1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani matumizi ya nguvu Myanmar

Grace Kabogo
22 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani matumizi ya nguvu yanayofanywa na waliohusika na mapinduzi ya kijeshi Myanmar na amelitaka jeshi kusitisha mara moja ukandamizaji na kuwaachilia huru wafungwa. 

https://p.dw.com/p/3phCM
Deutschland UN-Generalsekretär Guterres im Bundestag
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Akizungumza Jumatatu katika mkutano wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Guterres amelitolea wito jeshi la Myanmar kuacha ukandamizaji mara moja, kuwaachia wafungwa na kukomesha ghasia.

''Nautaka uongozi wa kijeshi kuheshimu haki za binaadamu na matakwa ya watu yaliyowekwa katika uchaguzi wa hivi karibuni,'' alifafanua Guterres.

Demokrasia inakandamizwa

Katika mkutano huo unaofanyika mjini Geneva kwa njia ya video, Guterres amesema wameshuhudia ukandamizaji wa demokrasia, matumizi ya nguvu na ukatili, watu kukamatwa kiholela na mashambulizi dhidi ya vyama vya kiraia.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia pia ukiukaji mkubwa wa jamii ya watu wachache bila ya wahusika kuwajibishwa, ikiwemo kile kinachoitwa mauaji ya kikabila wa jamii ya Warohingya.

Deutschland Pressekonferenz Maas zu Bekämpfung des Terrors in der Sahelzone
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko MaasPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema Umoja wa Ulaya unaweza kuiwekea vikwazo Myanmar kama hatua ya mwisho, baada ya jeshi kufanya mapinduzi na kuwakandamiza wapinzani wa serikali.

Maas ameyatoa matamshi hayo baada ya kuwasili Brussels, kabla ya mkutano utakaowashirikisha mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka nchi za Umoja wa Ulaya unaofanyika siku ya Jumatatu. Mkutano huo utahudhuriwa pia na Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken.

Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amesema hawawezi kusimama na kuangalia na kwamba watatumia njia zote za kidiplomasia kushinikiza kuzuia kuenea kwa ukandamizaji Myanmar, lakini pia kama uamuzi wa mwisho wa kuweka vikwazo kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar.

Soma zaidi: Ulaya yaungana dhidi ya mapinduzi ya kijeshi Myanmar

Wizara ya mambo ya nje ya Myanmar imejibu kwa kuushutumu Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa za kigeni kwa kuingilia waziwazi masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Myanmar Myitkyina | nach Militärputsch | Protest
Waandamanaji wa MyanmarPicha: REUTERS

Wiki tatu baada ya kuchukua madaraka, utawala wa kijeshi wa Myanmar umeshindwa kuzuia maandamano ya kila siku na harakati za uasi wa raia zinazotaka serikali irejeshwe kwa utawala wa kiraia na kuachiwa huru mwa kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, Aung San Suu Kyi.

Siku ya Jumamosi watu wawili waliuawa baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji kwenye mji wa Mandalay na mwanamme wa tatu alipigwa risasi kwenye mji wa Yangon.

Utawala wa kijeshi umewaonya waandamanaji kuacha kuwachochea watu kutumia njia ya makabiliano ambayo itawasababishia kupoteza maisha.

Mapema leo, waandamanaji hawakutishwa onyo hilo, ambapo maelfu ya watu wameandamana kwenye mji wa Yangon, ambao ni mkubwa na kivotu cha biashara nchini Myanmar.

(AFP, AP, Reuters)