Ujerumani yatoa msaada zaidi kupambana na janga la njaa
8 Agosti 2011Westerwelle, amesema, serikali ya Ujerumani itaimarisha msaada wake ili kurahisisha maisha ya wakimbizi, na hasa wanaotokea Somalia. Akaongezea, hivi karibuni pia, mjumbe maalum wa masuala ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, Walter Lindner, atafanya ziara nchini Tanzania, Uganda na Kenya. Nchini Kenya atatembelea pia kambi ya wakimbizi ya Dadaab, iliyo kubwa kabisa duniani.
Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi-UNHCR- limesema kuwa leo ndege itapeleka msaada wa dharura mji mkuu wa Somalia Mogadishu. Hii ni mara ya kwanza tangu miaka mitano, kwa UNHCR kufanya operesheni kama hiyo.
Kwa mujibu wa shirika hilo, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, hadi Wasomali 100,000 wamekimbilia Mogadishu kutafuta chakula, maji na makaazi. Umoja wa Mataifa umesema, zaidi ya watu milioni12 katika Pembe ya Afrika wanahitaji msaada wa dharura kwa sababu ya ukame mbaya kabisa kutokea, tangu miongo kadhaa.
Inatathminiwa kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, zaidi ya watoto 29,000 waliokuwa chini ya umri wa miaka mitano wamefariki kwa sababu ya njaa na ukame katika Pembe ya Afrika.