1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
24 Julai 2020

Aliyekuwa rais wa Sudan Omar al Bashir afikishwa mahakamani na bara la Afika lazingatiwa kuwa ni sehemu ya hatari kubwa kutokana na maambukizi ya corona ni mada zilizoandikwa juu ya Afrika kwenye magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3frfT
Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Hajaj

Süddeutsche

Makala ya gazeti la Süddeutsche inazungumzia juu ya hisia za kibaguzi. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba bara la Afrika, linazingatiwa kuwa sehemu ya hatari kubwa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti hilo linasema taasisi ya Robert Koch ya Ujerumani ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza imeziweka takriban nchi zote za Afrika kwenye orodha ya sehemu za hatari kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba nchi za Afrika ndizo zenye idadi ndogo kabisa ya maambukizi kulinganisha na sehemu nyingine yoyote duniani.

Gazeti hilo limetoa mfano wa Rwanda ambako mpaka sasa ni watu watano tu waliokufa miongoni mwa watu 1655 walioambukizwa virusi vya corona lakini taasisi ya Robert Koch imeiweka Rwanda katika orodha ya nchi za hatari kubwa! Süddeutsche linatilia maanani kwamba bara la Afrika lina watu bilioni 1.3 na kati ya hao ni laki saba na nusu walioambukizwa.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika juu ya aliyekuwa rais wa Sudan dikteta Omar al Bashir aliyefikishwa mahakani kwa mara ya pili kujibu mashtaka juu ya kupora mamlaka mnamo mwaka 1989 nchini Sudan. Gazeti hilo linakumbusha kwamba Omar al Bashir aliitawala Sudan kwa mkono wa chuma kwa muda wa miaka takriban 30. Gazeti la Süddeutsche linaeleza kuwa tangu mapema wiki hii al Bashir amesimamishwa kizimbani. Safari hii anakabiliwa na mashtaka ya kutwaa madaraka kwa mabavu baada ya kuiangusha serikali ya waziri mkuu Sadek al Mahdi aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba maalfu kwa maalfu ya watu waliuawa wakati wa utawala wa al -Bashiri. Gazeti hilo pia linakumbusha juu ya mauaji ya halaiki yaliyofanyika kwenye jimbo la Darfur chini ya uongozi wake. Frankufruter Allgemeine linatilia maanani kwamba Bashir amefikishwa hapo alipo kutokana na wimbi kubwa la maandamano ya kupigania demokrasia nchini Sudan. Maalfu ya watu walianza kuandamana kwenye mji wa Atbara mnamo mwaka 2018. Mwaka mmoja baadae wanajeshi walifanya uasi na kumwondoa al Bashir madarakani.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya maadhimisho ya siku ya Mandela nchini Afrika Kusini katika muktadha wa maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti hilo linaeleza kuwa iwapo angekuwa hai Mandela angelitimza umri wa miaka 102 tarehe 18 ya mwezi huu. Mnamo mwaka 2009, Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe ya kuzaliwa kwa Mandela kuwa siku ya maadhimisho ya serikali ya kwanza iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 1994.

Gazeti la die tageszeitung linasema badala ya mapumziko, serikali imewataka wananchi wote waiadhimishe siku hiyo kwa kufanya chochote kwa muda wa dakika 67 ili kupambana na umasikini na kupinga udhalimu. Kila dakika inawakilisha miaka 67 ya harakati za kisiasa za Madiba na miaka 27 kati ya hiyo ilikuwa ya kutumikia kifungo jela.

Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba katika miaka iliyopta siku ya Mandela iliadhimishwa kwa harakati mbalimbali nchini Afrika Kusini lakini gazeti linasema mambo ni tofauti mwaka huu siyo tu kutokana na janga la corona bali pia kutokana kifo cha binti yake Mandela Zindzi. Sherehe kuu safari hii ilifanyika kwa njia ya mtandao ambapo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  alitoa hotuba ya kutahadhrisha juu ya hatari  ya maambikizi ya Corona. Katika hotuba yake, Guterres alizumguzia juu ya tofauti kubwa za hali ya maisha zinazoonekana dhahiri wakati huu wa corona tofauti ambazo zimepuuzwa kwa muda wa miaka mingi.

Süddeutsche

Makala nyingine ya gazeti la Süddeutsche ni juu ya juhudi za nchi za Afrika magharibi za kuondokana na masimbi ya ukoloni wa Ufaransa. Nchi hizo ambazo zilikuwa makoloni ya Ufaransa zinataka kuanzisha sarafu ya CFA inayowafungamanisha na mkoloni wao wa zamani, Ufaransa. Lakini gazeti la Süddeutsche linasema mambo ni magumu kuliko ilivyotarajiwa. Sarafu hiyo ambayo bado inatengenezwa nchini Ufaransa ilianzishwa kwa ajili ya maslahi ya wakoloni wa kifaransa. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hata baada ya miaka 60 ya uhuru wa nchi za Afrika magharibi, sarafu hiyo inaendelea kuchapishwa Ufaransa.

Nchi nane za Afrika magharibi zilitaka kuanzisha sarafu mpya ya pamoja tarehe mosi mwezi huu a Julai lakini ilishindikana. Gazeti hilo linaeleza kwamba pana vizingiti kadhaa vilivyosimama katika njia ya kuazishwa sarafu mpya. Muhimu ni kutambua kwamba  chi zinazotumia sarafu hiyo pia zimo katika jumuiya kiuchumi ya Afrika Magharibi.

Nigeria imeziambia nchi hizo zisubiri kwanza. Mbali na tofauti hizo, wataalamu wamenukuliwa na gazeti la Süddeustche wakisema kwamba itakuwa vigumu kwa nchi za Afrika magharibi kujikomboa kisarafu madhali nchi hizo zimeweka sehemu ya fedha zao za kigeni kwenye benki kuu ya Ufaransa. Jambo la dhihaka ni kwamba tarehe ya kuanzishwa kwa sarafu hiyo ilitangazwa kwa pamoja mwezi Desemba mwaka jana na marais Emmanuel Macron wa Ufaransa na mwenzake wa Ivory Coast.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen