1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya magaidi wa NSU

6 Mei 2013

Kesi ya mauwaji dhidi ya wafuasi 5 wa vuguvugu la chini kwa chini la wazalendo wa kijamaa,hujuma za Israel dhidi ya Syria na mkutano mkuu wa chama cha kiliberali ni miongoni mwa mada zilizopewa umuhimu zaidi magazetini.

https://p.dw.com/p/18SrO
Waandamanaji wanazozana na polisi karibu na lango la kuingilia katika mahakama ya mjini MunichPicha: Getty Images/Alexander Hassenstein

Tuanzie lakini Munich ambako kesi iliyokuwa ikisuburiwa kwa hamu dhidi ya watuhumiwa wa siasa kali ya mrengo wa kulia imeanza hii leo.Gazeti la "Neue Presse" linaandika:

Kesi dhidi ya wafuasi wa vuguvugu la chini kwa chini la wazalendo wa kijamaa-NSU inaizonga jamii na idara za upelelezi,kwa masuala tete:Imekwendaje hata magaidi wakaweza kuuwa miaka nenda miaka rudi nchini Ujerumani?Kwanini waendesha mashtaka waliwatuhumu kwanza baadhi ya wahanga kuwa wanachama wa makundi ya wahalifu?Mahakama inakabiliwa na kitendawili kigumu hasa kwasababu mtuhumiwa mkuu Beate Tschäpe angali bado ananyamaza.Alikuwa msaidizi au mwasisi?Kusema kweli haiingii akilini kwamba alikuwa shahidi tuu wa kundi hilo la wauwaji-lakini jee kuna ushahidi ?

 Mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anamulika jinsi vyombo vya habari vinavyoishughulikia  kesi hii na kuandika:

Si sana kumuona jaji akifuatiliziwa na vyombo vya habari kwa wiki kadhaa-na ikiwa hivyo basi mara nyingi hiyo hutoa ishara mbaya.Hata kumhusu Manfred Götzl hali ndio hiyo hiyo.Mengi yameandikwa kumhusu jaji huyo wa mahakama ya mjini Munich alieifungua hii leo kesi dhidi ya watuhumiwa wa kundi la NSU.Kwa masilahi yawahanga kumi na familia zao na zaidi kuliko yote kwa maslahi ya hadhi ya mfumo wa sheria wa Ujerumani, kilichosalia ni kutaraji kwamba jaji Götzl anastahiki jukumu alilotwikwa.

Kitisho cha kuzidi makali mzozo wa Mashariki ya kati

Damaskus Angriff Israel Beschuss Syrien
Hujuma za madege ya kivita ya Israel dhidi ya mji mkuu wa Syria-DamascusPicha: Reuters

 Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na kitisho cha kuripuka zahma katika eneo la mashariki ya kati baada ya Israel kuihujumu kwa mara nyengine tena Syria.Gazeti la "Nordbayerischer Kurier" linaandika:

Mjini Jerusalem watu wanaamini serikali ya Assad imedhoofika haina tena nguvu ya kujibisha mashambulio.Lakini makombora kwa bahati mbaya hayajakosekana katika eneo hilo.Nchi zenye nguvu na ambazo zinaweza kuzishawishi pande zinazohasimiana zimlaani shetani,zimekaa kimya.Urusi inampatia silaha Assad na Marekani kwa sasa haijajitokeza na juhudi zozote za kidiplomasia.Damascus imeligeukia baraza la usalama la umoja wa mataifa lakini katika taasisi hiyo muhimu ya jumuia ya kimataifa madola yenye nguvu yanashindana.Kwa hivyo ulimwengu uko ukingoni mwa balaa.Walimwegu  hawana la kufanya,wameduwaa na kujionea jinsi balaa linavyozagaa.

FDP wapania kuzusha majabu September mwaka huu

Rainer Brüderle FDP
Mgombea kiti cha kansela wa chama cha FDP Rainer BrüderlePicha: Reuters

 Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mkutano mkuu wa chama cha kiliberali cha FDP uliomalizika jana mjini Nürnberg.Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika:

 Mara ngapi watu wamekuwa wakiashiria FDP kimekwisha?Wachunguzi wa maoni ya umma wanakitaja kuwa chama cha mgawanyiko hata wasanii wa vichekesho wanakiita chama hicho cha kiliberali "sarakasi".Mkutano mkuu wa Nürnberg lakini umedhihirisha FDP kipo.Na ikiwa wapinzani wake wataendelea kupigania kodi za mapato ziongezwe,basi si hasha FDP wakaendelea kuwepo madarakani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu