1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakataa mtihani wa ujuzi kwa madereva wazee

Oliver Pieper | Iddi Ssessanga
1 Aprili 2024

Mataifa mengi barani Ulaya na kote duniani hutahini mara kwa mara ujuzi wa kuedesha magari wa watu wenye umri mkubwa. Lakini mitihani kama hiyo ni ya hiari nchini Ujerumani. Je, hiyo inaweza hatari ya kiusalama?

https://p.dw.com/p/4eHLH
DW l Ukaguzi wa uwezo wa kuendesha mjini Cologne
Peter Mecking alifanya mtihani wake wa ukaguzi wa uwezo wa kuendesha mjini ColognePicha: Oliver Pieper/DW

Akiwa usukani kwa zaidi ya miaka 50, Peter Mecking hajawahi kusababisha ajali, na angependa rekodi hiyo iendelee. Sasa, akiwa na umri wa miaka 70, kwa hiari amefanya uchunguzi unaoitwa "ukaguzi wa utimamu wa uendeshaji." Aliendesha Cupra yake nyekundu kuzunguka jiji lake la nyumbani Cologne kwa dakika 45, chini ya uangalizi wa karibu wa mwalimu wa udereva Dominik Wirtz.

Mecking kwa ujumla huendesha takriban kilomita 100 (maili 62) kwa siku. Kwake, mtihani ulikuwa jambo la kweli.

"Nafanya mtuhani huu kwa sababu inafika wakati unapaswa kuacha kuendesha, kutokana na kupungua kwa utendaji wa kiakili na kimwili," aliiambia DW. "Na kama mtu angeniambia niache kuendesha gari, ningekubali hilo pia. Kwa sababu nitakuwa nikijiweka hatarini mwenyewe na wengine barabarani."

Soma pia: Ujerumani hatarini kupoteza sifa ya utengenezaji magari

Kwa ajili ya mtihani huo, mwalimu wa udereva Wirtz alimuongoza Mecking kupitia mitaa ya Cologne, na kisha hadi kwenye barabara kuu. Alitazama ikiwa Mecking alikuwa anazingatia ukomo wa kasi, akitumia vichochoro vizuri na kuweka umbali salama kutoka magari yaliyokuwa mbele. Na pia kama alikuwa anaheshimu haki ya njia na kuonyesha kuzingatia waendesha baiskeli, skuta za umeme na watembea kwa miguu.

Mecking alifaulu jaribio hilo la dakika 45 kwa kujiamini. Ustadi wake wa kuendesha gari ulisifiwa na mwalimu, ambaye ushauri wake pekee ulikuwa kwamba mzee huyo wa miaka 70 anapaswa kuangalia maeneo yake yasiyoonekana kupitia kioo mara nyingi zaidi.

DW l Ukaguzi wa uwezo wa kuendesha mjini Cologne
Peter Mecking akiwa kwenye mtihani wa majaribio ya uwezo wa kuendesha gari mjini Cologne.Picha: Oliver Pieper/DW

Mamilioni ya madereva wazee nchini Ujerumani

Watu milioni kumi walio na umri wa zaidi ya miaka 65 wana leseni ya udereva nchini Ujerumani, na zaidi na zaidi kati yao wanakaguliwa ujuzi wao wa kuendesha gari kwa hiari. Lakini wakufunzi wa udereva hawawezi kuwanyang'anya leseni, ikiwa wanafikiri inahitajika -- wanaweza tu kutoa maoni.

"Kwa sasa ninasimamia mitihani mwili ya udereva wa wazee kwa wiki," Wirtz aliiambia DW. "Watu wanaofanya mtihani ni watu wenye akili timamu na wenye mawazo wazi -- wako wazi kukosolewa -- nawaambia wengi kwamba wanaweza kuendelea kuendesha gari. Ni watu wasiokuja ndiyo tatizo. Wanakaa chini ya rada. "

Mjadala kuhusu majaribio ya lazima ya madereva wazee ulipamba moto hivi karibuni nchini Ujerumani, baada ya mzee wa miaka 83 mjini Berlin kuendesha gari kwenye njia ya baiskeli ili kukwepa msongamano wa magari, na kusababisha ajali ambapo mama na mtoto wake wa miaka 4 waliuawa.

Wirtz alisema mara kwa mara aliwajaribu watu ambao hawapaswi tena kuwa nyuma ya gurudumu. "Kulikuwa na ukaguzi mara mbili ambao baada yake nililazimika kuwajulisha wazee kwamba isingekuwa vizuri waendelee kuendesha gari. Katika tukio moja, mtu huyo alisimamisha gari wakati taa ya trafiki ilikuwa ya kijani [...] na ilipogeuka kuwa nyekundu, alitaka kuendesha gari kwenye makutano." "Ninapowapa maoni kama hayo, huwa yanawaumiza sana," aliongeza.

Changamoto kubwa zinazowakabili madereva wazee ni kulazimika kutazama kila wakati magari yote mara moja, uwezo wa kuzingatia na wakati wa kuchukuwa hatua.

Soma pia: VW yaamuriwa kulipa fidia kashfa ya 'dieselgate'

Hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulipendekeza vipimo vya lazima vya afya kwa madereva wazee, ikiwa ni pamoja na kupima uono na kusikia kila baada ya miaka mitano kwa madereva wenye umri wa zaidi ya miaka 70. Lakini pendekezo hilo lilikataliwa na Bunge la Ulaya mjini Strasbourg mwishoni mwa Februari, ambayo sasa ina maana kwamba nchi za Umoja wa Ulaya zinaweza kuamua kama wanataka kuanzisha majaribio ya lazima. Ujerumani, hasa, iliibua pingamizi dhidi ya pendekezo hilo.

DW l Majaribio ya uwezo wa kuendelea kuendesha gari
Mkufunzi wa udereva Dominik Wirtz (kushoto) anafikiri kwamba wazee ambao hawaji kwa ajili ya mtihani wa hiari ndiyo tatizo kuliko wale wanaofanya hivyo.Picha: Oliver Pieper/DW

"Hatuwezi kuweka kanuni za serikali badala ya wajibu binafsi wa watu," alisema Waziri wa Uchukuzi wa Ujerumani Volker Wissing, kutoka chama cha Free Democratic (FDP). "Na hatuwezi kulalamika juu ya vikwazo vya ukiritimba, wakati huo huo tukiunda urasimu mpya, usio wa lazima."

Katika maeneo mengi, ukaguzi wa afya ni wa kawaida

Msimamo wa Ujerumani juu ya ukaguzi wa lazima haukuwa maarufu kwa nchi nyingi jirani. Ukaguzi wa afya kwa madereva wakuu kwa muda mrefu umekuwa wa kawaida katika nchi 14 za EU.  Nchini Uhispania, mtihani wa lazima unahitajika kila baada ya miaka mitano kuanzia umri wa miaka 65. Katika Jamhuri ya Czech, upimaji huanza kwa miaka 60. Nchini Ureno, inahitajika kutoka miaka 50.

Madereva wazee huchunguzwa hasa nchini Italia, nchi inayopenda magari, na hata kuna ukaguzi wa lazima wa afya kwa madereva walio na umri wa chini ya miaka 50. Inahitajika tena baada ya miaka 10, na kisha kila baada ya miaka mitano.

Wakati madereva wanapofikia miaka 70, mtihani ni wa lazima kila baada ya miaka mitatu, na baada ya 80, kila baada ya miaka miwili. Watu walio na umri wa zaidi ya miaka 80 lazima pia wawasilishe cheti cha matibabu kinachothibitisha kuwa hawana ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa moyo. Japani huwapima madereva wazee hata kwa dalili za matatizo ya akili.

Wizara ya Uchukuzi ya Ujerumani na ADAC -- chama kikubwa zaidi cha magari barani Ulaya -- wote wamesema wazee wana uzoefu zaidi wa kuendesha gari, na kwamba takwimu za ajali zilizochapishwa na Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho la Ujerumani zinaweka ujuzi wao katika mtazamo chanya.

Bunge la Ulaya| Kikao cha Mjadala - Kikao cha kupiga kura
Bunge la Ulaya lilipiga kura dhidi ya kuanzisha mtihani wa lazima kwa wazee, ingawa nchi nyingi za Umoja wa Ulaya tayari zinaoPicha: Frédéric Marvaux/European Union

Takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa nchini Ujerumani madereva 77,700 wenye umri wa zaidi ya miaka 65 walihusika katika ajali zilizosababisha majeraha ya kibinafsi, sawa na asilimia 15 ya ajali zote zilizosababisha majeraha mwaka huo. Lakini wazee wanachangia asilimia 22 ya watu wa Ujerumani, ambayo ni asilimia kubwa zaidi.

Je, hilo linathibitisha kwamba madereva wazee si hatari kubwa ya usalama barabarani? Zingatia uchambuzi mwingine wa Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho, ambayo inasimulia hadithi nyingine: wakati madereva wenye umri wa zaidi ya miaka 75 wanaposababisha ajali, wanawajibika karibu asilimia 77 ya wakati. Hiyo ni asilimia kubwa kuliko ile ya madereva wanagenzi wenye umri kati ya miaka 18 na 20.

Mtihani wa lazima wa udereva baada ya 75?

Kirstin Zeidler, ambaye anafanya utafiti wa ajali kwa ajili ya makampuni ya bima, anaamini "kukagua uwezo wa uendeshaji" wa dakika 45 kwa hiari inapaswa kufanywa kuwa ya lazima kwa watu wenye umri wa miaka 75, na inapaswa kuitwa "uendeshaji wa mrejesho."

"Haihusu kuwanyang'anya watu leseni ya udereva," aliiambia DW. "Kinyume chake: inakusudiwa kusaidia watu kudumisha usafiri wao, kuwasaidia kuendelea kuendesha gari kwa muda mrefu iwezekanavyo, huku wakiwapa taarifa juu ya jinsi inavyofanya vizuri, na sio kujihatarisha wao wenyewe au wengine."

Soma pia: Mkutano wa masuala ya Diesel wakubaliana

Alisema, kwa mfano, kwamba wakufunzi wa udereva wanapaswa kuwapa wazee aina ya ushauri ambao Wirtz huutoa: usiendeshe usiku au nyakati za shughuli nyingi, usiendeshe katika miji mikubwa. Badala yake, bakia kwenye njia zinazojulikana -- kwenda kwa daktari, duka la dawa au Supermarket.

Lakini kipengele kimoja cha majaribio ni kikubwa. Mzee akipoteza leseni yake ya udereva, inaweza kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha yao -- wanapoteza uhuru, na katika baadhi ya matukio wanapoteza udhibiti wa maisha yao.

Ujerumani l Dr. Volker Wissing, Waziri wa Shirikisho wa Dijitali na Uchukuzi
Waziri wa Uchukuzi wa Ujerumani Volker Wissing anafikiri vipimo vya lazima vya kuendesha gari kwa wazee vinaweza kusababisha urasimu usio na maanaPicha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Zeidler ana pendekezo la majaribio ya lazima. "Nchi nyingine zina ukaguzi wa afya ya kimatibabu unaofanywa katika ofisi ya daktari. Tunaamini kuwa njia hiyo si sahihi," alisema, akieleza kuwa matatizo ya kuendesha gari yalikuwa ni matokeo ya kupungua polepole kwa uwezo wa utambuzi kuliko afya ya kimwili. Kuendesha gari vizuri kulitegemea "kutambua hali na kuitikia haraka," alielezea.

"Tunapaswa kuangalia tabia na ujuzi wa kuendesha gari katika hali mazingira ya trafiki," alisema.