1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti: Mabadiliko ya hali ya hewa yalisababishwa na binadamu

Maja Dreyer16 Novemba 2007

Wiki tatu kabla ya mkutano wa kilele kuhusu ulinzi wa hali ya hewa utakaofanyika kisiwani Bali, Indonesia kuanzia tarehe 3 Disemba, wajumbe wa baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya hali ya hewa walikubaliana juu ya ripoti inayokusanya yale yaliyoandikwa katika ripoti nyingine tatu zilizotolewa awali. Hati hiyo ambayo inatajariwa kupitishwa kesho inatoa msingi wa sera za hali ya hewa kwa miaka ijayo na hivyo kuwa msingi wa mazungumzo ya Bali.

https://p.dw.com/p/CImd
Ujoto utaongezeka zaidi duniani
Ujoto utaongezeka zaidi dunianiPicha: DLR

Rasimu iliyokubaliwa na wataalamu baada ya mazungumzo marefu inatoa onyo kwamba ongezeko la ujoto duniani linaweza kuwa na matokeo mabaya ambayo hayataweza kubadilishwa tena. Ripoti hiyo ya Halmashauri ya kimataifa inayojihusisha na Mabadiliko ya Hali ya Hewa, IPCC, inatoa picha ya hali halisi ya tatizo la ongezeko la ujoto ikilenga kutoa muelekeo kwa wale wanaoamua juu ya sera za mazingira katika muda wa miaka mitano ijayo.

Yale yanayofanywa na binadamu yanaweza kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayawezi kupinduliwa tena, ripoti inasema. Wakati huo huo, wataalamu walikubaliana kwamba mabadiliko yaliyotokea katika miaka 30 hivi ya nyuma yalisababishwa hasa na binadamu – jambo ambalo halikukubaliwa na wanasiasa kadhaa.

Ripoti ya kurasa 20 ambayo inajumlisha ripoti nyingine tatu juu ya hali ya hewa inatarajiwa kupitishwa kesho, na halafu kutolewa hadharani kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao pia utahudhuriwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon. Tayari katika kufungua mkutano huu wa Valencia mwanzoni mwa wiki hii, Katibu mkuu huyu alisisitiza juu ya umuhimu wa suala hilo hapo aliposema: “Ni hali ya dharura na inabidi tuchukue hatua kwa haraka na kuwa na nia imara ya kisiasa. Tunahitaji jibu la kisiasa kutoka kwa viongozi wote ulimwenguni.”

Hata hivyo, kwenye mkutano huu wa Valencia ambapo wajumbe wa serikali wa zaidi ya nchi 100 walihudhuria kulitokea migogoro kadhaa. Hususan wajumbe wa Marekani walipinga sana kutumika kwa matamshi kwamba mabadiliko ya hali ya hewa hayawezi kupinduliwa wakidai kwamba milima ya barafu iliyoyeyuka inaweza kuwa tena kwa vile maji yanaweza tena kugeuka kuwa barafu.

Naibu waziri wa mambo ya mazingira wa Ujerumani, Bw. Michael Müller, hakuridhishwa na matokeo haya ya mkutano wa Valencia. Alisema, wajumbe wa Marekani walijaribu kuzuia kuwepo shinikizo kubwa kwa wanasiasa kabla ya mkutano wa kikele huko Bali. Licha ya hayo lakini, rasimu iliyofikiwa bado inatoa muelekeo mkali wa kutosha kwa mkutano wa Bali.

Kulingana na utabiri wa wataalamu wa halmashauri hiyo, wastani wa ujoto utazidi kwa nyuzi moja ya Celsius hadi mwaka wa 2100 na kima cha maji kitaongezeka kwa sentimita 18 hadi 59. Mafuriko, vimbunga na ukame utaweza kutokea mara nyingi zaidi. Nchi zote zitaathirika, ripoti hiyo inasema, lakini mzigo utakuwa mkubwa zaidi kwa nchi maskini.

Mkutano wa Disemba kisiwani Bali unalenga kupunguza zaidi utoaji wa gesi chafu baada ya mwaka 2012 wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika.