1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
9 Februari 2018

Gazeti la Süddeutsche linahesabu siku za mwisho madarakani za rais Zuma wa Afrika Kusini. Der Tagesspiegel linafahamisha wakimbizi kutoka Afrika nchini Israel wanapaswa kuchagua kati ya kwenda jela au kufukuzwa nchini.

https://p.dw.com/p/2sPt1
Israel Flüchtlinge in Holot Haftanstalt
Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya misukosuko inayomwandama Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma. Gazeti hilo linasema kwa mara nyingine Zuma yumo matatani na huenda safari yake ya kisiasa ikafikia mwisho kabla ya kumalizika rasmi kwa muhula wake kabla ya kufanyika uchaguzi wa mwaka ujao wa 2019 gazeti hilo linaeleza.

Linaendelea kusema Zuma hataki kuachia ngazi licha ya shinikizo kubwa. Rais Zuma anatiwa vikumbo lakini hakubali kuanguka. Kwa mara ya kwanza ameahirisha hotuba ya kila mwaka inayotolewa na rais juu ya hali ya nchi. Na kutokana na wasiwasi wa kufanyiwa uchunguzi juu ya madai ya rushwa, Zuma anakusudia kung'ang'ania madarakani.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: Getty Images/S.Maina

Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba macho ya watu wote nchini Afrika Kusini yanaelekezwa kwa Cyril Ramaphosa kiongozi wa chama tawala cha ANC. Kwa muda wa wiki kadhaa Ramaphosa na viongozi wengine wa chama cha ANC wamekuwa wanafanya mazungumzo na rais Zuma kuhusu mustakabali wake.

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema swali sasa ni iwapo Zuma atang'tuka, au ataendelea kuwamo madarakani kwa muda wa miezi 16  ijayo ambapo muhula wake unafikia mwisho. Gazeti hilo pia limeandika juu ya Rais Jacob Zuma na linasema kwamba siku zake madarakani zinakaribia mwisho. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba kura ya kutokuwa na imani na rais Zuma imepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi huu na huenda kura hiyo ndiyo ikawa mwisho wa Zuma anayehofia kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Der Tagesspiegel

Maalfu ya vijana wa Kiafrika walioko nchini Israel kama wakimbizi, wanasubiri kufukuzwa au kufungwa jela. Hizo ni habari zilizoandikwa wiki hii na gazeti la Der Tagesspiegel. Gazeti hilo linasema Israel inataka wakimbizi hao waondoke nchini haraka na linaeleza jinsi wakambizi hao kutoka Eritrea na Sudan walivyosubiri hatima yao.

Wakimbizi wa Kiafrika walio katika kambi ya Holot nchini Israel
Wakimbizi wa Kiafrika walio katika kambi ya Holot nchini IsraelPicha: Getty Images

Mwanzoni mwa wiki iliyopita idara husika nchini Israel zilianza kutoa vitambulisho kwa ajili ya kuwafukuza wakimbizi 20,000 kati ya jumla ya wakimbizi 34,000 walio nchini humo. Haijulikani, kwa uhakika watu hao watapelekwa wapi, lakini baadhi ya vyombo vya habari vinasema huenda wakapelekwa Rwanda na Uganda. Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Der Tagesspiegel baadhi ya wakimbizi wanagoma kuondoka kwa sababu hawajui kinachowasubiri kule watakakopelekwa.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/F. Lenoir

Gazeti hilo limemnukuu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akisema yeye hawapingi wakimbizi walioingia nchini kwa njia halali. Hata hivyo akizungumza kwenye baraza lake la mawaziri Netanyahu alitamka wazi kwamba serikali yake itachukua hatua dhidi ya wakimbizi walioingia nchini kinyume cha sheria. Lakini gazeti la Der Tagesspiegel linafahamisha kuwa Waisreal wengi wamejitokeza kuupinga mpango wa serikali yao wa kuwafukuza wakimbizi.

Miongoni mwa watu hao ni wazee 36 walionusurika katika maangamizi yaliyofanywa na utawala wa Wanazi (Holocaust) wengine ni madaktari, marubani, viongozi wa kidini, waandishi riwaya na wasomi. Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine limewanukulu wazee hao 36 wakimkumbusha waziri mkuu Benjamin Netanyahu juu ya yale yaliyowafika wao walipokuwa wakimbizi. Watu hao wameuliza vipi serikali ya Kiyahudi inapanga kuwafukuza wakimbizi wanaoweza kujitosa katika safari za hatari?

Mlinzi wa wanyama pori aliyeuwawa Esmond Bradley Martin
Mlinzi wa wanyama pori aliyeuwawa Esmond Bradley MartinPicha: picture alliance/AP Photo/B. Inganga

Makala nyingine ya gazeti la Süddeutsche wiki hii inahusu habari za kusikitisha juu ya mlinzi mashuhuri wa wanyama pori Esmond Bradley alievamiwa na kuuawa huko nchini Kenya. Bradley alipambana na majangili ili kuwalinda ndovu na faru. Alifanya kazi yake kama askari kanzu kuwachunguza majangili waliokuwa wanauza pembe za faru na meno ya tembo duniani kote. Gazeti hilo linaeleza. Mmarekani huyo aliekutwa ameuawa nyumbani kwake karibu na jiji la Nairobi alikuwa na umri wa miaka 75. Alifanya kazi kubwa ili kuwalinda wanyamapori. Kwa mujibu wa taarifa, Esmond Bradley alivamiwa na kuchomwa visu.

Gazeti hilo la Süddeutsche linaeleza kwamba juhudi zake ziliwezesha kukibainisha kiwango cha biashara haramu ya vipusa iliyokuwa inafanywa nchini Marekani, Nigeria, Angola, China, Hongkong na katika sehemu nyingine za dunia. Gazeti hilo pia linasema walinzi wa wanyamapori wakati wote wamo katika hatari ya kuuawa. Tangu mwaka 2010, walinzi 1,000 wa wanyama pori wameshauawa duniani kote.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Grace Patricia Kabogo