniani. Linatilia maanani kwamba virusi vya Polio vinawakumba hasa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na inachukua muda wa saa chache tu kwa virusi hivyo kusababisha ulemavu kwa mtoto. Linakumbusha kwamba mnamo mwaka 1996 watoto 75,000 walikumbwa na ulemavu barani Afrika. Neue Zürcher linafahamisha kuwa mamilioni ya watoto walipatiwa chanjo barani Afrika katika juhudi za kuutokomeza ugonjwa wa Polio.  

Berliner Zeitung,

Gazeti la Berliner linakumbusha juu ya tahadhari inayotolewa mara kwa mara na madaktari juu ya hatari ya kula nyama pori. Hata hivyo gazeti hilo linasema haitafaa kuwapiga watu marufuku kwa jumla kula nyama kama ya sokwe. Gazeti la Berliner limemnukulu daktari Fabian Leendertz kutoka taasisi ya Robert Koch inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza akibainisha kwamba maradhi mengi ya hatari yametokana na binadamu kula nyama pori. Daktari Leendertz amenukuliwa na gazeti hilo akieleza kwamba magonjwa mengi ya hatari yametoka kwa wanyama na kuingia kwa binadamu. Ametoa mfano wa maradhi ya UKIMWI.

Gazeti la Berliner linasema utafiti uliofanywa na madaktari wa Ujerumani nchini Ivory Coast umeionyesha kuwa watu nchini humo wanapendelea kula nyama ya panya wa aina mbalmbali. Limemnukulu mtaalamu mwengine, Mona Bachmann akisema ni muhimu kujua mengi juu ya aina ya nyama pori zinazopendelewa ili kuweza kuepusha hatari ya maambukizi. Hata hivyo mtaalamu huyo ameeleza kuwa halitakuwa jambo la busara kuwazuia watu kujipatia nyama kutoka kwa wanyama pori kwa sababu hatua kama hiyo itasababisha maradhi makubwa kwenye vyanzo vingine vya mahitaji ya nyama.

Der Tagesspiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel limeandika juu ya masaibu ya kijana mmoja kutoka Eritrea, Filimon Mebrhatom aliyeondoka nchini mwake akiwa na lengo la kuwa huru. Hata hivyo gazeti hilo linasema Mebrhatom alikumbana na misukosuko ya kila aina akiwa njiani kuelekea Ujerumani. Gazeti linasema kijana huyo ameandika yote yaliyomkuta katika kitabu chake. Gazeti la Der Tagesspiegel limenukulu sehemu ambapo anauliza kwa nini hakuna njia salama ya kufika barani Ulaya na kwa nini watu wa Ulaya hawayaoni masaibu yanayosababisha watu kuzikimbia nchi zao?

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba maalfu ya watoto wakimbizi wanakuja Ujerumani bila ya kusindikizwa na watu wazima. Der Tagesspiegel limenukulu sehemu ya kitabu ambapo Mebrhatom anasema hakupokewa kwa uchangamfu nchini Ujerumani. Alitambua kwamba watu wa barani Ulaya wanatofautisha binadamu, jambo ambalo hakutarajia kuliona. Filemon Mebrhatom ametambuliwa kama mkimbizi nchini Ujerumani lakini anasema katika kitabu chake kwamba yeye bado yumo njiani kama mkimbizi kwa sababu amepewa viza ya miaka mitatu tu nchini Ujerumani.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen

Mwandishi: Zainab Aziz