1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yafungishwa virago na Spain bao 1:0

8 Julai 2010

Ujerumani na Uruguay kuania mshindi 3.

https://p.dw.com/p/OE0j
Shabiki wa Ujerumani aangua kilioPicha: AP

FINALI SPAIN DHIDI YA HOLLAND:

Finali ya Kombe la dunia 2010 Jumapili hii huko City Stadium,Johannesberg,itakua kati ya mabingwa wa ulaya-Spain na Holland. wakati Holland.Hii itakuwa finali yao ya 3 Holland baada ya ile ya 1974 hapa Ujerumani na 1978 huko Argentina na ya kwanza kwa Spain. Yeyote kati ya timu hizi mbili atakaetoroka na taji Jumapili hii, itakuwa mara ya kwanza kutrwaa Kombe la dunia.

Mashabiki wa Ujerumani, baada ya vilio vya usiku mzima, wameshafuta machozi yao kwa pigo la jana la bao 1:0 kutoka Spain. Na wale ambado bado wamekasirika , wanaandaa karamu maalumu ya "paela" aina ya pilau ya kispain kumpika hapo Jumapili usiku yule pweza "Paul "alieagua ushindi wa Spain, ingawa hakuagua angeishia kuliwa yeye katika karamu ya kisasi cha wajerumani Jumapili hii.

Mlinzi wa FC Barcelona,Carles Puyol, aliwatilia Wajerumani kitumbua choa mchanga kwa bao lake la dakika ya 73 ya mchezo na kuifungulia Spain, mlango kucheza finali ya Kombe la dunia Jumapili hii na Holland,ilioipiga kumbo juzi,Uruguay, timu ya mwisho ya kanda ya Amerika Kusini katika Kombe hili la dunia.

Kwavile, hakuna hata moja kati ya timu hizi 2 iliowahi kutwaa Kombe la dunia, mshindi yeyote huko Soccer City Stadium, Johannesberg, ataandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya ulaya kutwaa Kombe la dunia nje ya bara lao.

Ushindi wa Spain dhidi ya Ujerumani, ulistahiki kwavile, Ujerumani, jana ilishindwa kucheza mchezo wake wa kushambulia uliowaangusha waustralia, Waingereza,Waargentina na Waghana.

UJERUMANI YAFUTA MACHOZI:

Hata hivyo, wakifuta machozi wajerumani, wanafurahia kuona timu yao imecheza uzuri sana katika Kombe hili la dunia kuliko ilivyotazamiwa.Mshindi Jumapili hii, atajiunga na kikosi cha mataifa ya Ulaya yaliotawazwa mabingwa wa dunia:Itali mara 4;Ujerumani, mara 3,Uingereza mara 1 na Ufaransa mara 1.

Kwa kanda ya Amerika Kusini,Brazil mara 5,Argentina,mara 2 na Uruguay mara 2.

UJERUMANI DHIDI YA URUGUAY:

Ujerumani ,sasa itakumbana na Uruguay, Jumamosi, usiku kuania nafasi ya 3 -iliomalizia Kombe lililopita la dunia nyumbani,2006.Nahodha wa Ujerumani,Philipp Lahm,aliekorofishana na nahodha wa zamani Michael Ballack, kuhusu nani kati yao abakie na wadhifa huo, alisema,

"Tumevunjika moyo sana hivi sasa.Tulipanga kufika mbali zaidi hii leo,lakini hatukuweza." Alisema Philipp Lahm.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw,ametoa pongezi kwa waspain.Alisema,

"Tumevunjika moyo na tuna huzuni,lakini Spain, ilicheza vizuri kabisa."

PWEZA PAUL HAKUAGUA KUGEUKA MHANGA

Ama kwa mashabiki wa Ujerumani nyumbani, kuna wale waliokasirishwa sana na uaguzi wa "Paul", ni jina la yule pweza alieagua mara zote ushindi wa Ujerumani kwa kutambaa katika kisanduku chenye bendera ya Ujerumani.Kwa changamoto ya jana,alihamia katika kisanduku chenye bendera ya Spain.Lakini, umaarufu wake na mapenzi yake yaliishia firinmbi ya mwisho kwa kuagua matokeo sawa sawa kwa mara nyengine tena.

Kwavile, mkuki wanasema, ni kwa nguruwe kwa binadamu unauma, kuna shauri sasa la kumkanga "Paul"-pweza huyo na kuandaa pilau ya kispain-maarufu kwa jina la "paela".Natumai,kabla hawakumkangaa Paul,wasubiri aague finali ya Jumapili itamalizika vipi .Kwani, nani ajuwae,pengine, atahamia kisanduku cha Holland na kuwalipizia Wajerumani kisasi chao.Je, hiyo itatosha kuepuka paela`?

Mwandishi: Ramadhan Ali/AEFPE/DPAE

Uhariri:Abdul-Rahman