Yaliyoandikwa na wahariri hii leo nchini Ujerumani | Magazetini | DW | 01.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Yaliyoandikwa na wahariri hii leo nchini Ujerumani

Sheria ya kodi ya urithi inabidi ibadilishwe wanasema mahakimu wa Karlsruhe

Hukumu ya korti kuu ya katiba kuhusu kodi ya urithi,amri ya ofisi ya mwanasheria mkuu ya kukamatwa watuhumiwa 13 wa shirika la upelelezi la Marekani CIA wanaohusika na kisa cha kutekwa nyara El Masri na kuachishwa kazi kocha wa timu mashuhuri ya Bayern München ni miongoni mwa mada zilizomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Korti kuu ya katiba imeitaja sheria inayotumika hivi sasa ya kodi ya urithi kua ni kinyume na sheria.BÖRSEN ZERITUNG linaandika:

“Mahakimu wa Karlsruhe wamewavuta masikio watunga sheria.Wamepoteza wakati mrefu sana katika juhudi za kubuni sheria mpya ya kodi ya urithi ili kuachana na sheria inayotumika ambayo haiambatani na kanuni za usawa.Badala ya kutunga sheria mpya,imepatikana njia ya kutathmini thamani ya milki inayowafaidisha zaidi wenye majumba makubwa makubwa na makampuni.Hali hiyo sio tuu inakwenda kinyume na katiba lakini pia si bayana na madhara yake hayakadiriki.-linaandika BÖRSEN ZEITUNG.

Gazeti la Frankfurter RUNDSCHAU linaandika:”Kizazi cha enzi za baada ya vita hivi karibuni kitawarithisha watoto wao miliki kubwa kupita kiasi.Kwa mwaka miliki hiyo inatazamiwa kutuwama kati ya yuro bilioni moja hadi bilioni moja na nusu.Kuna miliki kubwa kubwa sawa na nyengine ambazo ni ndogo,majumba ya fakhari,sawa na nyumba nyenginezo ambazo ni ndogo tuu kuweza kuitosha familia moja.Suala hapa sio kwamba serikali inataka kujikusanyia fedha tu bila ya kutilia maanani tofauti iliyopo..Suala hapa ni kuondowa mapendeleo na dhulma katika aina zote za malipo ya kodi na kuleta hali ya usawa.Na hilo nijukumu la watunga sheria,sio kusubiri mpaka korti kuu ya katiba iwakumbushe-linaandika gazeti la Frankfurter Rundschau.

Gazeti la Münchener ABENDZEITUNG linaitia ila hukumu ya Karlsruhe na kuanadika:

„Kwa upande mmoja mahakimu wa korti kuu ya katiba mjini Karlsruhe wanakosoa hali ya kupendelewa wenye kumiliki majumba makubwa makubwa.Kwa upande wa pili lakini wanawataka watunga sheria wasake njia za wastani.Sasa watu wafuate njia gani?Wanasiasa wataitumia hali hiyo isiyo bayana ili kuzidi kubishana.SPD na vyana ndugu vya CDU/CSU toka hapo havina msimamo mmoja katika suala hilo.Uamuzi huo ni njia mojawapo pia ya kukusanya kodi za mapato toka kwa waliorithi majumba na makampuni.Waziri gani wa fedha angeyapuuza mabilioni katika wakati hguu ambapo makasha ya seerikali za majimbo ni matupu?

Mada nyengine magazetini inahusu kisa cha kutekwa nyara El Masri.Ofisi ya mwanasheria mkuu mjini München imetangaza sheria ya kukamatwa watuhumiwa 13 wa shirika la upelelezi la Marekani CIA wanaohusika na kisa hicho.Gazeti la SÄCHSICHE ZEITUNG linaandika:

„Hakuna anaeamini kama Marekani itaruhusu waletwe Ujerumani watumishi wa shirika lake la upelelezi.Hata hivyo kimoja ni hakika watuhumiwa hao hawataiona tena njia ya kuingi katika nchi yoyote ya Ulaya,seuze Ujerumani.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linakumbusha“ Mahakama ya Italy,tangu mwaka mmoja na nusu uliopita imepitisha amri kama hiyo.Kwa namna hiyo wanasheria wakuu wa Ulaya wanawaandama wamarekani karibu 40 wanaotuhumiwa kuwateka nyara,kwa amri ya serikali ya Washington watuhumiwa wa kigaidi , kuwahoji na kuwatesa kwa miezi kadhaa .Kwa kufanya hivyo wanasheria wakuu wa Ulaya wametaka kuwaonya washirika wao wa Marekani,visa kama hivyo vinavyokwenmda kinyume na sheria havitavumiliwa.“

Mada ya mwisho magazetini inahusu hatima ya makocha wawili wa timu za ligi kuu ya Ujerumani.Siku ya pili haikuwahi kumalizika tangu michuano ya ligi kuu kuanza upya baada ya mapumziko ya msimu wa baridi,na makocha wawili mashuhuri wamelazimika kufunga virago.Trena wa Borussia MÖNCHENGLADBACH Jupp HEYNECKES amejiuzulu,na muda mfupi baadae akatimuliwa kocha wa timu bingwa Bayern München Felix Magath.