1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Vita Sudan havionyeshi dalili ya kuisha miezi minne baadae

11 Agosti 2023

Miezi minne ya vita vya Sudan ambavyo pande zinazohasimiana zote zinaamini kuwa zitaibuka na ushindi, jeshi limepoteza udhibiti wa mji mkuu Khartoum kwa vikosi vya msaada wa dharura RSF wanaotuhumiwa kuwashambulia raia.

https://p.dw.com/p/4V4iZ
Athari ya vita vya Sudan kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya RSF
Jumba na gari lililoharibiwa kufuatia makabiliano kati ya jeshi na RSFPicha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Martha Pobee amesema vita hivyo vinaendelea kuiathiri nchi hiyo na raia wake na kusisitiza kwamba huu ndio wakati wa kuvimaliza vita hivyo na kurejea kwenye mazungumzo. 

Wakati vita vilipoanza mnamo Aprili 15, mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alikuwa na uhakika kwamba vita hivyo vingekamilika "ndani ya wiki mbili tu.”

Soma pia: Jeshi laelezwa kupata nguvu katika baadhi ya maeneo nchini Sudan

Makamu wake wa zamani aliyegeuka kuwa adui Mohamed Hamdan Daglo, ameapa kuwa vikosi anavyoviongoza vya RSF vitapata ushindi.

Hata hivyo, licha ya mahasimu hao wawili kujipiga kifua kwamba wataibuka na ushindi, hakuna hata mmoja anayeonekana kupiga hatua muhimu kuliko mwenzake huku vita hivyo vikigharimu maisha ya watu 3,900 na kusababisha zaidi ya watu milioni 4 kupoteza makao na kuzidisha uhaba wa chakula.

Sio hayo tu, vita hivyo vimezua madai ya kufanyika uhalifu wa kivita.

Wachambuzi waeleza mitazamo yao juu ya vita hivyo

Raia wengi wa Sudan wamekimbilia nchi jirani ikiwemo Chad
Mwanamke raia wa Sudan aliyekimbia vita katika jimbo la DarfurPicha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Mtaalamu wa usalama Mohammed Abdelkarim amesema jeshi lilipiga hesabu zao vibaya juu ya uwezo wa vikosi vya msaada wa dharura RSF.

Afisa wa zamani wa jeshi, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina ameeleza kuwa kwa upande wa RSF, waligundua kwamba vita hivyo vinaweza kuchukua muda mrefu na mara moja, wakachukua udhibiti wa maeneo ya mipaka ya kuingia na kutoka Khartoum na pia kuchukua laini za usambazaji wa bidhaa muhimu.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema vita hivyo vimewanasa mamilioni ya watu katika "janga la binadamu" na uwezekano wa mzozo mpya wa kikabila kuenea.

Ripoti iliyotolewa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Martha Pobee na mkurugenzi wa kitengo cha oparesheni wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa Edem Wosornu, imetoa taswira ya kutisha juu ya vita hivyo ambavyo havionyeshi dalili ya kumalizika.

Soma pia: HRW yaitolea wito Marekani kukomesha mauaji Darfur 

Bi Pobee ameeleza, "Mgogoro wa Sudan unaendelea kuwa na athari kubwa nchini humo na raia wake wanaendelea kukabiliwa na mateso yasiyofikirika. Mahitaji ya kibinadamu na usalama yanaongezeka kila siku, na hakuna ya dalili ya ahueni."

Mnamo mwezi Juni, serikali ilisema vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000, hata hivyo tangu wakati huo hakuna takwimu zozote zilizotolewa juu ya idadi ya wahanga.

Vita kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya RSF vimeendelea hasa katika mji mkuu Khartoum na miji ya karibu pamoja na eneo kubwa la magharibi la Darfur, ambalo linahusishwa na uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki miongo miwili iliyopita.

UN: Hakuna upande unaoelekea kupata ushindi

Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia baraza hilo kuwa hakuna upande wowote unaopata ushindi au kupata mafanikio makubwa kwenye vita hivyo, na kwamba raia wa Sudan wanakabiliwa na "mateso yasiofikirika.”

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan akiwa na wafuasi wake
Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Sudanese Armed Forces/AA/picture alliance

Bi Pobee ameelezea juu ya mashambulizi ya kiholela na wakati mwengine yakilenga raia na miundombinu ya kiraia, unyanyasaji wa kijinsia na watoto kuuawa, kudhulumiwa ama kuwa katika hatari ya kusajiliwa kama wapiganaji. Ameendelea kusema juu ya ongezeko la visa vya kutekwa na kuuawa kwa wanaharakati wa haki za binadamu mjini Khartoum na Darfur.

Soma pia: Jeshi la Sudan laendelea kufunga anga 

Pobee anayesimamia kitengo cha masuala ya kisiasa cha Umoja wa Mataifa kwa Afrika, ametoa wito wa kufanyika mazungumzo haraka iwezekanavyo kama suluhu ya vita hivyo.

Ametahadharisha kuwa kadiri vita vinavyoendelea, ndivyo hatari ya migawanyiko zaidi inavyoongezeka, uingiliaji wa nchi za kigeni na mmomonyoko wa uhuru na kupotea kwa mustakabali wa Sudan, hasa vijana wake.