1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

UNICEF: Ukeketaji wanawake waathiri wanawake milioni 230

Tatu Karema
8 Machi 2024

Ripoti mpya ya UNICEF, imesema idadi ya wanawake walioathirika kutokana na ukeketaji imefikia milioni 230 kote duniani, hili likiwa ongezeko la asilimia 15 tangu mwaka 2016

https://p.dw.com/p/4dIeU
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la UNICEF akizungumza wakati wa mkutano wa wanahabari mjini Kabul nchini Afghanistan mnamo Februari 25, 2022
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la UNICEF - Catherine RussellPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Claudia Coppa, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo ya UNICEF, iliyotolewa Alhamisi, siku moja kabla ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake,  amesema takwimu hiyo ni ya juu mno kuwahi kushuhudiwa na kuongeza kuwa ni habari mbaya.

Juhudi za kukabiliana na ukeketaji wanawake zinapaswa kuimarishwa

Coppa amesema kuwa juhudi zinapaswa kuongezwa mara 27 zaidi ya kiwango cha sasa kutokomeza utaratibu huo wa ukeketaji wanawake kufikia mwaka 2030 kama ilivyoratibishwa katika agenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.

Kubadilisha desturi kutachukuwa muda

Coppa ameongeza kuwa ijapokuwa mitazamo inabadilika , ukeketaji wanawake umekuwa ukifanyika kwa miongo kadhaa sasa hivyo basi kubadilisha desturi za kijamii kuhusiana na utaratibu huo itachukuwa muda.

Soma pia:Kenya: Kampeni ya kukabiliana na ukeketaji wazinduliwa

Coppa pia amesema kuwa katika baadhi ya jamii kwa mfano, ukeketaji wanawake unachukuliwa kama utamaduni wa kudhibiti masuala mbali mbali yanayohusiana na hali ya kuwa mwanamke.

Ufaransa yapitisha sheria ya kuruhusu uaviaji mimba

Katika kura ya kihistoria siku ya Jumatatu, mabunge yote mawili ya Ufaransa yaliidhinisha uaviaji mimba kama haki ya kisheria , hatua iliyopokelewa kwa shangwe na watetezi wa haki za wanawake.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza na wanahabari mnamo Desemba 9, 2021
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AP Photo/picture alliance

Hafla ya kushuhudia hatua hiyo kuwa ya kisheria imepangiwa leo ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, na inakuja mwaka mmoja baada ya Rais Macron kuahidi kuchukuwa hatua hiyo.

Hatua hiyo inaungwa mkono na raia wengi wa Ufaransa ijapokuwa kuna baadhi ya watu wanaoipinga.

Ufaransa yataka sheria ya uaviaji mimba itumike Ulaya

Siku ya Jumatano, msemaji wa serikali ya Ufaransa Prisca Thevenot, alisema kwamba Ufaransa lazima sasa itetee sheria hiyo hadi katika ngazi ya Umoja wa Ulaya.

Thevenot amesema kwamba mnamo mwaka 2022, Rais Macron alisema kuwa alitaka kuongeza haki hiyo ya uaviaji mimba katika mkataba wa haki za kimsingi za Umoja wa Ulaya.

Human Rights Watch yasema haki za wanawake zimekandamizwa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, HRW limesema kuwa serikali nyingi zinazohofia mshikamano na hatua za pamoja za wanawake, zimekandamiza haki za kujieleza kwa wanawake kupitia vikwazo mbali mbali, kampeini za kuharibia sifa na mashtaka ya jinai.

Soma pia:Baraza la usalama la UN lashinikizwa kuingilia kati ukandamizaji wa wanawake unaozidi nchini Afghanistan

HRW imetolea mfano mataifa kama vile Afghanistan na Iran, ambapo wanawake wanakamatwa na kuzuiwa kiholela na pia kulazimishwa kutoweka pamoja na kuteswa kutokana na harakati zao.

HRW yasema mitandao ya kijamii yachangia katika ukandamizaji wanawake

HRW imesema kuwa  kampuni za mitandao ya kijamii, hazijachukuwa hatua za kutosha kuwalinda wanawake dhidi ya vurugu za mitandaoni hivyo basi kuchangia katika ukandamizaji wa uhuru wa wanawakekujieleza katika mitandao hiyo.

HRW imesema kuwa siku ya leo kuna mengi ya kusherehekewa na mengi ya kuomba na kuwataka wanawake kutumia haki yao ya kujielezea na kusikika.