1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maporomoko ya ardhi yaua watu 47 Tanzania

4 Desemba 2023

Takriban watu 47 wamekufa na wengine 85 wamejeruhiwa kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mafuriko katika mkoa wa Manyara kaskazini mwa Tanzania.

https://p.dw.com/p/4ZjR4
Tansania Überschwemmung in Daressalaam
Picha ikionyesha mafuriko yaliyotokea huko TanzaniaPicha: Said Khamis/DW

Hayo yameelezwa jana usiku na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga huku akionya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka.

Mkuu wa wilaya Janeth Mayanja amesema mvua kubwa ilinyesha Jumamosi katika mji wa Katesh, karibu kilomita 300 kaskazini mwa mji mkuu Dodoma. Mayanja ameongeza kuwa barabara nyingi katika eneo hilo zimezuiliwa na udongo, miti na mawe vilisombwa na mafuriko hayo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akihudhuria mkutano wa Umoja wa mataifa wa hali ya hewa wa COP28, ametuma salamu za rambirambi na kusema ameagiza kuwepo " juhudi zaidi za serikali ili kuokoa maisha ya watu".

COP28 | Tansanias Prädidentin Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Hali ya Hewa wa COP28 huko Dubai: 01.12.2023Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Picha zilizorushwa na kituo cha televisheni cha serikali TBC, zimeonyesha nyumba nyingi na magari yakiwa kwenye tope zito.

Baada ya kukumbwa na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa, kwa wiki kadhaa sasa eneo la Afrika Mashariki linakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na El Nino. Nchini Somalia, mvua hizo zimesababisha vifo vya mamia ya watu huku wengine zaidi ya milioni moja wakiyahama makazi yao.

Tukio kama hilo mwaka huu nchini Rwanda

Mwezi Mei mwaka huu, mvua kubwa iliyonyesha ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda na kusababisha vifo vya takriban watu 130.   

El Nino ni tukio la kiasili la hali ya hewa ambalo huanzia katika Bahari ya Pasifiki na huchochea ongezeko la joto duniani kote, na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo na mvua kubwa mahali pengine. Wanasayansi wanahofia kushuhudiwa kwa athari mbaya zaidi za El Nino mwishoni mwa mwaka 2023 hadi mwakani.  

Ruanda Regen Überschwemmung Katastrophe
Wakazi wakiokoa mali zao baada ya nyumba kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika wilaya ya Rubavu, mkoa wa Magharibi nchini Rwanda: Mei 3, 2023. Picha: JEAN BIZIMANA/REUTERS

Kati ya Oktoba 1997 na Januari 1998, mafuriko makubwa yaliyochochewa na mvua kubwa ya El Nino yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 6,000 katika nchi tano za eneo hilo.  

Wanasayansi wanasema matukio makali ya mabadiliko ya tabia nchi kama vile mafuriko, dhoruba, ukame na moto wa nyika yamekuwa makali zaidi na hushuhudiwa mara kwa mara na kwa muda mrefu zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayochochewa na shughuli za binadamu.

(AFPE)