1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya Mjini Brussels

19 Julai 2011

Rais Bashar al Assad wa Syria anashinikizwa azungumze haraka na upande wa upinzani na kuanza kutia njiani mageuzi aliyoahidi

https://p.dw.com/p/11yyf
Kutoka kushoto,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Luxembourg,Jean Asselborn,wa Ubeligiji Steven Vackere na Hispania Trinidad JimenezPicha: dapd

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels wanazidi kuitia kishindo serikali ya rais Bashar al Assad wa Syria inayowatumilia nguvu wapenda mageuzi. Mawaziri hao wanaunga mkono vikwazo viimarishwe na kulitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilaani matumizi ya nguvu nchini Syria.

Wengi wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wamemtaka Bashar al Assad ajiuzulu. Alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Sweden, Carl Bildt, aliyesema kinaga ubaga mbele ya waandishi habari na hapa tunanukuu: "Panahitajika utawala mpya. Utawala huu umepoteza imani na uhalali," mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Sweden.

Kwa mujibu wa makundi yanayopigania haki za binaadam,watu wasiopungua1800, wakiwemo raia na vikosi vya usalama, wameuwawa nchini Syria tangu serikali ya rais Bashar al Assad ilipoanza kuwavunja nguvu waandamanaji wanaodai demokrasia mwezi March mwaka huu.

"Tabia hii ya serikali ya Syria haiwezi kukubalika hata kidogo na lazima ilaaniwe na walimwengu", amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, aliyekiri hata hivyo kwamba  bado baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linasita sita na kuna kazi kubwa ya kuweza kulitanabahisha."

Urusi na China zimedhamiria kuzuwia azimio lolote litakalolaani utawala wa Bashar al Assad katika baraza la Usalama.

Außenminister und Vizekanzler Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

Guido Westerwelle amezungumzia nchi nyingi zinazoonyesha wasi wasi kuelekea azimio  la baraza la usalama dhidi ya Syria ambalo litafungua njia kama ile ya Libya, na hasa katika suala la operesheni za kijeshi.

"Halihusiani na maandalizi yoyote ya kuingilia kati", amesisitiza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, na kuongezea tunanukuu: "hapa jumuia ya kimataifa itabidi isake msimamo wa aina moja, sio tu vikwazo, bali pia kisiasa," Mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Alain Juppé, amehoji baraza la Usalama linabidi lipime kile alichokiita "hatari kwa usalama na utulivu wa kimkoa na zaidi kuliko yote ukandamizaji wa nguvu na wa kinyama dhidi ya wananchi wa Syria."

Duru za kuaminika kutoka mjini Brussels zinasema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wanapanga kumtaka "kwa sauti kali" Bashar al Assad azungumze na upande wa upinzani.

Jerusalem mit Felsendom
Jerusalem:Mji unaowakilisha waumini wa Kikristo,kiislam na kiyahudiPicha: picture alliance / abaca

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wamezungumzia pia utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati na kuwatolea mwito Waisraeli na Wapalastina waonyeshe moyo wa uadilifu na kuanzisha upya mazungumzo ya ana kwa ana ya amani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/afp

Mhariri:Miraji Othman