1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundestag yaidhinisha mfuko wa uokozi wa Ulaya ulio madhubuti

29 Septemba 2011

Bunge la Ujerumani, Bundestag, limepiga kura na kuiamua hatima ya mfuko wa uokozi mahsusi kwa mataifa yanayokabiliana na madeni makubwa na nakisi ya bajeti.

https://p.dw.com/p/12iwJ
Bunge la Ujerumani, BundestagPicha: picture alliance/dpa

Wabunge hao wanaripotiwa kuwa na mitazamo tofauti kuhusu suala hilo, hususan vigezo vitakavyotumiwa kuitoa mikopo, kadhalika kiwango cha fedha. Duru zinaeleza kuwa zoezi hilo linagubikwa na mivutano kati ya wabunge wa muungano tawala wa kansela Angela Merkel wasioliunga pendekezo hilo moja kwa moja.

Upinzani uko ngangari

Mdahalo huo uliofanyika bungeni mjini Berlin umegubikwa na mitazamo tofauti kuhusu hatima ya mfuko wa uokozi mahsusi kwa mataifa yanayokabiliwa na madeni na nakisi ya bajeti barani Ulaya. Hata hivyo , duru zinaeleza kuwa wabunge wa upinzani huenda wakaliunga mkono pendekezo hilo la kuyanyanua mataifa yanayopambana na madeni.

Bundestag Debatte Euro-Rettungsschirm Schuldenkrise Krise Merkel Flash-Galerie
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel:mivutano chamani CDU/CSU inazua mitazamo tofautiPicha: picture alliance/dpa

Ujerumani iliyo na uchumi mkubwa zaidi katika eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro barani Ulaya inalazimika kuchangia kwa kiasi kikubwa zaidi ili kuuimarisha uwezo wa mfuko huo wa uokozi, EFSF. Endapo pendekezo hilo litapata ridhaa ya bunge la Bundestag, Ujerumani itahitajika kuthibitisha kuwa itatoa mikopo ya hadi kiasi ya bilioni 211 badala ya bilioni 123 katika siku zijazo.

Ridhaa na kura ya ndio

Ifahamike kuwa kwa mujibu wa katiba ya Ujerumani, serikali haina ruhusa ya kuchangia fedha zozote kwenye mfuko huo wa uokozi au kufanya mabadiliko yoyote pasina ridhaa ya bunge au kamati yake ya bajeti inapotokea hali ya dharura.

Kiasi ya wabunge 500 kati ya 620 wanatarajiwa kuunga mkono mswada huo ambao umewasilishwa na kujadiliwa kwa kasi bungeni.

Imani na Kansela Merkel

Hata hivyo suala analokabiliana nalo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ni iwapo chama chake kinaweza kupata kura 311 au zaidi ili kiungane na kambi inayouunga mkono mswada wenyewe. Endapo atakitimiza kigezo hicho, ushawishi wake katika muungano tawala utapata sura mpya.

Kwa upande mwengine, kiasi ya wabunge 20 wa muungano tawala huenda wakalisusia zoezi hilo, kuupinga mswada au kutohudhuria kikao chenyewe kabisa kwa sababu za binafsi. Muungano tawala unaoegemea mrengo wa kulia una jumla ya viti 330 katika bunge la Ujerumani, Bundestag.

Bundestag Merkel Rösler
Kansela Angela Merkel (CDU) Westerwelle na Waziri wa Uchumi Philipp Rösler (FDP).Picha: picture alliance/dpa

CDU/CSU njia panda

Kwa upande wake, Horst Seehofer, Waziri Mkuu wa mkoa wa Bavaria aliyepia kiongozi wa chama cha CDU kinachoshirikiana na CSU cha Angela Merkel ni mmoja ya wanaouunga mkono mswada huo kwani ni kipimo cha ushawishi wa Kansela, kisiasa. 

Ifahamike kuwa mwezi wa Julai, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliafikiana katika kikao cha kilele kukiongeza kiwango cha fedha za mfuko huo kutokea Euro bilioni 440 hadi 780.

Masoko na wasiwasi

Wakati huohuo, wasiwasi umetanda katika masoko ya hisa kwasababu ya tatizo jumla la kiuchumi linalolikumba bara la Ulaya. Bei za hisa zinaripotiwa kupungua kwa leo.

Hapo jana Jumatano, serikali ya Finland iliuidhinisha mswada huo wa kuiongeza nguvu ya mfuko wa uokozi hata baada ya kutishia kuwa haitahusika na harakati za kujaribu kuinusuru Ugiriki.

Bundestag Debatte Euro-Rettungsschirm Schuldenkrise Europa Krise Steinbrück
Peer Steinbrück wa SPDPicha: picture alliance/dpa

Hata hivyo, mswada huo unaounga mkono mabadiliko yoyote na kuiamua hatima ya mfuko wa uokozi mahsusi kwa mataifa yanayokabiliana na madeni ya eneo linalotumia sarafu ya Euro sharti upate ridhaa ya serikali za nchi 17 wanachama wa eneo hilo.  

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-DPAE,AFPE, ZDF Multimedia

Mhariri: Miraji Othman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi