Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 12.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Yaliyoandikwa juu ya masuala ya barani Afrika kwenye magazeti ya Ujerumani ni pamoja na matukio ya nchini Sudan baada ya Rais wa nchi hiyo Omar Al-Bashir kuondolewa madarakani na jeshi lake.

die tageszeitung 

Kutokana na msimamo thabiti wa waandamanaji, hatimaye wanajeshi nchini Sudan wamembandua Omar al -Bashir kutoka kwenye kiti chake baada ya kutawala kwa muda wa takriban miaka 30. Jee huo ni ushindi wa wanajeshi? Aliyetangaza hatua ya kumwondoa al-Bashiri ni waziri wa ulinzi  Awad Mohammed Ibn Ouf alityeuliwa kuwa makamu wa rais mnamo mwezi wa Februari. Hakika yeye siye mtu wa kuzindua mwanzo mpya nchini Sudan! Waandamanaji wataendelea na harakati zao. 

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche pia limeandika juu ya matukio ya nchini Sudan. Gazeti hilo limemnukulu mtaalamu wa masuala ya siasa na aliyekuwa mwanadiplomasia wa Sudan, Abdelwahab al-Affendi akisema mabadiliko ya amani yanaweza kuletwa nchini Sudan na amekaririwa akieleza zaidi kwamba Sudan inahitaji utulivu wakati wa kipindi cha mpito ili kujenga mfumo kamili wa kidemokrasia. Hata hivyo njia ya kufika kwenye lengo hilo itakuwa ngumu, kwa sababu viongozi wengi waliomo madarakani sasa, ni wahalifu wakubwa na pia jeshi limegawika juu ya  Omar Al-Bashir.

Kölner Stadt Anzeiger

Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger wiki hii limeandika juu ya mradi wa bwawa la umeme kwenye mbunga ya hifadhi ya Selous nchini Tanzania linasema bwawa hilo litasababisha maafa makubwa. Barabara za mbunga hiyo iliyopo kusini mwa Tanzania zinaelekea  kwenye mto Rufiji ambako tayari sehemu kubwa iliyokuwa na miti imefyekwa. Kituo cha nishati ya umeme cha bwawa hilo litakalokuwa miongoni mwa miradi mikubwa kabisa barani Afrika kitakuwa na urefu wa mita 131.

Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linasema mradi huo wa kuzalisha nishati ni mwanaserere wa rais John Magufuli aliyepewa jina la utani la tingatinga lakini utasababisha madhara makubwa. Gazeti hilo linaeleza kwamba ujenzi wa mradi huo wa nishati ya umeme utaondoa rutuba ya ardhi kutokana na ukubwa wake wa kilometa za mraba 1200. Maziwa yatakauka na kusababisha ukame. Kuna hatari ya rutuba kuondoka kwenye bonde lote la mto Rufiji na kuathiri maisha ya wakulima na wafugaji 200,000. Mradi huo utakaozalisha megawati 2100 za umeme na kugharimu dola bilioni 3 unajengwa kwenye bonde la Stiegler ambalo limo katika orodha ya turathi za dunia. Hata hivyo serikali ya Tanzania inahoji kwamba mradi huo utakidhi mahitaji ya nishati ya umeme kwa wananchi wengi na mahitaji ya viwanda.

Neues Deutchland

Nalo gazeti la Neues Deutchland wiki hii limeandika juu ya mpango wa waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller juu ya kudhibiti uzazi na hasa katika nchi za Afrika kwa kutumia mbinu za kisasa. Wizara yake inakusudia kuongeza fedha kwa ajili ya mradi wa kuwapa wanawake haki zaidi.

Waziri Müller amesema Ujerumani itaongeza mchango wake wa fedha kwa ajili ya kusaidia juhudi za shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia afya ya uzazi. Amesema Ujerumani itachangia Euro milioni 33 kwa ajili ya mfuko wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa UNFP. Waziri huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa lengo la kuongeza juhudi za shirika hilo ni kuwapa wanawake haki zaidi ya kujiamulia wenyewe mipango yao ya uzazi.

Gazeti la Neues Deutschland limemnukuku waziri Müller akitanabahisha kwamba idadi ya watu barani  Afrika itaongezeka mara mbili hadi kufikia mwaka 2050. Kwa kasi hiyo Nigeria itashika nafasi ya tatu duniani kwa idadi kubwa ya watu, baada ya China na India. Gazeti la Neues Deutchland pia limemnukulu mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNFP, akifahamisha kwamba kwa wastani wanawake 800 wanakufa kila siku kutokana na matatizo ya ujauzito na wakati wa kujifungua. Mkurugenzi huyo Natalia Kanem amesema wanawake wapatao milioni 214 duniani wanataka kujipanga vizuri zaidi kuhusu uzazi.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen