1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Nuklia wa Iran bado unaumiza vichwa vya mataifa husika

9 Machi 2007

Mataifa yenye nguvu duniani yanatafakari juu ya mapendekezo ya vikwazo dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa Kinuklia unaofikiriwa na nchi za magharibi kuwa wa kutengeneza silaha za kinuklia.

https://p.dw.com/p/CHIW
Marais AhmedNejad wa Iran na Gorge Bush wa Marekani
Marais AhmedNejad wa Iran na Gorge Bush wa MarekaniPicha: AP

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia mali zitakazotumika kuendeleza jeshi pamoja na mahusiano ya nje ya benki ya Sepah inayomilikiwa na serikali .

China na Urussi zimepinga hatua kadhaa za kuchukuliwa dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa kinuklia.Hata hivyo nchi hizo mbili ambazo ni wanachama wa kudumu kwenye baraza la usalam la Umoja wa Mataifa zimekubaliana na vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.

Hata hivyo lakini kuna mambo mengi ambayo hayajaafikiwa kuhusiana na azimio la kuiweka vikwazo Iran.

Hakuna tarehe iliyowekwa kwa ajili ya kupiga kura katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa na kwa hivyo azimio la mwanzo halitarajiwi kuidhinishwa hadi wiki ijayo.

Mabalozi kutoka nchi tano wanachama wa Kudumu kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa Marekani Uingereza,Ufaransa,Urussi na China pamoja na Ujerumani walikutana siku ya alhamisi ikiwa ni mara ni ya tatu wiki hii na kupanga kikao kingine hapo jana Ijumaa.

Mjumbe wa Marekani Alejandro Wolff aliwaambia waandishi habari kwamba bado hakuna azimio la kuzungumzia na kwamba walikuwa wanajadiliana juu ya pale walipofikia.

Azimio hilo jipya linafuatia azimio jingine lilloidhinishwa na baraza la usalam la umoja wa mataifa mwezi Desemba 23 ambalo liliiwekea vikwazo vya kibiashara katika bidhaa nyeti za Nuklia pamoja na technologia pamoja na kusimamisha akaunti za benki za watu mashuhuri nchini Iran makundi na biashara nchini humo.

Hatua hiyo ilikusudiwa kuifanya Iran ikomeshe urutubishaji wa madini yake ya Uranium ambayo yanaweza kutoa mafuta yanayotumika katika mtambo wa nguvu za umeme au kuweza kutumiwa kutengenezea mabomu lakini Iran ilikataa kuzingatia hilo.

Mapendekezo mapya ambayo yanajadiliwa hivi sasa ni pamoja na kuwekea vikwazo vya lazima vya usafiri,kifedha na kibiashara na vile vile kuongeza idadi ya maafisa wa Iran pamoja na biashara ambazo akaunti zao zitazuiliwa.Makampuni ambayo yatahusishwa ni pamoja na yale yanayodhibitiwa na jeshi na vile vile benki ya taifa ya Sepah.

Urussi na China lakini zimejizuia kidogo kuzungumzia juu ya vikwazo dhidi ya jeshi la Iran..

Lakini kwa Upande wa Marekani tayari utawala wa Bush umeweka viwakwazo vyake binafsi dhidi ya Iran na mnamo mwezi Januari Marekani imezizuia Kampuni zake na raia wake kuendesha biashara na Benki ya taifa ya Iran ya Sepah.

Mapendekezo dhidi ya mpango wa Nuklia wa Iran pia yanataka paweko vikwazo vya kuizuia Iran isisafirishe silaha zake nje lakini nchi hiyo inaweza kuingiza silaha.

Baraza la usalama hadi sasa lakini limeshindwa kufikia makubaliano juu ya kuitia adabu Iran kutoka na Urussi na China kutokubaliana na baadhi ya vikwazo hivyo hasa Sababu kubwa ni kwamba Urussi ambayo vile vile ina,kura ya turufu kama Marekani,Ufaransa,Uingereza na China ni muuzaji mkubwa wa silaha kwa Iran.