1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Japan aomba radhi kwa kashfa ya rushwa

Angela Mdungu
30 Januari 2024

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida anaendelea kuomba msamaha kutokana na chama chake kukumbwa na kashfa kubwa ya rushwa, kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa nchini humo.

https://p.dw.com/p/4bqaM
Japan | Waziri Mkuu Fumio Kishida
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida akihutubiaPicha: Kyodo/AP Photo/picture alliance

Kishida amesisitiza kuwa dhamira yake ni kuepukana kabisa na rushwa wakati ambapo chama tawala chini ya uongozi wake kimo katika msukosuko unaodidimiza sera zake muhimu za kuimarisha jeshi na ushirikiano wa nchi yake na Marekani. 

Kiongozi huyo wa Japan alilazimika kuanza hotuba yake wakati wa kufungua vikao vya bunge vya mwaka huu kwakuomba radhibaada ya chama chake kukumbwa na moja ya kashfa kubwa zaidi za rushwa kuwahi kutokea nchini humo ndani ya miongo kadhaa.

Waendesha mashtaka nchini humo hivi karibuni waliwashtaki watu 10 wakiwemo wabunge na wasaidizi wa kisiasa.

Soma pia:Japan yajiunga na nchi nyingi za Magharibi kusitisha msaada wa fedha kwa shirika la kuwasaidia Wapalestina la UNRWA

Katika hotuba hiyo Kishida amesema  hana budi kukiri kuwa makundi ndani ya chama chake cha Liberal Democratic yameonekana kufanya kazi kwa misingi ya fedha badala ya sera na ameahidi kuongoza mageuzi ndani ya chama hicho.

Kishida hakutoa maelezo zaidi kuhusu kashfa ya rushwa iliyokikumba chama hicho au namna ya fedha zilivyotumika wakati vyama vya upinzani vikimshinikiza atoe maelezo. 

Ameongeza kuwa, anahitaji kuaminiwa tena na umma akitolea mfano changamoto kadhaa zikiwemo tetemeko baya lililotokea siku ya mwaka mpya pamoja na masuala ya uchumi.

Kishida: Tutaendeleza mahusiano yetu na Marekani

Waziri Mkuu Fumio Kishida ameahidi kuendelea kukuza na kuyatanua mahusiano ya Japan na Marekani aliyoyataja kuwa ni nguzo muhimu kwa sera za kidiplomasia za Japan ikiwemo kwa kukutana na Rais Joe Biden katika ziara mjini Washington  mwezi April.

Kiongozi huyo wa Japan amesema, Japan inahitaji kukuza zaidi uhusiano wake zaidi na Marekani ili kuimarisha usalama wa nchi yake na kusaidia kutimiza jukumu kubwa zaidi katika usalama na amani katika kanda.

Tokyo, Japan |Fumio Kishida na Lloyd Austin
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida akiwa na Waziri wa wa Ulinzi Marekani Lloyd AustinPicha: Eugene Hoshiko/AFP/Getty Images

Chini ya mkakati wa usalama wa taifa ambao uliopitishwa Desemba 2022, Kishida alitangaza mipango ya kuongeza mara mbii matumizi yake katika masuala ya ulinzi ndani ya miaka mitano, kwa ajili ya kuliongezea nguvu jeshi ikiwa ni pamoja na uwezo wa kushambulia wakati kukiwa na ongezeko la vitisho vya China na Korea ya Kaskazini.

Soma pia:Idadi ya vifo yaongezeka na kufikia 161 kufuatia tetemeko la ardhi Japan

Kishida hakutoa maelezo zaidi kuhusu namna serikali yake inavyopanga kupata fedha  za kufanya hivyo.

Takwimu zinakadiria kuwa, uungwaji mkono wa serikali ya Rais huyo wa Japan nchini humo umeshuka kwa asilimia 20.

Na wakati mhula wake wa uongozi ukitazamiwa kufupishwa, chama chake cha Liberal Democratic (LDP) huenda kikaendelea kukaa madarakanikutokana na vyama vya upinzani kuwa na mpasuko mkubwa na hivyo havionekani kuwa mbadala unaofaa.

Chama cha kishida na kashfa ya rushwa

Chama cha LDP kimekuwa kikitawala Japan baada ya vita bila ya usumbufu na  mara kwa mara kimekumbwa na kashfa za rushwa zikifuatiwa na ahadi za kubadilika na kufanya siasa safi.

Kashfa ya hivi karibuni inahusu fedha za chama zilizopatikana kutokana na tiketi zilizonunuliwa na watu binafsi makampuni pamoja na mashirika katika matukio ya chama.

Mapema Jumatatu, Kishida alikiri kuwa takriban wabunge 37 hivi sasa wanafanya marekebisho ya mahesabu ya mifuko fedha zao.

Soma pia:Marekani kuongeza misaada kwa waathiriwa wa tetemeko Japan

Wabunge wa chama tawala wanasema kuwa mapato yanayotokana na michango inayopatikana kutoka kwenye matukio ya kuchangisha fedha yanazalisha fedha muhimu zinazosaidia kufidia gharama za uchaguzina shughuli nyingine za kisiasa na wanakanusha kuwa wamezifisha au kuziweka kama mapato ambayo hawayaripoti.

Darasa la kutabasamu Japan

Hata hivyo wataalamu wanaeleza kuwa, Sheria inayodhibiti mapato ya kisiasa ina mianya mingi. 

Wakosoaji nao wanasema kuwa tatizo hasa siyo makundi ndani ya chama bali ni mambo yanayofanyika nyuma ya pazia ambayo mara nyingi yanategemea uhusiano wa wabunge ba wapiga kura katika majimbo yao ya uchaguzi.

Kishida hahitaji kuitisha uchaguzi wa bunge hadi mwaka 2025 lakini chama chake kimeshapanga kupiga kura ya kuchagua uongozi mpya mwezi Septemba