PDP yakataa kujiunga na Ennahda kuunya serikali Tunisia | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

PDP yakataa kujiunga na Ennahda kuunya serikali Tunisia

Huku matokeo kamili yakisubiriwa na waangalizi wa kimataifa wakiuita uchaguzi wa kwanza wa Tunisia kuwa "huru na wa haki", chama cha Progressive Democratic (PDP) kimekataa kujiunga na Ennahda kuunda serikali ya mseto.

Wafuasi wa Ennahda wakifurahia ushindi wa chama chao.

Wafuasi wa Ennahda wakifurahia ushindi wa chama chao.

Msimamo wa PDP umetangazwa na kiongozi wa chama hicho, Najib Chebbi, ambaye amesema haoni umuhimu wa kushirikiana na Ennahda katika serikali, ingawa hakupinga ushindi wake. Chebbi amesema "PDP haitakuwamo kwenye serikali ili kuipa nafasi Ennahda kutekeleza ilani yake".

Ushindi wa Ennahda haukuwa kwa wapiga kura waliomo ndani ya Tunisia tu, bali hata walioko nje. Nchini Ufaransa, nyumbani kwa Watunisia wapatao 500,000, chama hicho kimejizolea viti vinne kati ya viti 10 vilivyogombaniwa.

Vyama vinavyokifuatia Ennahda ni vya mrengo wa kushoto, Congress for the Republic (CPR), na Ettakatol vilivyopata viti viwili viwili kila kimoja, huku Democratic Modernists kikipata kiti kimoja na mgombea huru, Hashmi Haamdi, akishinda kwa asilimia 10.17, kusini mwa Ufaransa.

Ennahda yaahidi kushirikiana na wote

Maofisa wa uchaguzi wa Tunisia wakihesabu kura.

Maofisa wa uchaguzi wa Tunisia wakihesabu kura.

Kufuatia ushindi huu, meneja kampeni wa Ennahda, Abdel Hamid Jelassi, amesema huo ni ushahidi kuwa chama chake hakifuati Uislamu wa siasa kali, bali kinatafuta maridhiano ya kitaifa.

"Kitu muhimu ni kuwa tumeshiriki kwenye uchaguzi kwa kiwango kikubwa. Ushindi wa chama unaweza lisiwe jambo la muhimu sana. Hata hivyo, tulisema hilo hapo mwanzoni, tukasema wakati wa uchaguzi na leo tunarudia: tutafanya kazi na pande zote, na mirengo yote ya kisiasa. Tutahakikisha uhuru wa watu wote na wa mtu binafsi, uhuru wa mawazo, wa kujieleza na wa kujiunga".

Tume ya Uchaguzi imesema kuwa muelekeo wa matokeo ya kura unaonesha Ennahda ina uwezo wa kushinda nusu ya viti 18 vilivyowekwa kwa ajili wawakilishi wa Tunisia katika nchi za kigeni katika Bunge litakalokuwa na jumla ya viti 217. Vituo vya kupiga kura kwa Watunisia walioko nje viliwekwa Ujerumani, Italia, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Umoja wa Ulaya waridhika na uchaguzi

Mkuu wa chama cha Ennahda, Rashid Ghannoushi.

Mkuu wa chama cha Ennahda, Rashid Ghannoushi.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wamesema kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na wa wazi, ukiacha kile walichokiita "matukio madogo madogo" yasiyo ya kawaida.

"Tume ya Uchaguzi ya Tunisia imeendesha uchaguzi huu kwa uwazi na sisi tumeridhika kwa namna ambavyo upigaji kura katika vituo 97 umefanyika." Amesema mkuu wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Michael Gahler.

Kwa jumla, ushindi wa Ennahda utakaribia asilimia 40 , ambao hata hivyo unakilazimisha kuungana na vyama vingine kuunda serikali. Baada ya PDP kukataa kuungana na Ennahda, vyama vikubwa viwili vinavyoweza kuungana nacho ni CPR cha Munsif Marzouki na Ettakatol cha Mustafa Bin Jaafar.

Kwa vyovyote serikali hiyo itakavyoundwa, uchaguzi huu umeonesha picha nyengine ya mataifa ya Kiarabu na ya Kiislamu, kwani licha ya wafuatiliaji wa siasa kutoka nje ya Tunisia kutokukiamini Chama cha Ennahda kwa hofu ya siasa za Kiislamu, wapiga kura wa Tunisia wameonesha hisia tafauti kwa kukipa kura chama hicho.

Ennahda kinasema kinafuata mfano wa siasa wa chama kinachotawala Uturuki cha AKP, ambacho nacho kinaongoza nchi yenye Waislamu wengi, lakini wanaofuata mfumo wa siasa zisizoelemea dini.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/DPA
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 25.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12ypw
 • Tarehe 25.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12ypw

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com