1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni mbaya Somalia.

Halima Nyanza24 Julai 2009

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ametoa mwito kwa nchi zote kutoa msaada wa haraka wa kijeshi kuiunga mkono serikali ya mpito ya Somalia. Wito huo unakuja wakati ambapo watu 46 wameuawa katika mapigano.

https://p.dw.com/p/Iwtl
Hali bado ni mbaya nchini Somalia., wanajeshi wakitanda mitaani.Picha: AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameiomba jumuia ya kimataifa isiyumbe katika kukabiliana na kuongezeka kwa mapigano na kutoa majeshi zaidi, silaha na kuiwezesha serikali ya nchi hiyo.

Mapigano yaliyotokea katikati mwa Somalia na katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu, yamesababisha vifo vya watu 46, ambapo katika katika miji ya Wabho na Mahas mapigano kati ya wapiganaji wa Al Shabaab na kundi la Ahlu Sunna Waljamaa yamesababisha vifo vya watu 31 tangu siku ya Jumatano, huku katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogaduishu, watu 15 wakiuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika mapigano makali yaliyotokea katika wilaya tatu za mji huo.

Aidha wapiganaji wa Al Shabaab, ambao nchi za magharibi zinalizingatia kama kundi la kigaidi, wanadhibiti eneo kubwa kusini na katikati mwa nchi hiyo.

Wakati hali ikiwa bado ni mbaya nchini humo, serikali ya mpito ya Somalia imemteua Abdullahi Mohamed Ali kuwa Waziri wa Ulinzi nchini humo kuchukua nafasi ya Waziri aliyeuawa mwezi uliopita kwa bomu la kujitoa mhanga, shambulio ambalo lilifanywa na waasi.

Akizungumzia kuhusu majukumu yake, waziri huyo ameahidi kutoa kipaumbele katika kuimarisha jeshi la nchi hiyo na usalama wa taifa.

Wakati serikali ikielezea mikakati yake ya kujiimarisha, makundi ya wapiganaji nchini humo nayo pia yametoa taarifa ya kujiimarisha zaidi kwa kuungana.

Wakati huohuo, Umoja wa Afrika umesema unachunguza ugonjwa wa ajabu uliouwa wanajeshi watatu wa Burundi wa jeshi la kulinda amani nchini Somalia, ambapo wengine 18 wamelazwa hospitalini nchini Kenya kutokana na ugonjwa huo.

Jumla ya wanajeshi wa kulinda amani 4,300 kutoka Burundi na Uganda wapo Somalia kuyasaidia majeshi ya nchi hiyo dhidi ya wapiganaji.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, ap, Interview)

Mhariri: Miraji Othman