YANGON : Kiongozi wa kijeshi kukutana na Suu Kyi kwa masharti | Habari za Ulimwengu | DW | 05.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

YANGON : Kiongozi wa kijeshi kukutana na Suu Kyi kwa masharti

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Myanmar ameweka masharti ya kukutana na kiongozi wa kutetea demokrasia nchini humo Aung San Suu Kyi wakati vikosi vya usalama vikiendelea kukamata watu na kuwasaili mamia wengine waliotiwa mbaroni katika msako mkali dhidi ya watu walioandamana kuipinga serikali.

Vyombo vya habari vya taifa vimeripoti kwamba Generali mwandamizi Than Shwe amedai kwamba Suu Kyi kwanza lazima aachane na wito wake kwa jumuiya ya kimataifa kuiwekewa vikwazo nchi hiyo na kwa wanaharakati wa demokrasia kukabiliana na utawala huo wa kijeshi.Repoti zinasema kiongozi huyo wa utawala wa kijeshi ametowa kauli hiyo kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari wakati wa ziara yake nchini Myanmar mapema wiki hii.

Zaidi ya watu 2,000 wametiwa mbaroni wakati wa kuvunjwa kwa kutumia nguvu maandamano ya kudai demokrasia wiki iliopita.Serikali inasema watu 13 wameuwawa wakati wa kuvunjwa kwa maandamano hayo wakati duru za kujitegemea zinasema idadi ya watu waliouwawa ni kubwa kuliko hiyo.

Mark Canning balozi wa Uingereza nchini Myanmar anasema ushahidi unadokeza kwamba kuna watu wengi mamia ya watu ambao wanashikiliwa mjini Rangoon na kwengineko.Hususan suala la mahala walipo watawa ni kitendawili na kwamba wameona ushahidi fulani kwamba kuna vituo kadhaa vya kuwashikilia watawa kwenye eneo la Rangoon.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kusikiliza repoti ya Gambari katika mkutano wa hadhara leo hii.

Wakati huo huo Radio Deutsche Welle imeongeza muda wa matagazo yake kwa Myanmar kufuatia serikali kuvunja maadamano ya kudai demokrasia kwa kutumia nguvu.

Matangazo ya saa moja kwa siku kutoka Idhaa ya Kingereza ya radio Deutsche Welle yataelekezwa kwenye nchi hiyo kwa kupitia kifaa maalum cha kurushia matangazo ya masafa mafupi kupitia stesheni ya kupokea matangazo ya Trincomalee nchini Sri Lanka.

Mkurugenzi wa Deutsche Welle Eric Bettermann amesema kwamba ikiwa ni sauti ya uhuru Deutsche Welle imekuwa ikifanya kazi kuhakikisha matangazo yake yanapokewa katika hali nzuri ya usikivu kwenye eneo hilo la mzozo.

Matangazo hayo yatasikika kila siku saa nne na nusu usiku saa za Yangon kwenye KHz 9485.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com