1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya kijeshi yashambulia makundi ya waasi Mogadishu .

30 Machi 2007

Wanajeshi saba wa Ethiopia wameuwawa huku Mizinga ikiendelea kulipuliwa kwa siku ya pili ya mapigano ambapo wanajeshi wa Somalia na Ethiopia wanawasaka waasi wa makundi ya kiislam. Watu thelathini wameripotiwa kuwawa na wengine mia moja wamejeruhiwa vibaya.

https://p.dw.com/p/CHH5
Waathiriwa wapelekwa kupata matibabu,Mogadishu.
Waathiriwa wapelekwa kupata matibabu,Mogadishu.Picha: AP

Raia mjini Mogadishu hawana amani tena,tangu vita hivi vilipozuka baina ya makundi ya waasi na wanajeshi wa Somalia na Ethiopia . Wengi wao wamesikika wakisema kuwa wanahofia maisha yao, Faisal Jamal mwenyeji wa Mogadishu kusini alisema ``mzinga umeangukia nyumba ya jirani,tunasikia watu wakilia,moto unawaka kila pahali,yaani ukitizama angani unaona tuu mizinga ikiripuka’’.Ndege moja ya kijeshi ya Ethiopia iliyokuwa ikiwashambulia waasi,ililipuliwa kwa mzinga

Vita hivi vilianza wakati wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wanajeshi wa serikali ya mipito ya Somalia walipolipua mizinga dhidi ya waasi siku ya Alhamisi. Na hadi sasa idadi ya majeruhi iliyoripotiwa kuwa mia moja inaendelea kuongezeka huku watu thelathini wakiripotiwa kuuwawa.

Wakaazi wanasema majeruhi hao hawajapata matibabu kwani barabara hazipitik,na vita vinaendelea katika maeneo mbalimbali ya Mogadishu.Nazo Hospitali pia zimejaa maiti na majeruhi

Wapiganaji wa koo ambao awali waliokuwa wakitawala baadhi ya miji nchini Somalia, wamedaiwa kuungana na waasi wa kundi la mahakama za kiislamu na kusababisha vurugu la kivita baina yao na wanajeshi wa Ethiopia na viongozi wa ukoo wa Hawiye ambao ndio ukoo mkubwa zaidi Somalia.

Japo hali hii inaonekana kuwa kikwazo kwa mikakati ya amani,waziri mkuu wa Ali Mohammed Ghedi amesema mkutano wa upatanishi uliotarajiwa kuanza mwezi Aprili utaendelea kama ulivyopangwa na wale viongozi wa mahakama za kiisalmu wanounga mkono maazimio ya amani yalioundwa nchini Kenya mwaka 2004 wataalikwa.

Waziri mkuu Mohammed Ghedi amepinga pia madai ya kuzorota kwa usalama nchini humo,lakini waandishi wa habari walioko Somalia wanasema kuwa mili ya watu imetapakaa katika maeneo kadhaa. Mwandishi mmoja Osman Gabayre alinukuliwa kusema kuwa, aliona mili ya wanajeshi kumi na saba wa Ethiopia wakiwa wamefariki ndani ya gari lao la kijeshi.

Na japo Umoja wa Africa ulituma wanajeshi elfu moja mia mbili kutoka Uganda hali bado ni ileile ya patashika. Kwani wanajeshi hao pia walishambuliwa katika nchi ambayo ilipinga usaidizi wa Umoja wa Mataifa na Marekani miaka kumi na tisa iliyopita tangu vita kuanza.

Mataifa mengine ya Afrika nayo,yanadaiwa kusita kutuma wanajeshi wake kupelekea hali ya ukiukaji wa mapatano ya kukomesha vita

Muda wa serikali ya mpito unatarajiwa kuisha miaka miwli ijayo 2009, ambapo Somalia inatarajiwa kuwa katika hali itakayofanikisha uchaguzi mkuu. Lakini hali inayodhihirika sasa,inahitaji mikakati kabambe ikiwa Somalia itarudi kuwa nchi ya amani.

Isabella Mwagodi