Syria kupata mpatanishi mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Syria kupata mpatanishi mpya

Mwanadiplomasia mkongwe na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Algeria Lakhdar Brahimi, anatarajiwa kuwa mpatanishi mpya wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuchukua nafasi iliyoachwa na Kofi Annan.

default

Lakhdar Brahimi

Wakati huo huo, vikosi vya serikali nchini Syria vimewafurusha tena waasi katika mji wa Aleppo huku Umoja wa Mataifa ukizidi kuonyesha wasiwasi kuhusu machafuko hayo.

Waasi wakiwa kwenye mapambano ya Aleppo nchini Syria.

Waasi wakiwa kwenye mapambano ya Aleppo nchini Syria.

Majadiliano bado yanaendelea juu ya wajibu wa mpatanishi huyo namna ambavyo umoja wa mataifa utafanya kazi zake Syria kutokana na ongezeko la machafuko. Mamlaka ya ujumbe wa amani wa umoja wa mataifa nchini humo itafikia tamati tarehe 20 mwezi huu.

Duru za kidiplomasia zinasema kuwa tangazo rasmi la kuteuliwa huko kwa Brahimi mwenye umri wa miaka 78 linatarajiwa kutolewa mapema wiki ijayo. Kiongozi huyo ndiye chaguo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon. Duru hizo zinaarifu kuwa mambo yanaweza kubadilika katika dakika za mwisho ikiwa nchi ina wasiwasi na uteuzi au muhusika mwenyewe aliyeteuliwa ana wasiwasi na nafasi aliyopewa.

Wasifu wa Brahimi

Brahimi amewahi kuwa mpatanishi wa umoja wa mataifa nchini Afghanistan baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani, pamoja na Iraq baada ya uvamizi wa Marekani kwenye taifa hilo uliomuondowa Saddam Hussein.

Mashambulizi mjini Aleppo, Syria

Mashambulizi mjini Aleppo, Syria

Ameshiriki pia katika masuala ya usuluhishi nchini Afrika ya Kusini katika miaka ya mwanzo wakati nchi hiyo ilipokuwa ikiachana na utwala wa kibaguzi. Amehudumu nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria katika kipindi cha 1991 hadi 1993.

Akitangaza kujiuzulu kwake siku kadhaa zilizopita, Kofi Annan alilinyooshea kidole baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa ndiyo chanzo cha hatua yake hiyo lakini akasema kuwa huenda atakayemrithi akawa na bahati na kufanikiwa.

Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, alisema wiki iliyopita kwamba anaachia ngazi kama mpatanishi wa mzozo wa Syria kwa kuwa hakuweza kufanya kazi yake kutokana na kutokuelewana kwa wananchama wa baraza la usalama.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice

Wakati hayo yakiendelea waasi wamerejea tena katika mapambano muda mfupi uliopita kwenye wilaya ya Salaheddine mjini Aleppo.

Kamanda wa waasi hao Hossam Abu Mohammed ameapa kuwa wapiganaji wake watapambana hadi dakika ya mwisho. Umoja wa Mataifa umesema kuwa namna vita hivyo vinavyoendelea hakutakuwa na mshindi.

Balozi wa Marekani kwenye umoja huo Suzan Rice amesema kuwa timu ya waangalizi haiwezi kufanya kazi katika hali hiyo

Hapo awali vikosi vya Rais Bashar al Assad viliwatimua waasi hao kwenye mji huo. Watu 250 wanaarifiwa kuuawa katika kwenye eneo hilo kuanzia juzi hadi leo.

Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com