1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan laelezwa kupata nguvu Khartoum

Sudi Mnette
9 Agosti 2023

Jeshi la Sudan limeripotiwa kupata nguvu zaidi katika maeneo ya mji mkuu wa Khartoum na baadhi ya maeneo mengine yenye mapigano makali, tangu kuzuka mgawanyiko jeshini ambao umesababisha ongezeko la janga la kibinaadamu.

https://p.dw.com/p/4Uwi7
Sudan Khartum | Rauch und Flammen in Omdurman
Picha: REUTERS

Wakazi wanasema tangu Jumatatu jeshi limefanya mashambulizi ya angani na kuvurumisha makombora ya mizinga, kwa jaribio la kutaka kulidhibiti daraja moja linalokatisha katika eneo la Mto Nile, ambalo kwa kawaida linatumiwa na wapiganaji pinzani wa kikosi cha kukabiliana na matuko ya dharura (RSF), ambacho kinalitumia kwa kujiletea nyenzo muhimu ikiwemo silaha kuitoka Omdurman na maeneo mengine mawili yanayounda eneo kubwa la Khartoum.

Wapiganaji wa  RSF, ambao wamekuwa wakidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu baada ya kuzuka mapigano katikati mwa  Aprili, walijibu mashambulizi hayo kwa nguvu, na kusababisha mapigano makali katika vitongoji vya makazi na watu kupoteza maisha na wengine kuyakimbia makazi yao. Wanaharakati katika eneo la mashariki mwa Omdurman walisema takriban watu tisa walikuwa wameuawa.

Hali mbaya katika eneo la Omdurman.

People watch as smoke rises during clashes between the army and the paramilitary Rapid Support Forces (RSF), in Omdurman
Baadhi ya wakazi wa Omdurman wakishuhudia hali ya mashambulizi katika viunga vya mji wao.Picha: Mostafa Saied/REUTERS

Akizungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la Uingereza Reuters mkazi mmoja mwenye umri wa miaka 52, Nader Abdullah amesema hali ya Omdurman inatisha, milio ya risasi na sauti za mizinga na mashambulizi ya angani yamekuwa yakisikika. Alisema kumekuwa na miripuko ya mabomu kutoka kila upande.

Akiwa njiani akitumia usafiri wa punda kuelekea Chad, Mkimbizi wa Sudan aliyetambulishwa kwa jina moja Khamis alisema "Hali ni ngumu. Kuna mashambulizi ya usiku, wanapiga watu na kuchukua pesa zao. Ili kujinusuru na hali hiyo, lazima ulipe pesa. Hiki ndicho kinachotokea:” Alisema mkimbizi huyo.

Kiini cha machafuko ya Sudan.

Vita vya Sudan vilizuka miaka minne iliyopita baada ya kupinduliwa kwa Omar al-Bashir wakati wa vuiguvgu la wananchi, na muendelezo wake ukawa hali iliyojitokeza sasa ya mvutano kati ya jeshi na RSF. Ambapo pande zote mbili kwa pamoja zilishiriki mapinduzi mwaka 2021, lakini zimeshindwa kuelewana kuhusu mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.

Pande zote mbili zimedai kupiga hatua za  kijeshi katika siku za hivi karibuni ingawa hakuna dalili za mafanikio ya wazi. Juhudi zinazoongozwa na Saudi Arabia na Marekani ili kupata usitishaji wa mapigano zipo katika mkwamo.

Soma zaidi:OCHA: Watu milioni 3 wameyakimbia makaazi yao kutokana na vita nchini Sudan

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mapigano haya ya sasa ya Sudan yamesababisha zaidi ya watu milioni 4 kuyahama makazi yao, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 900,000 ambao wamekimbilia mataifa jirani ambayo hata hayo pia yanakabiliwa na machafuko na migogoro ya kiuchumi.

Chanzo: RTR