1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Waathirika wa mafuriko Tanzania wahitaji msaada wa haraka

11 Aprili 2024

Miito ya kutaka kuchukuliwa hatua za dharura na haraka kuwanusuru wananchi walioathirika na mafuriko huko Rufiji na Kibiti mkoani Pwani Tanzania, imeendelea kupazwa, huku mawaziri kadhaa wakielekea katika eneo hilo

https://p.dw.com/p/4eej4
Mafuriko Tanzania
Wito wa kupeleka misaada ya haraka watolewa kuwafikia waathirika wa mafuriko katika wilaya ya Kibiti na Rufiji nchini Tanzania Picha: Amas Eric/DW

Kuanzia wanasiasa, makundi yanayofuatilia ustawi wa jamii pamoja na wananchi wengine wa kawaida wamekuwa wakipaza sauti kutaka misaada ya haraka kuwafikia waathirika hao ambao baadhi yao wanaonyesha kukata tamaaa kutokana na mazingira wanayopitia.

Bado haijafahamika mara moja ni lini hali itatengamaa katika maeneo hayo na tayari serikali imesema imeanza kutuma watendaji wake kukagua uharibifu uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Hadi sasa wilaya nne zimefunikiwa na maji, na Waziri Mkuu Majaliwa anasema kutokana na uharibifu huo kuwa mkubwa, mawaziri kadhaa wamefunga safari kwenda kupinga kambi katika maeneo yaliyoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini na kisha kubainisha mahitaji yanayopaswa kuzingatiwa.

Takriban watu 47 wamekufa Tanzania kufuatia maporomoko ya ardhi

Samia asema serikali itaendelea kutoa msaada kwa waathirika

Rais Samia wa Tanzania
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Picha: Presidential Press Service Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa waathirika wa majanga hayo, na wakati alipokuwa akizungumza katika sherehe za Baraza la Eid Ul Fitr aliwahakikishia wakazi wa maeneo hayo kuwa serikali itaendelea kunyosha mkono wake ili kuwanusuru katika hali wanayokumbana nayo.

Hayo yanajiri huku mamlaka ya hali ya hewa nchini(TMA) ikionya kuhusu mvua kubwa inayotarajia kunyesha kuanzia kesho Ijumaa katika mikoa 14 na hivyo kuashiria uwezekano wa kutokea mafuriko na uharibifu katika maeneo mengi.

Mamlaka hiyo imesema mvua hizo zitanyesha katika kipindi cha siku tatu mfululizo na kwamba upo uwezekano na kushuhudia maafa katika baadhi ya maeneo.

Mwandishi: George Njogopa DW Dar es Salaam