Hali nchini Thailand bado tete | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali nchini Thailand bado tete

Serikali yakataa kufanya mazungumzo na imewataka waandamanaji wanaoipinga serikali kumaliza vurugu.

default

Wanajeshi wa Thailand wakiwa katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok kwa ajili ya kukabiliana na waandamanaji.

Waandamanaji wanaoipinga serikali nchini Thailand wamesema wako tayari kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo na kutoa mwito kwa mfalme wa nchi hiyo kusaidia kumaliza ghasia zinazoendelea baina ya waandamanaji hao na vikosi vya jeshi, ambazo zimesababisha watu 37 kuuawa.

Mbali na kutoa tangazo hilo la kuwa tayari kufanya mazungumzo na serikali, waandamanaji hao waliuomba Umoja wa Mataifa kuingilia kati kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo, mwito uliokataliwa na serikali ya Thailand. Hata hivyo, akijibu iwapo serikali iko tayari kufanya mazungumzo na waandamanaji hao, msemaji wa serikali ya Thailand, Panitan Wattanayogorn, amesema kuwa ghasia na vurugu dhidi ya vikosi vya jeshi lazima zimalizike kwanza. Amesema kuwa serikali itakuwa tayari kufanya mazungumzo na waandamanaji hao wanaojiita ''mashati mekundu'' iwapo waandamanaji hao wanaoipinga serikali watamaliza vurugu na kuacha kuwashambulia viongozi wa nchi.

Hali hiyo inayaweka mazungumzo hayo njia panda kutokana na kila upande kumtaka mwenzake kuacha vurugu kwanza. Miongoni mwa watu waliouawa ni mwanajeshi wa zamani na kiongozi wa vuguvugu la waandamanaji hao, Meja Jenerali Kahttiya Sawasdipol. Meja Jenerali Sawasdipol amefariki hii leo akiwa hospitalini kutokana na majeraha aliyoyapata wakati alipopigwa risasi kichwani Alhamisi ya wiki iliyopita. Kifo cha kiongozi huyo kimeelezwa kuleta wasi wasi zaidi wa kuzuka ghasia mpya katika taifa hilo lililopo kusini-mashariki mwa Bara la Asia. Katika mji mkuu, Bangkok, waandamanaji hao wameendelea kukabiliana na vikosi vya jeshi katika barabara za mji huo. Serikali imewataka waandamanaji wapatao 5,000 kuondoka katika mitaa ya katikati mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok, vinginevyo watafunguliwa mashitaka ya uhalifu. Wenye hoteli mbalimbali za mji huo wamewataka wateja wao kuondoka katika hoteli hizo, huku shule zikiwa zimefungwa.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa waandamanaji hao, Jatuporn Prompan, amewaambia wafuasi wake kuwa huruma ya mfalme wa nchi hiyo, ndio tumaini pekee la kumalizika kwa mzozo huo wa kisiasa. Mfalme Bhumibol Aduladej wa Thailand amekuwa akitatua mizozo iliyopita katika ufalme wake wa miaka 63. Lakini mfalme huyo, mwenye umri wa miaka 82, amelazwa hospitalini miezi saba sasa na hajazungumzia hadharani kuhusu mzozo unaondelea sasa. Waziri Mkuu wa Thailand, Abhisit Vejjajiva, ameahidi kutowavumilia magaidi wenye silaha wanaotaka kuiangusha serikali yake. Waandamanaji hao, wafuasi wa waziri mkuu wa zamani wa Thailand, Thaksin Shinawatra, aliyeondolewa katika mapinduzi mwaka 2006, wanataka kiongozi huyo arejeshwe madarakani. Pia wanaitaka serikali ilivunje bunge na kuitisha uchaguzi mwingine. Mzozo huo ambao ulianza katikati ya mwezi Machi mwaka huu umesababisha watu 66 kuuawa na wengine zaidi ya 1,600 kujeruhiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/APE)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 17.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NPpQ
 • Tarehe 17.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NPpQ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com